Kongole Profesa Mkenda, Necta

Baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuanza utaratibu mpya wa kutotangaza shule 10 bora na wanafunzi 10 bora kwa matokeo ya mitihani ya kitaifa, zimeibuka hoja nyingi kupinga utaratibu huo mpya, ambazo kimsingi hazina mashiko kwa maendeleo ya elimu nchini.

Wote tunakubaliana kwamba shule nyingi za Serikali zina changamoto nyingi ikiwamo, upungufu wa walimu, uhaba wa madarasa na madawati, uhaba wa vitabu ya kiada na ziada.

Kitabu cha kiada ni kitabu ambacho kipo kwenye silabasi na kitabu cha ziada hutumika kujazia kwenye somo au mada ambazo zipo kwenye kitabu cha kiada.

Pia, tunakubaliana shule nyingi za Serikali hazina maktaba kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ni wapi mwanafunzi atapata kitabu cha ziada? Pia, kitabu cha kiada ambacho ni rasmi na kimo kwenye silabasi, nacho upatikanaji wake una changamoto kwa shule za Serikali.

Tunakubaliana shule za Serikali kuna changamoto za mishahara midogo ya walimu, pia, mishahara yao inapitia benki, huku walimu wengine wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata mshahara.

Tunakubaliana mwalimu wa shule za Serikali mazingira yake ya maisha ni magumu, hakuna nyumba za kuishi, wakati mwingine shule zimejengwa mbali na mahitaji ya kijamii kama soko, maduka na hospitali, mwalimu analazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Pia, kuna shule wanafunzi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kutoka majumbani kwao kwenda shule na wale wa shule za mjini mwanafunzi kila kukicha anapambana na manyanyaso ya makondakta wa daladala.

Kuna sehemu nyingine kuna migomo ya walimu; pia chakula kwa wanafunzi nacho siyo cha uhakika sana.

Lakini, sote tunakubaliana kuwa mwanafunzi anayesoma shule binafsi zikiwamo zinazoitwa ‘English Medium’ hakuna changamoto kama anazopata mwanafunzi anayesoma shule za Serikali.

Mwanafuni wa ‘English Medium’ ana vifaa vyote vya shule. Ana vitabu vyote, shule ina maktaba, chakula kipo shule, mwalimu analipwa vizuri. Kuna ‘school bus’, kompyuta na mazingira ya shule ni bora.

Inashangaza anasimama mtu anataka kulinganisha mwanafunzi wa shule Serikali na yule wa ‘English Medium’, wawe sawa kwenye matokeo ya mitihani, bila aibu mtu anasema uamuzi wa Necta ni kuwanyima furaha waliofaulu vizuri. Jukumu la Necta siyo kufurahisha waliofaulu.

Naungana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ya kutumia njia ya nyongeza ya thamani kwa kuangalia mwanafunzi alianza akiwa vipi na shule imechangia nini katika kumuinua kwenye masomo yake.

Hii ndio njia bora ya kuzipima hata hizo shule za ‘English Medium’ ambazo mwanafunzi akiwa na maendeleo hafifu darasani wanamfukuza shule.

Profesa Mkenda anasema utaratibu huu wa nyongeza ya thamani unatumika katika nchi nyingi duniani. Hii ni kweli kabisa; mfano ni nchi jirani ya Kenya.

Kenya alama za ufaulu kwa shule za Serikali na zile za ‘English Medium’ ni tofauti. Wao wanasema huwezi kumpima kwa kiwango sawa mwanafunzi aliyepitia changamoto nyingi tangu anaanza shule hadi anamaliza na yule aliyesoma bila kupitia changamoto hizo.

Mitihani ya kitaifa kwa Kenya, alama za ufaulu kwa mwanafunzi wa shule za Serikali ni tofauti na yule aliyesoma ‘English Medium’.

Mwanafunzi aliyesoma na kuhitimu shule za Serikali alama zake za ufaulu ziko chini, mfano pointi za kupata daraja A kwa shule za Serikali ziko chini ukilinganisha na pointi za kupata daraja A kwa shule za ‘English Medium’.

Kwa nini Kenya wanafanya hivyo, wana sababu kadhaa, kwanza ni kutenda haki kwa wanafunzi wanaopitia changamoto nyingi kwenye shule za Serikali ikilinganishwa na zile za ‘English Medium’.

Kenya wanajua wanafunzi wa shule za Serikali wanakabiliwa na migomo ya walimu, lakini huyu mwanafunzi wa ‘English Medium’ mwalimu hagomi na analipwa vizuri.

Wakaona kuna sababu gani ya kuwapa sawa pointi za ufaulu wa masomo kwenye mitihani yao, haki iko wapi? Maana siku zote mwanafunzi aliyesoma kwenye mazingira mazuri atafaulu tu.

Uamuzi wa Necta na hoja zilizotolewa na Profesa Mkenda uwe mwanzo wa kutenda haki wa alama za ufaulu kati ya shule za Serikali na zile za ‘English Medium’.