Jinsi ya kuacha tabia usiyoipenda
Nilipoanza mkakati wa kuacha kutumia sukari kwenye chai au kahawa, haikuwa kazi rahisi.
Kwa muda mrefu, nilihisi kama adhabu kwangu. Mara kadhaa nilijitahidi kuacha sukari, lakini baada ya siku chache ningejikuta nikisema, “acha nitumie sukari leo kwa mara ya mwisho, kesho nitaendelea na mpango wangu.”
Haikuwa sukari pekee; nililenga pia kupunguza uzito wa mwili, hivyo nikaamua kuacha kunywa soda, hasa Coca-Cola.
Soda hii ilinipa changamoto kubwa kuiacha, kwani mara kwa mara, niliingia kwenye mazingira ambayo yalinifanya nirudi kwenye mazoea yangu ya zamani. Licha ya kuwa na nia thabiti ya kuachana na vinywaji vyenye sukari, kuchukua hatua ya kweli ilikuwa kazi ngumu sana.
Jaribio hili la kuachana na sukari lilinifundisha mambo kadhaa. Kwanza, ingawa nilikuwa na sababu za msingi za kunifanya niache sukari, sikuwa na uwezo wa kuacha.
Uelewa wa athari za matumizi ya sukari kupita kiasi haukusaidia kukata tamaa yangu. Nilijua kuwa matumizi makubwa ya sukari yanachangia kuongezeka kwa uzito wa mwili, jambo ambalo sikutaka.
Hata hivyo, kila niliposhika kikombe cha chai, nilijikuta natumia sukari bila kujua jinsi ilivyotokea. Mara nyingine nilijinyima sukari kwa siku kadhaa, lakini nilipojikuta kwenye mazingira kama kufanya kazi usiku, nilishindwa kujizuia. Mchanganyiko wa njaa na uchovu wa ubongo ulinishawishi kutumia vijiko vya sukari kama njia ya kujipa nguvu. Hapo ndipo niligundua kuwa akili yangu inasimamia kiu ya sukari bila mimi kuelewa kinachoendelea.
Nilihitaji nguvu ya utashi ambayo ingeamuru akili yangu kuamini vinginevyo. Ndivyo akili zetu zinavyofanya kazi, kile ambacho akili zetu zinaamini tunakitaka, ndicho tunachofanya bila hata kufikiria.
Kwa hivyo, niliazimia kuaminisha akili yangu kuwa sihitaji tena sukari. Nilianza kujisemea maneno ya kujihamasisha, na hatua kwa hatua, ufahamu wangu ukabadilika na kuamini kuwa hicho ndicho ninachokitaka. Mazoea mapya yakaanza kujengeka, na ikawa rahisi kusimamia kile nilichotaka kitokee.
Jambo la pili nililojifunza ni umuhimu wa kuweka mazingira yanayonihamasisha kusimamia msimamo wangu. Mbali na kuaminisha akili yangu kuwa suala la kuacha sukari halikuwa mchezo, niligundua kuwa ninahitaji watu watakaonisaidia kutorudi nyuma.
Kwa hiyo, niliwaambia watu wangu wa karibu kuhusu nia yangu ya kuacha sukari. Hii iliniongezea msukumo wa kusimamia uamuzi wangu.
Nadhani unaweza kutumia mbinu hii hata kwa tabia nyingine unazotaka kuacha. Usifanye uamuzi wako uwe siri. Unapowaambia watu kuhusu kusudio lako, unajitengenezea mazingira ya kulazimika kusimamia kile ulichokiamini hata pale unapojisikia kuahirisha mpango wako.
Ukiwa na watu sahihi wanaounga mkono uamuzi wako, itakuwa rahisi zaidi kusimamia mpango wako.
Huwezi, kwa mfano, kuacha pombe ikiwa umezungukwa na watu ambao mlikuwa mnakunywa pamoja.
Ukiendelea kuwa na watu wa aina hii, utahisi ugumu wa kuwa tofauti. Katika mazingira kama haya, inaweza kuwa vigumu kuacha. Mbali na kuwaambia ‘wanywaji’ wenzako kuwa unaacha pombe, ni muhimu kutengeneza mtandao mpya wa watu watakaokusaidia kuona thamani ya maamuzi uliyofanya. Unahitaji watu watakaokufanya ujisikie umepungukiwa ukiendelea na tabia hiyo.
Jambo la tatu nililojifunza ni kuifanya tabia usiyoipenda iwe ngumu.
Nakumbuka nilipopambana kuachana na matumizi yasiyo na faida ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp, ilibidi niondoe programu hiyo kwenye simu yangu.
Hatua hii ilikuwa ngumu, lakini ilinisaidia kuweka ugumu wa kurudi kwenye tabia nisiyoitaka. Unaweza kufanya hivyo kwa karibu kila tabia usiyoipenda.
Kama wewe ni mtumiaji mbaya wa fedha, unahitaji kujiwekea mazingira magumu ya kuchukua fedha benki. Fanya iwe vigumu kutoa fedha kwenye akaunti yako. Kwa mfano, badala ya kujiunga na huduma za kibenki zinazopatikana kwenye mitandao ya simu, lazimika kwenda benki au ATM ili kutoa fedha. Ikiwezekana, akaunti ya pamoja na mwenzi wako inaweza kusaidia. Usumbufu wa kumtafuta mwenzi wako asaini hati ya kuchukua fedha unaweza kukusaidia kujidhibiti.
Inaendelea wiki ijayo