Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa nini chanjo ya paka, mbwa isiwe lazima?

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Tanzania ina ng’ombe milioni 22.8, kondoo milioni saba, mbuzi milioni 15.5, nguruwe milioni mbili na kuku milioni 60. Hiyo ni mifugo inayoliwa na binadamu, lakini pia wapo mbwa na paka wengi.

Jana katika toleo la gazeti hili kulikuwa na habari iliyoitaja Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kuwa ina idadi kubwa ya mbwa na paka katika eneo lenye watu wachache.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Tanzania ina ng’ombe milioni 22.8, kondoo milioni saba, mbuzi milioni 15.5, nguruwe milioni mbili na kuku milioni 60. Hiyo ni mifugo inayoliwa na binadamu, lakini pia wapo mbwa na paka wengi.

Kulingana na habari hiyo, iliyobeba kichwa cha maneno kisemacho “Wilaya ya Moshi ina paka na mbwa 40,000, yapewa chanjo”, wanyama hao wanaishi kwenye eneo lenye wakazi 182,292. Mbaya zaidi ni kuwa viumbe hao wamegeuka kuwa tishio kwa kusababisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa binadamu.

Inaelezwa kwamba, takriban watu 1,500 hapa nchini hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa unaotokana na kung’atwa na mbwa au paka wenye ugonjwa huo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega anasema takriban dozi 33,700 zenye thamani ya Sh103 milioni zimepatikana kutoka kwa wadau wa maendeleo kutokana na ongezeko la ugonjwa huo wilayani Moshi. Katika maelezo yake, Ulega anasema licha ya msaada huo wa chanjo uliotolewa na Shirika la Misaada la Marekani (Usaid) kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (Fao) kwa ajili ya Moshi, tatizo hili liko karibu kila wilaya isipokuwa kwa upande wa Moshi tatizo liko juu.

Hivi karibuni mtoto wa miaka miwili alifariki dunia wilayani humo baada ya kuparuliwa na paka mwenye virusi vinavyosababisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa na watu wengine watatu walifariki katika maeneo ya wilaya hiyo katika kipindi cha mwezi wa Machi.

Naibu waziri huyo alitoa wito kwa wafugaji wote nchini kuhakikisha wanaitunza mifugo yao na muhimu kuichanja.

Kwanza, tunaipongeza Serikali kwa kuliona tatizo wilayani humo na nchi nzima na kuanza kukabiliana nalo ili kuokoa maisha ya wananchi, lakini pia ni vyema chanjo hiyo ikatolewa nchi nzima bila kujali mkoa au wilaya gani ili kudhibiti kichaa cha mbwa nchini.

Hata hivyo, licha ya kuwa na wingi wa mifugo, inavyoonekana jamii imekuwa ikijielekeza zaidi kuchanja ile inayotumiwa na wengi kama kitoweo na kujitenga na jukumu la kuwapa kipaumbele mbwa na paka katika mipango ya uchanjaji. Hili ni kosa kubwa.

Ni vyema sasa Serikali ikatunga sheria itakayosukumwa na sera madhubuti ya mifugo inayowalazimisha wafugaji wa mifugo ya aina zote kuhakikisha kwamba wanaipa kipaumbele katika uchanjaji, vinginevyo kama Taifa tutakuwa hatulitendei haki.

Vifo 1,500 vilivyotokana na kichaa cha mbwa vingeepukika kama wangekuwa wamechanjwa, lakini jambo jingine ni kuwa, umefika wakati sasa kwa Serikali kuwabana wafugaji wa paka na mbwa kutimiza wajibu wa kuitunza mifugo hiyo vizuri, badala ya kuiacha kuzurura ovyo mitaani.

Hivi sasa wapo paka na mbwa wengi mitaani wanaozurura na ni hao ndio wanaobeba magonjwa mbalimbali ikiwemo kichaa cha mbwa na kukileta katika makazi ya watu ambako husababisha vifo vya watu wanapowararua au kuwang’ata. Ni vyema sasa zikawepo takwimu za paka na mbwa pamoja na orodha ya wamiliki wa mifugo hiyo ili iwe rahisi kuwabana wahusika pale inapotokea kuonekana wanazurura mitaani.

Vilevile, ni wakati sasa mkazo ukaelekezwa kuandikisha paka na mbwa, na kuwabandika namba maalumu zitakazowatambulisha kirahisi ili iwe rahisi kufuatiliwa. Wenzetu katika mataifa mengine, hususan yaliyoendelea huu ndio mfumo wanaoutumia ambapo mbwa au paka ni rahisi kujulikana kupitia utambulisho walionao.