Mheshimiwa Janwari Marope, tusikie diaspora

Janwari Marope a.k.a Maghoe kwa washambaa na wanyika. Nzeze? Nkhozeza Osie. Juzi nilikuona ukihojiwa na fyatu aitwaye Petro Eliyasi (siyo aliyemuasi mwana wa Adamu). Tuyaache.

Nilifuatilia mahojiano yenu. Niligundua namna mafyatu wanene na miungumafyatu, mnavyotaka kuwafyatua mafyatu wa diaspora a.k.a ughaibuni a.k.a majuu a.k.a kwa walaji bata a.k.a wabeba maboksi a.k.a Ulaya a.k.a Amerika. Tuyaache.

Nianze kukufyatua maswali kifyatu. Mosi, ulisema mmeandaa sera ya hadhi maalumu kwa mafyatu wa diaspora. Cool, nyinyi ni nani muwapangie wenzenu? Nieleweke. Mpangaji nani awe mdanganyika au la si mwingine bali waliowatengeneza.


Tuna tofauti na vyungu mbele ya waliotufyatua? Kaya zote za kichovu za Kiswahili zilifyatuliwa kule Berlin mwaka 1884 na wakoloni. Hivyo, zinazofanya ni kuendeleza ukoloni zikijidai ziko huru. Ulisema kwamba Mbongo yeyote mwenye ganda la kigeni mradi ana asili ya Tanzania, anaruhusiwa kumiliki ardhi kama ambavyo Mtanzania ana haki, na uwezo wa kurithisha hiyo ardhi.

Sasa wakati sheria yenyewe haijapitishwa? Anakuwaje Mtanzania wakati mshakataa uraia pacha? Unamaanisha au unajifyatua mtama kwa kulazimisha kitu hiki? Inaonyesha Utanzania wa Mtanzania kumbe hauuawi hata kwa wale wanaojidai kuua? Mgoshingwa kazaliwa Bumbui. Babu kazikwa Mponde. Bibi yuko Mashindei Vuga kwa zumbe Kimwei. Mwezukuu alizaliwa Maezangula. Yuko Minesota akitasaka fursa. Unataka kumfuta. Hao wazazi wake nao utawanyang’anya uraia?

Hiyo ardhi mnayobania mnaifanyia nini zaidi ya kuwapa wachukuaji mnaowaita wawekezaji? Hivi Deep Weed ya Do-buy nao ni wadanganyika mliowaachia kila kitu? Mnazuia wanadiaspora kumiliki ardhi. Je, mnaihitaji, kuitumia au roho mbaya tu?

Wakati mwingine huwa sioni tofauti ya fyatu wajomba zetu manyani wanaokaa ardhini wasiitumie. Sijui kama wangekuwa wadanganyika wangeibania wakati hawaitumii kujiletea maendeleo.

Pili, wanene wanaotufyatua kama akina Rost tamu wa Kagoda na wengine wana uraia pacha na uzalendo wa kweli? Je, mafisi na mafisadi waliomwezesha gabacholi Chauda kukaa Danganyika pamoja na kuwa persona non grata, wana uraia pacha au uzalendo?

Na walioleta IPTL na waliowaachia mahakamani tukala hasara wana uraia pacha? Waliochoma Benki Kuu walikuwa na uraia pacha? Je, uzalendo ni idadi ya uraia au chaguo la fyatu?

Tatu; je, hatuna walowezi toka nonihino wanaosifika kuwa na uraia wa Canada na Uingereza ambao ni raia wa kaya mafyatu wanaohadaiana na kudanganyana hadi kuitwa Wadanganyika mbali na wa mipakani waliong’ang’ania uraia wao asili baada ya Afrika kugawanywa?

Je, unajua kuwa mafyatu wajanja wakienda ughaibuni huwa wanakaa na ukazi wa kudumu bila kuchukua uraia, vinginevyo hakuna jinsi hasa wale wanaotaka kuingia siasa za huko au kufaidi haki za kielimu?

Nne, kwa nini mnahangaishwa na ardhi kana kwamba hakuna hii kitu huko diaspora? Huku ni njuluku zako. Hata uwe mkazi wa kudumu. Hakuna uchawa na roho mbaya eti mara ardhi. Yupo atayehamisha? Huku wanachojali ulipe kodi. Ununue au kuuza ardhi, hawana stori na mambo ya kizamani kama hayo japo ni makaya tajiri kwelikweli.

Huku ukipata ardhi imepimwa, unapata umeme si mgawo, maji na barabara wala huhongi kupata hati. Mafyatu wa diaspora ni wazalendo wanaopenda nyumbani kwao walikokimbia sababu ya shida. Hakuna haja ya roho za korosho. Huwa nawaona kama baniani wabaya, njuluku yao dawa.

Semeni kweli. Mnaweka mikingamo kwa kuogopa kufyatuliwa kisiasa kutokana na exposure ya diaspora ambako nako kuna siasa. Wapo walioziingia na kuukwaa na magazeti ya umbea ya mafyatu yakaripoti yakijisifu.

Huwa nashangaa kusoma “Mdanganyika ashinda Nobel Prize au cheo”. Vipi, wakati mshamkana kwa kuukataa uraia pacha? Je, nani kawapa mamlaka ya kutoa hadhi maalumu wakati huo udanganyika mnaobania na kuringia ulianzishwa kule Berlin, Ujerumani?

Nitawaomba Wajerumani wachukue uraia waliowatengenezea nione mtakachoringia. Hamjui kuwa wakoloni weusi waliwarithi weupe waliowatengeneza? Mnalenga kufyatua haki au kutaka kuwafyatua wanadiaspora ili mfyatue njuluku zao ambazo zimesaidia sirkali nyingi fisadi na mbovu kuserereka maulajini kimabavu kinyume cha sheria kwa vile mafyatu wanapozwa hasira na shida na remmitances?

Who’s fooling whom here? Au niseme who’s fyatuaing whom here? Wasingekuwa machizi, ningewahamasisha wasitume hata njuluku tuwaone. Mnataka waongeze njuluku zipigwe?

Mwisho, nilikusikia ukisema “Watanzania wamechelewa sana kutoka nje, nchi nyingine, watu walianza kutoka tangu miaka ya 1950 lakini Tanzania ilibaki nyuma.” Pamoja na maghumashi, wapo wajanja waliotoboa mnaowatillia mtima nyongo. Je, zaidi ya nyinyi kuzidi kuwachelewesha mmefanya nini kuwaharakisha?

Hujui kukataa uraia pacha ni mojawapo ya mambo yanayozidi kuwachelewesha na kujichelewesha? Ukienda uhamiaji, mafisi na mafisadi wanataka saini ya bibi wa bibi wa babu wa babu mbali na makandokando mengine ili ushindwe wakufyatue mshiko.

Huu ulabu! Hadhi maalumu yenyewe iko wapi wakati kigwena hakijakaa kuwafyatua na kuwavunga diaspora? Kumbe tunafungana kamba! Kumbe kiki!