Mkeo siyo ngoma upige utakavyo
Mkeo ni mwenzi. Umtunze akutunze, umpende akupende, na ukimtesa utateseka. Hata hivyo, kuna imani potofu za baadhi ya makabila ambazo hatujui kama ni za kweli kuwa bila mume kumtandika mkewe inaonyesha hampendi vilivyo.
Kadhalika, kwa baadhi ya makabila na karibu yote, dhana hii inashangaza na kufanya hata kuwa vigumu kuielewa, achia mbali kuikubali. Gereza ni gereza, hata liwekewe vyakula safi na kila anasa. Na kipigo ni kipigo na hakuna kipigo kizuri, kinachokubalika au kuzoeleka.
Kabla hujaamua kumpiga au kumdhulumu mwenzako, jiulize. Je, ningekuwa yeye ningependa nitendewe au nitenzwe vipi? Tunarudia. Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Sie waandishi siyo malaika. Pia, siyo mashetani. Tuna udhaifu wetu kama binadamu wengine.
Ila tuna ubora ambao tunaweza kusema wengi hawana au unaoweza kuwafunza wengine vitu vya maana kutokana na uzoefu wetu katika taasisi hii adhimu na ngumu. Pamoja na kukaa kwenye taasisi hii yenye kila aina ya changamoto na maadui, hatujawahi kupigana au kuitana majina mabaya hata siku moja. Tumewahi kununiana. Hili ni jambo la kawaida kwa binadamu. Hatujawahi kutukanana hata siku moja.
Hatuandiki haya kinadharia, kujifurahisha, au kumfurahisha yeyote, bali kufunza na kushare uzoefu wetu. Tumeyaishi na kujua kuwa yanawezekana. Kama yamewezekana kwetu, kwa nini yasiwezekane kwa wengine? Amani, furaha na ufanisi katika ndoa ni suala la uamuzi ila ni muhimu. Hata mafarakano, huzuni na maanguko katika ndoa ni masuala ya kupima na kuamua.
Tutoe mfano wa mwanandoa anayemdhulumu au kumuumiza mwenzie. Je, ni haki kwa mwanandoa huyu kutegemea kutendewa kinyume na atendavyo? Wahenga walisema kuwa dawa ya moto ni moto. Japo wanawake, mara nyingi, hawatumii fujo kama wanaume inapotokea ndoa ikawa na dhuluma na unyanyasaji, wana namna yao ya kulipiza kisasi, hata kama wapo pia wanaosamehe, kuamua kuachana, au kuvumilia hata kuachika. Kumpiga mkeo, licha ya kumuumiza na kumdhalilisha, ni kumuonea na kumdhulumu. Ni dhuluma kama dhuluma nyingine.
Kuna rafiki wa familia ambaye alikuwa na tabia ya kumtukana na kumpiga mkewe tena mbele ya watoto wake wachanga bila kujua kuwa angewaambukiza watoto uhovyo na ukatili huu. Siku moja akiwa kazini, mtoto wake mmoja alimuomba mama yake ampe ice cream (hatuna Kiswahili chake). Mama alimpa ice cream. Hata hivyo, mtoto hakutosheka, pamoja na kupewa ice cream nyingi tu tena jioni, jambo ambalo humsababishia kukosa usingizi na si jema kiafya.
Mtoto aliomba tena apewe ice cream. Safari hii, mama alimkatalia. Bila hili wala lile, yule mtoto mdogo alimrushia kibao mama yake huku akifoka kama afanyavyo baba yake. Kujua tatizo vilivyo, mama hakumrudishia kibao zaidi ya kumuonya asirudie. Mtoto naye hakukubali, badala ya kumpiga tena, alimwambia “kwa nini nisikupige?” Mama alimjibu mtoto “kwa nini unipige, kosa langu nini?” Mtoto alijibu “mbona baba huwa anakupiga na haelezi ni kwa nini?”
Mama alimdanganya mtoto kwa kumshauri asome kitabu na mtoto alisahau lakini bila kujutia. Je, wewe baba unayempiga mkeo, ungekuwa wewe ungefanya nini? Ungemfanya nini yule mtoto? Si rahisi kujibu. Na kama ukijibu, majibu yatakuwa mengi na tofauti. Kwa ufupi ni kwamba, kama walivyosema wahenga, kazimbi si mchezo mwema. Watoto wetu ni sisi wa jana na kesho.
Hivyo, tunapofanya mambo, tusijiangalie au kuwaangalia tu wale tunaowaonea au kuwadhulumu. Dhuluma kwa mama ni dhuluma kwa mtoto. Hivyo, iwe ni mila au imani, kumpiga mkeo si jambo jema. Kunajenga chuki ya chinichini na madhara yake yanaweza kuwa makubwa na ya muda mrefu kuliko unavyoweza kudhani. Mtoto wa nyoka ni nyoka.
Hivyo, ni vizuri ukajua kuwa kupigana ni udhalilishaji na ukatili. Je, hakuna njia nyingine za kuonyeshana mapenzi au kutatua ugomvi?
Kisa kingine, kuna jamaa mmoja alizoea kumpiga mkewe mara kwa mara. Mama alichukia na kumwekea kisasi. Alipougua akawa hana uwezo wa kujisaidia, alihitaji mkewe amsaidie. Mkewe alimjibu “sitakusaidia ili upone uendelee kunipiga. Nawe, acha ugonjwa ukupige uonje uchungu wa kuumizwa.”
Tumalizie. Mkeo siyo ngoma upige. Ni binadamu mwenye kuumia, anayehitaji heshima na mapenzi na si mateso na udhalilishaji. Je, unapata faida gani kumuumiza mwenzio uliyeahidi kumpenda, kumlinda na kumtunza ili naye akutunze hivyo?