Juhudi zaidi zinahitajika katika kuifikia hedhi salama

Hedhi ni kipindi maalumu ambacho msichana au mwanamke hubalehe na kila mwezi kwa siku tatu mpaka saba hutokwa na damu ukeni. Mara nyingi kitendo hiki hutokea kila baada ya siku 28, japo wapo wanaotoka kabla au baada ya siku hizo.
Licha ya kuwepo kwa kampeni na harakati nyingi kwenye jamii zinazotolewa na wadau mbalimbali zikilenga kutoa elimu juu ya hedhi salama, bado mwamko na uelewa kwa wananchi ni mdogo.
Tofauti na miaka ya nyuma, hivi sasa suala la hedhi linazungumzika hadharani, linafundishwa shuleni na hata wanaume wanalizungumza, japo siyo kwa kiasi kikubwa. Lakini angalau ile hali ya kuona hedhi ni siri imepungua.
Kwa sasa baadhi ya shule zinakuwa na taulo kwa ajili ya wanafunzi, japo sio za muda wote, lakini pale inapotokea akiwa shuleni ana uwezo wa kupata ya kuvaa na kuendelea na masomo badala ya kurudi nyumbani kama ilivyokuwa awali.
Pamoja na mafanikio hayo, bado tunapaswa kujiuliza je, mazingira tuliyonayo kwenye jamii yanamfanya mwanamke kuwa na hedhi salama?
Ili hedhi iwe salama, mwanamke au msichana aliye katika hedhi anapaswa kuwa na uwezo wa kupata kifaa salama cha kuzuia damu ili asichafuke, apate maji tiririka ya kujisafisha kuwe na sabuni lakini pia kuwe na chumba maalumu cha kujisitiri pamoja na sehemu sahihi ya kutupa au kutunzia kifaa baada ya kukitumia.
Kitaalamu mwanamke au msichana anashauriwa kukaa na taulo anayotumia siyo zaidi ya saa nane, baada ya hapo anapaswa kubadili. Lakini kutokana na mazingira yasiyo rafiki, wapo wanaolazimika kutumia muda mwingi zaidi na hii ni hatari kiafya.
Mei 28 kila mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya hedhi salama na siku hizo huambatana na kaulimbiu mbalimbali, zote zikilenga kuelimisha na kuhamasisha elimu ya hedhi salama na mazingira rafiki kwa mtoto wa kike.
Kwa mwaka 2024 kaulimbiu ya siku hii ni “Wezesha Mazingira Rafiki na Endelevu kwa Hedhi Salama”.
Kaulimbiu ya mwaka huu inaendana na uhalisia kuwa hedhi, haiwezi kuwa salama kama hakutakuwa na uwezeshwaji wa mazingira rafiki na endelevu.
Zipo juhudi nyingi zimefanyika za kuhamasisha upatikanaji wa taulo kwa wasichana, hasa waliopo shuleni ziwe za kununua au za kutengeneza kwa mkono. Lengo likiwa kumkinga na magonjwa yatokanayo na kutumia vifaa visivyo salama.
Pamoja na juhudi hizo, bado mazingira yanayotuzunguka hayamwezeshi kuwa na hedhi salama.
Licha ya mwanamke kuwa na uwezo wa kutumia taulo safi na wakati mwingine za dukani zilizothibitishwa na mamlaka na zenye viwango, bado hana uhakika wa kupata maji tiririka, sabuni au eneo la kubadilishia pindi atokapo nyumbani.
Pia inapotokea amepata hedhi ghafla, hana sehemu ambayo itamwezesha aweze kujisitri bila kuchafuka na kudhalilika.
Miundombinu mingi iwe ni hospitali, vituo vya mabasi, kwenye taasisi za umma hata zile binafsi ambazo zinatoa huduma za kijamii, hazina vyumba maalum vya kumsaidia mwanamke kujisitiri aidha kubadili aliyokuwa amevaa au kujisitiri pale alipopatwa na hedhi nje ya utaratibu wake wa kawaida.
Kama ambavyo sasa Serikali na wadau wanapambana kuhakikisha shule zinakuwa na vyoo na chumba maalumu chenye maji, sabuni na taulo kwa ajili ya kuwasaidia wasichana walioko kwenye hedhi kubadili, basi juhudi hizi ziende pia kwenye majengo mengine ya umma.
Nafurahishwa sana na stendi ya mabasi ya Shinyanga ambayo mbali na kuwa na chumba maalumu cha kumsaidia mwanamke kubadili, lakini wamekwenda mbali na kuweka taulo za kike ndani, hii inamsaidia yule ambaye kwa bahati mbaya mzunguko wake umetoka akiwa safarini bila kutegemea.
Badala ya kuchafuka akiwa kwenye eneo hilo, ana uwezo wa kujisafisha na kubadili, kisha kurudi kwenye usafiri kuendelea kuwa safi na salama awapo safarini.
Kama Shinyanga imewezekana, ni dhahiri hata kwa vituo vingine hili linawezekana. Kwa pamoja inawezekana kumfanya mwanamke aifurahie hedhi na kuona ni kitu cha thamani, siyo karaha au mzigo kwenye maisha yake.
Tunapoadhimisha siku ya hedhi salama, unahitajika mkazo zaidi wa kuhakikisha mazingira rafiki na endelevu yanakuwepo.
Taulo, maji, sabuni na chumba maalumu cha kujisitiri iwe ni takwa la lazima kwenye majengo ya umma na hata yale ya binafsi, hii itamsaidia mwanamke kuwa safi na salama na hapo ndipo tutasema hedhi ni salama kwa kuwa mazingira yanayomzunguka ni rafiki na endelevu.
Rehema Matowo ni Mwandishi wa Mwananchi Mkoa wa Geita, anapatikana kwa namba 0756919691.