Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JKT imeonyesha njia wengine wafuate

Muktasari:

  • Huu ni muendelezo wa alama nzuri ambayo JKT inaendelea kuweka katika sekta ya michezo nchini na pia ni uthibitisho kuwa ndani ya hii nchi, tunao wataalam ambao wakipewa imani na sapoti.

Kwa muda mrefu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limekuwa likitoa mchango mkubwa katika kusaidia maendeleo ya sekta ya michezo hapa nchini.

Kwa miaka mingi tumeshuhudia uwekezaji ambao JKT inafanya kwa wanamichezo binafsi, wa kitimu na pia wa ujenzi wa miundombinu ya michezo kama viwanja na kambi za wanamichezo.

Jambo la kufurahisha ni kuona JKT haina ubaguzi katika uwekezaji wake michezoni kwani imekuwa ikitoa fursa kwa michezo ya aina tofauti na sio soka pekee kama ambavyo taasisi nyingi hapa nchini zimekuwa zikifanya.

Iko mifano mingi ya kuthibitisha namna JKT inavyojitoa katika kusaidia harakati za kuendeleza sekta ya michezo Tanzania.

Ukizungumzia ngumi, hauwezi kuikwepa JKT kwani imekuwa ikisaka vipaji vingi vya mchezo huo, kuviendeleza kwa kuvipa fursa ya kufanya mazoezi katika maeneo tofauti ya vikosi vyake lakini pia kutoa fursa kwa mabondia hao kushiriki mashindano tofauti ambayo huwawezesha kukuza thamani zao, kupata uzoefu na fedha lakini pia kuitangaza nchi.

Mfano ni mwaka 2022 ambapo mabondia wawili wa JKT, Kasimu Mbundwike na Yusuph Changalawe walishinda medali za shaba katika michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Birmingham, England.

Riadha ni mchezo mwingine ambao umenufaika sana na sapoti kutoka JKT ambapo jeshi hilo limekuwa likitoa ajira kwa wanariadha wanaofanya vizuri na hata wale wanaochipukia ambao wanaonekana wanaweza kuja kuwa wanariadha mahiri siku za usoni.

Mfano wa wanariadha ambao ni matunda ya JKT ni  Alphonce Simbu, Emmanuel Giniki, Magdalena Shauri na Fabian Joseph.

Katika soka JKT inatambulika kwa kuwa taasisi ambayo inaongoza kwa kuwa na timu nyingi zilizowahi kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi daraja la kwanza upande wa wanaume.

Kulikuwa na JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mlale JKT, JKT Kanembwa, JKT Oljoro ambazo hizo awali zilikuwa chini ya usimamizi wa vikosi lakini baadaye tukashuhudia kuanzishwa kwa JKT Tanzania ambayo hiyo ikasimama kama timu moja inayobeba bendera ya Jeshi la Kujenga Taifa ikiwa chini ya usimamizi wa makao makuu ingawa bado jeshi halikuzuia vikosi vilivyokuwa na timu kuendelea kuzisimamia.

Hata hivyo kwa bahati mbaya timu hizo ambazo zimekuwa zikishiriki ligi za madaraja ya juu kwa upande wa wanaume, katika miaka yote hazijafanikiwa kutamba kwa kuchukua mataji au kumaliza katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi kuu.

Mafanikio makubwa ya uwanjani ambayo Jeshi la Kujenga Taifa linajivunia ni timu ya wanawake ya JKT Queens kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka ya wanawake Tanzania kwa miaka mitatu.

JKT Queens imekuwa ikiiheshimisha taasisi ya JKT kwani imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa timu ambayo inatoa idadi kubwa ya wachezaji wa kuzitumikia timu za taifa za wanawake za Tanzania kuliko timu nyingine yoyote na kikosi chake kinaundwa na wachezaji wazawa tupu.

Wakati tukitazama uwekezaji wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa timu na wanamichezo, miaka ya hivi karibuni, taasisi hiyo imeonyesha na kuthibitisha kuwa inaweza kufanya mambo makubwa katika sekta ya michezo Tanzania katika upande wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo hasa viwanja.

Ni JKT kupitia kampuni yake ya Suma-JKT ndio iliyojenga kwa asilimia mia moja Uwanja wa soka wa KMC Complex ambao umekuwa gumzo katika siku za hivi karibuni kutokana na ubora wake.

Uwanja ambao ulijengwa ili utumiwe na KMC FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni lakini leo hii umegeuka kimbilio la Simba na Yanga ambazo pia zinautumia kwa mechi zao za nyumbani zq ligi na Kombe la  Shirikisho la CRDB.

Ikumbukwe pia kuwa uwanja huo umekuwa ukitumika hata na timu zetu za taifa kwa ajili ya mazoezi pia umetumika kwa baadhi ya mashindano ya baraza la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Na baada ya hicho kilichofanyika katika Uwanja wa KMC Complex, serikali ilishawishika kuipa tenda Suma JKT ya kujenga na kuboresha viwanja ambavyo vitatumika kwa ajili ya mazoezi kwa timu zitakazoshiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) mwezi ujao.

Kwa hapa Dar es Salaam, viwanja hivyo ni Gymkhana, Leaders Club, shule ya sheria pamoja na Meja Jenerali Isamuhyo.

Ukiangalia kazi ambayo imefanyika hadi sasa, JKT inapaswa kupokea pongezi kwa vile viwanja hivyo ndani ya muda mfupi vinakaribia kukamilika na vimekidhi kwa zaidi ya asilimia 75 vigezo ambavyo vimewekwa na shirikisho la mpira wa miguu Afrika (Caf).

Huu ni muendelezo wa alama nzuri ambayo JKT inaendelea kuweka katika sekta ya michezo nchini na pia ni uthibitisho kuwa ndani ya hii nchi, tunao wataalam ambao wakipewa imani na sapoti.

Katika kipindi hiki ambacho nchi ina mpango wa kuboresha viwanja hasa vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine, itakuwa ni jambo jema kuona taasisi ya JKT inaendelea kuaminiwa na kupewa jukumu hilo badala ya kuzipa kampuni za nje ya nchi.

Itasaidia kupunguza gharama lakini pia ni kuonyesha thamani kwa kile ambacho imekifanya.

Wanasema chanda chema huvikwa pete hivyo tuonyeshe hili kwa JKT.