Madai ya bima ni nguzo ya kufidia majanga
Bima ni kinga ambayo hufanya familia isimame tena baada ya kukumbana na majanga. Moto unapoteketeza nyumba, ajali inapoliharibu gari au mafuriko yanapoharibu makazi ama mazao, bima ndiyo inayoweza kubadilisha hasara kubwa kuwa mwanzo mpya. Kwa maana hiyo ni kwamba, bima ni chombo cha kuondoa hofu na kuleta uhakika.
Changamoto kubwa haiko kwenye uwezo wa bima kufanya kazi, bali ni namna tunavyoshirikiana kuhakikisha kila dai linashughulikiwa kwa uwazi, haki na kwa uharaka.
Kwa wengi, madai ya bima yanaendelea kuwa fumbo. Watu hujiunga na bima kwa imani kwamba wakipatwa na janga watalipwa, lakini mara nyingi hukosa kufahamu hatua za kufuata. Matatizo mengi hutokea si kwa sababu kampuni za bima haziko tayari kulipa, bali kwa sababu mteja hakujulishwa mapema kinachohitajika.
Inapotokea ajali, taarifa zinapocheleweshwa, ushahidi unapokosekana, au masharti madogo yasiyoeleweka hujitokeza. Hapo ndipo migogoro huanza na imani huanza kupotea. Matokeo yake, bima huonekana kama mzigo badala ya msaada, na hali hii inaua ama kurudisha nyuma dhamira ya bima kama nyenzo ya kuleta faraja.
Kama sekta, tunalazimika kukiri kuwa tumechelewa kutoa elimu ya kutosha kwa wateja wetu. Ni jukumu letu kuwaelekeza kabla ya majanga kutokea. Tunapaswa kuwaambia tena kwa uwazi kwamba ripoti ya polisi ni muhimu, picha na risiti zinaweza kuamua uhalali wa dai, na kwamba kutoa taarifa mapema ni njia rahisi ya kupata malipo ya haraka.
Hatupaswi kumwachia mteja pekee mzigo wa kutafuta majibu wakati tayari ameshakumbwa na hasara. Tunapaswa kuwa bega kwa bega naye, tukimweleza hatua kwa hatua, ili afahamu anachopaswa kufanya kuanzia siku ya kwanza anaponunua sera yake ya bima.
Lakini, jukumu hili halibaki kwa watoa bima pekee. Wateja nao wana wajibu wa kuuliza maswali sahihi kabla hawajasaini mkataba wowote. Ni lazima wafahamu ni nini hasa kimeingizwa na ni nini hakipo kwenye mkataba alioingia mteja. Ni lazima watambue muda wa kutoa taarifa na nyaraka zinazohitajika.
Elimu hii inahitaji kuingizwa moja kwa moja kwenye mazungumzo kati ya mtoa bima na mteja. Wakati mwingine, kukosa kuuliza swali moja dogo tu, kama “nikichelewa kutoa taarifa, nini kitatokea?” kunatosha kufanya dai liharibike. Hii ndiyo sababu uwazi na majadiliano ya mapema ni msingi wa uaminifu.
Kwa upande wa watunga sera, hatua kadhaa tayari zimepigwa. Kanuni za TIRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania) zinazotaka madai yalipwe ndani ya siku 45 baada ya kusainiwa kwa nyaraka, huu ni mfano wa kulinda haki za wateja wa bima.
Lakini, tunahitaji kwenda mbali zaidi. Kanuni zetu zinapaswa kulazimisha uwazi mkubwa zaidi, kuhakikisha kila mkataba wa bima unakuwa na maelezo mafupi kwa lugha rahisi, na kuhimiza uwekezaji kwenye mifumo ya kidijitali ambayo itarahisisha uwasilishaji wa madai na kupunguza urasimu.
Ikiwa taarifa za polisi au hospitali zingeweza kuunganishwa moja kwa moja na mifumo ya bima, wateja wasingelazimika kukimbizana na makaratasi kila mahali. Hatua kama hizi zingeokoa muda na kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Iwapo wateja wataelimishwa, watoa bima watajitolea kuwa wa wazi na wabunifu, na watunga sera wakahakikisha sheria zinazingatiwa ipasavyo, basi madai ya bima yatakuwa si tu malipo baada ya hasara, bali nguzo ya kufidia Maisha baada ya majanga.
Dai la bima halipaswi kuonekana kama ombi linaloweza kukubaliwa au kukataliwa kwa hiari. Ni haki. Na haki hiyo inapotekelezwa kwa ufanisi, familia inarejesha tena heshima yake, biashara inainuka, na jamii inabaki thabiti.
Bima si anasa ya matajiri. Ni ulinzi wa msingi unaohitajika na kila familia, kila mkulima, kila mfanyabiashara mdogo.
Mkulima mdogo wa mpunga anapopoteza shamba lake kwa mafuriko, au mama mjane anapopoteza nyumba yake kwa moto, bima inaweza kuwa tofauti kati ya kubaki kwenye lindi la umaskini na kuanza tena safari ya maisha kwa matumaini.
Wakati majanga hayakwepeki, matumaini ya kurejea kwenye hali ya kawaida yanapaswa kuwa ya hakika, na si ya bahati. Tukishirikiana sote—wananchi, watoa bima na watunga sera, tunaweza kujenga Tanzania ambayo madai ya bima yanamaanisha mwanzo mpya, sio mzigo mwingine.
Jumanne Mbepo ni Meneja Mwandamizi wa Bima, Benki ya Stanbic Tanzania