Serikali yabariki uamuzi wa Necta

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda.

Muktasari:

  • Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameeleza jinsi udanganyifu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022 ulivyofanyika na hatua zinazoendelea kuchukuliwa.

Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema wamejiridhisha na hatua zilizochukuliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa wanafunzi 337 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani yao ya kidato cha nne mwaka 2022.

 Necta ililifuta matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 337 sawa na asilimia 0.06 ya watahiniwa wote 560,335 waliofanya mitihani yao ya kumaliza elimu hiyo huku matokeo ya wanafunzi 20 yakizuiliwa ili kupisha uchunguzi.

Februari 5 mwaka huu wazazi waliokuwa na watoto waliomaliza kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari ya Thadaafa iliyopo jijini Mwanza, waliandamana wakitaka viongozi wa juu wa Serikali kuingilia kati suala hilo ili waweze kupata matokeo.

Akizungumza leo Jumatano Februari 8, 2023, Profesa Mkenda amesema kati ya watahiniwa waliofutiwa matokeo, wanne waliandika matusi katika vitabu vyao vya majibu ya mitihani huku 51 wakikutwa na maandishi yasiyoruhusiwa kwenye vyumba vya mitihani.

“Wako 10 walikamatwa na simu ama smart watch kwenye vyumba vya mitihani, wote wanajua hawaruhusiwi kuingia navyo na wanakumbushwa wakati wanavyoingia na wanajua kuwa wakikamatwa matokeo yao yanafutwa,”amesema.

Amesema wako watahiniwa tisa ambao hawakwenda katika vyumba vya mitihani bali walituma watu kuwafanyia mitihani na kwamba tayari wamekamatwa na polisi lakini waliofanyiwa walifutiwa matokeo yao.

 “Wanafunzi 27 walikamatwa wakiwa wanasaidiana katika chumba cha mitihani kinyume na kanuni za mitihani nao wamefutiwa. Wako watahiniwa sita matokeo yao yamefutwa kwasababu ya kutumia jukwaa la Whatsapp,”amesema.

Profesa Mkenda amesema suala hilo la kutumia jukwaa la Whatsapp limejitokeza katika Shule ya Sekondari ya Mnemonic ya Mjini Magharibi Zanzibar ambapo mtahiniwa mmoja alipiga picha mtihani na kuituma mmliki wa shule ambaye aliratibu majibu ya maswali hayo na kurushwa katika kundi la whatsapp.

Amesema watahiniwa wengine watano ambao hawakukamatwa na simu, walifutiwa matokeo yao kwasababu uwepo katika kundi hilo ni jitihada za kufanya udanganyifu.

Profesa Mkenda amesema watahiniwa 20 wengine waliofanya mitihani katika kituo cha shule hiyo matokeo yao yamezuiliwa kwasababu katika kundi hilo kuna majina 20 yasiyofanana na watahiniwa wasiofahamika.

Amesema wako 206 wamefutiwa matokeo kwa kufanana kwa majibu yao kusiko kwa kawaida waliyotoa katika matokeo ambapo kati yao 140 wanatoka katika Shule ya Thadaafa ya jijini Mwanza huku 66 wakitoka Shule ya Sekondari ya Twibhoki ya mkoani Mara.

“Wakati mtihani unaendelea taarifa za siri ziliwasilishwa Baraza la Mitihani kuna wizi mkubwa na udanganyifu mkubwa unaendelea baraza likachukua hatua mbalimbali. Baraza liliamua kupitia majibu yaliyotolewa,”amesema.

Amesema wizara yake imeridhika na uamuzi huo na kwamba watapeleka Muswada Marekebisho ya Sheria ya Necta bungeni ili kutoa adhabu kali zaidi kwa watakaobainika kufanya udanganyifu.