Mkoa wa Lindi (i): Majimbo ya Lindi Mjini na Ruangwa – 50 kwa 50
Muktasari:
UJUE MKOA WA LINDI
Mkoa wa Lindi uko kusini mwa Tanzania na umepakana na mikoa ya Pwani, Mtwara, Ruvuma, Morogoro. Upande wa mashariki hupakana na Bahari Hindi” Bahari ya Hindi. Mkoa huu ulianzishwa mwaka 1971 na una eneo la kilometa za mraba 67,000.
UTANGULIZI
Leo tunaianza rasmi safari ya Mkoa wa Lindi baada ya kumaliza uchambuzi wa majimbo 41 yaliyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mara, Kigoma na Kilimanjaro.
UJUE MKOA WA LINDI
Mkoa wa Lindi uko kusini mwa Tanzania na umepakana na mikoa ya Pwani, Mtwara, Ruvuma, Morogoro. Upande wa mashariki hupakana na Bahari Hindi” Bahari ya Hindi. Mkoa huu ulianzishwa mwaka 1971 na una eneo la kilometa za mraba 67,000.
Karibu robo ya eneo la Mkoa wa Lindi (Kilometa za mraba 18,000) ni sehemu ya Hifadhi ya Wanyama ya Selous, moja ya vivutio vikubwa vya utalii lakini hifadhi hii haijatangazwa ipasavyo ili kulisaidia taifa mapato ya kutosha. Kivutio kingine kilichoko Lindi ni mito mikubwa ya Lukuledi, Matando na Mavuji ambayo yote inaeleka Bahari Hindi bila kusahau miji ya kale ukiwemo ule wa Kilwa Kisiwani ambao ni wa kihistoria kwa pwani ya Afrika ya Mashariki. Pia kuna magofu muhimu ya kale yanayoonesha namna gani mji huo wa Kilwa ulivyowahi kuwa kitovu cha biashara karne nyingi zilizopita.
Mkoa una wilaya sita za Lindi Mjini, Lindi Vijijini, Kilwa, Nachingwea, Liwale na Ruangwa pamoja ya majimbo manane ambayo ni Lindi Mjini, Ruangwa, Kilwa Kaskazini, Kilwa Kusini, Liwale, Nachingwea, Mchinga na Mtama.
Wakazi
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Lindi una jumla ya wakazi 864,652 huku asilimia 90 kati yao wakiwa ni wakulima. Makabila makubwa yaliyojikita ni Wamwera ambao hasa hupatikana wilaya za nachingwea na katika baadhi ya tarafa za Lindi Vijijini. Pia kuna Wamachinga na Wamalaba ambao wako zaidi Lindi Mjini bila kusahau Wamatumbi na Wangindo ambao wanapatikana Kilwa.
Miundombinu ya Mawasiliano
Kwa sababu Lindi ni mkoa ulioko kusini mwa Tanzania, maendeleo yamekuwa kwa mwendo wa jongoo kutokana na kukosekana kwa barabara ya uhakika kwa miongo mitano tokea nchi yetu ipate uhuru. Ni hivi sasa tu ndipo mawasiliano kati ya wana Lindi na Mikoa mingine ya Tanzania yameimarika, hasa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Mkapa mwaka 2002.
Ukosefu wa barabara za uhakika uliodumu kwa miaka mingi umeathiri uchumi wa Lindi ikiwemo Miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ilishakufa “kifo cha mende”.
Lindi kuna bandari ambayo imetelekezwa bila kuendelezwa huku Gesi iliyopatikana baharini karibu na Kisiwa cha Songosongo ikiwa haina manufaa makubwa kwa wana Lindi na Taifa kwa ujumla. Ukimuuliza raia yeyote wa Lindi gesi ile imemnufaishaje hakuna anayejua, mikataba yake iliingiwa kwa siri na ni vigumu kwa mtu mwingine kujua nini kinaendelea huko.
Kilimo na Biashara
Wakazi wengi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima wa mazao ya biashara na chakula. Mazao ya biashara ni pamoja na Korosho ambazo zinapatikana kwa wingi katika wilaya za Ruangwa, Lindi Vijijini na Nachingwea. Pia kuna zao la Ufuta kama zao la biashara katika Wilaya ya Kilwa. Wakazi wengi wa Mkoa wa Lindi wanafanya biashara ndogondogo.
Elimu
Mkoa wa Lindi uko nyuma kielimu, pamoja na ongezeko la shule za sekondari za kata pamoja na zile za msingi, shule hizo hazina walimu, vifaa na maabara na hivyo mara nyingi mkoa wa Lindi umekuwa ukiingia kwenye mkumbo wa mikoa inayofanya vibaya sana kielimu.
JIMBO LA LINDI MJINI
Jimbo hili ndilo linaunda sehemu yote ya manispaa ya mji wa Lindi na kwa sababu ni eneo la mjini lilifikika kirahisi wakati wanaharakati mbalimbali wakijitosa kusajili vyama vyao mwaka 1992. Hata ilipofika mwaka 1995 haikuwa kazi kubwa kwa upinzani kupenya na kueneza harakati zake, uchaguzi huo wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi ulikaribishwa na jumla ya vyama sita kwa wakati mmoja, kila kimoja kikitaka mbunge wake ashinde.
Baada ya kampeni, upigaji kura na matokeo, Mohamed Abdul – Aziz Abdi wa CCM aliwazidi wenzake ujanja na kulitwaa jimbo hilo kwa asilimia 75.6 (kura 9,144) huku akifuatiwa na mgombea wa NCCR, Amba Hassan Abdallah aliyepata kura 1,393 (asilimia 11.5) na mgombea wa CUF, Ndifwa Tumaini Bambo akipata kura 670 (5.5 asilimia ). Wagombea wa vyama vya TLP, NLD na Chadema kwa pamoja walipata asilimia 7.4 ya kura zote. Hivyo Mohamed Abdul Aziz alipata bahati ya kuliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha kwanza (1995 – 2000).
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ulipofanyika, CCM ilikuwa imejiimarisha vilivyo Lindi Mjini, nguvu ya NCCR ilikuwa imepungua sana kutokana na migogoro ndani ya chama hicho hivyo Mohamed Abdul–Aziz Abdi wa CCM alishinda tena na kuliongoza jimbo la Lindi Mjini kwa kipindi cha pili (2000 – 2005).
Ilipofika mwaka 2005, mabadiliko makubwa mawili yalitokea Lindi: Kwanza NCCR iliporomoka kabisa na Chama cha Wananchi (CUF) kikapanda na kuchukua nafasi hiyo. Pili, mgombea wa CCM, Mohamed Abdul–Aziz Abdi akizidi kuchokwa na wananchi. Mara kadhaa tumeeleza kuwa, mbunge anapoongoza jimbo kwa miaka 10 hawezi kuwa na jambo jipya la kufanya akiongezewa miaka mingine zaidi. Hata hivyo, CCM bado haikusita kumpa bendera Mohamed Abdul–Aziz, pamoja na kuchokwa kiasi cha kutisha.
Uchaguzi ulipofanyika Mohamed Abdul–Aziz wa CCM alipata asilimia 58.5 (kura 10,019) huku mshindani wake mkuu kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Salum Khalfan Barwany akipata asilimia 39.1 (kura 6,687) na vyama vya Chadema, TLP, Chausta na NLD kwa pamoja vikipata asilimia 2.5 ya kura zote. Hivyo, Mohamed Abdul–Aziz wa CCM alitangazwa kuwa mbunge na akaliongoza jimbo la Lindi Mjini kwa kipindi cha tatu mfululizo (2005 – 2010) na ni kipindi hiki ndipo Salum Baruany Khalfan wa CUF alizidi kujichimbia Lindi na kujiimarisha akitegemea mawindo yake kutokea mwaka 2010.
Je, unaikumbuka ile methali ya “sikio la kufa halisikii dawa?” Sikio hilo lilitokea Lindi Mjini mwaka 2010, wananchi wa Lindi walianza shangwe, nderemo na vifijo mara baada ya CCM kurejesha jina la Mohamed Abdul–Aziz kama mgombea wake kwa awamu ya nne mfululizo, yaani awaongoze kwa miaka 20. Wakasema hapana! Na ndiyo sababu walipokea uteuzi wa mbunge huyu kwa shangwe, kwamba walianza sherehe za kumuangusha kabla hata ya kinyang’anyiro chenyewe. CUF nayo haikucheza mbali, mwiba uleule uliomtikisa kigogo huyu mwaka 2005 ndiyo wakaurejesha.
Matokeo ya mwisho yalipotangazwa, Salum Khalfan Barwany wa CUF, Mtanzania mwenye ulemavu wa ngozi (albino), alishinda katika uchaguzi wa Lindi Mjini. Jina la Lindi Mjini likang’ara katika medani za siasa kitaifa na kimataifa kwa kuthubutu kumchagua mlemavu wa ngozi kuwa mbunge kupitia kura za kawaida. Jambo la namna hii halikuwahi kutokea tangu nchi yetu ianzishe mfumo wa vyama vingi na huwenda tangu tupate uhuru. Barwany alishinda kwa asilimia 51.44 (kura 13,155) akimshinda Mohamed Abdul Aziz kwa asilimia takribani saba kwani Mohamed alipata asilimia 44.75 (kura 11,445). Enzi za CCM kulitawala Jimbo la Lindi mjini kwa muongo mmoja na nusu chini ya siasa za vyama vingi zikakoma rasmi.
Salum Barwany ambaye mwezi Juni mwaka huu atatimiza umri wa miaka 56, ana elimu nzuri ya sekondari na ni mtu mwenye uelewa mpana wa masuala ya kitaifa na hasa kanda ya kusini anayotoka. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa wilaya wa NCCR mwaka 1993, akawa mwanachama wa TLP mwaka 1996 na kisha akahamia CUF mwishoni mwa miaka tisini ambako alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (mwaka 1999), ameendelea na nafasi hiyo akichaguliwa kila mara na hata katika uchaguzi wa ndani ya CUF uliofanyika Juni 2014, Barwany alichaguliwa tena kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa, wadhifa ambao anatarajiwa kuushikilia hadi mwaka 2019. Pia, yeye ndiye mwenyekiti wa CUF wilaya ya Lindi Mjini kwa zaidi ya muongo mmoja.
Pamoja na uzoefu mkubwa wa Barwany, anakabiliwa na kitisho kikubwa katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu kwa sababu kiongozi mwingine wa CCM, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi anayewakilisha Wilaya ya Lindi Mjini, Mama Salma Kikwete “First Lady wa Tanzania” anatarajiwa kuomba ridhaa ya kugombea katika jimbo hilohilo kwa tiketi ya CCM.
Mama Salma amekwishafanya ziara nyingi Lindi Mjini na ni tishio hasa kwa uongozi wa Barwany na CUF. Majaliwa ya jimbo hili kuendelea kuwa chini ya CUF na Ukawa yatategemea zaidi na namna Barwany mwenyewe, CUF na vyama vya Ukawa vitakavyojipanga ili kuhakikisha jimbo hili linatoa matokeo bora kwa Ukawa. Ikiwa Mama Salma Kikwete atagombea kupitia CCM nachelea kutabiri nini kitatokea, jimbo la Lindi Mjini linabaki 50 kwa 50 kati ya Ukawa na CCM.
WILAYA YA RUANGWA
Wilaya ya Ruangwa ni moja kati ya wilaya sita za mkoa wa Lindi na inapakana na wilaya ya Liwale kwa upande wa Kaskazini, wilaya ya Nachingwea kwa upande wa Kusini na Mkoa wa Morogoro kwa upande wa Magharibi.
Wakazi wa Ruangwa wanajishughulisha zaidi na masuala ya kilimo cha mazao ya biashara hasa korosho na ufuta na wanashiriki katika uchimbaji wa madini na vito mbalimbali vya thamani kwenye maeneo ya Namungo (Mbekenyera) Mandawa, Kitandi na Nambilanje.
Vito vya thamani ambavyo vimekuwa vikipatikana hapa ni Green tomalin/garnet, Red Garnet, Blue Sapphire, Rhodolites, Emarolds, Pigment materials (External Rendering Rangi ya puchi) Acquamarine na alexandarite.
JIMBO LA RUANGWA
Jimbo hili ndilo linaunda wilaya nzima ya Ruangwa na limekuwa ngome ya CCM kisiasa kwa muda mrefu. Vyama vya upinzani vilianza kuwa na nguvu hapa Ruangwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2009 na kuongezeka zaidi katika chaguzi zilizofuata.
Kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 pamoja na uchaguzi mkuu wa kihistoria ndani ya nchi yetu mwaka 1995 kulishuhudia mpambano wa kisiasa lakini ukikua polepole. Katika uchaguzi wa mwaka 1995 CCM ilikuwa imejipanga, na ilifanikiwa kulichukua jimbo la Ruangwa bila kizingiti kikubwa kutoka kwa upinzani. Ni msomi mwenye shahada ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, Philip Alfred Magani ndiye aliyevaa viatu vya uongozi wa jimbo hili na akafanikiwa kufanya hivyo hadi mwaka 2000.
Bila shida, CCM ilimrejesha tena Philip Alfred Magani kuomba ridhaa ya kuwaongoza wana Ruangwa kwa mara nyingine mwaka 2000. Mwana kilimo huyu ambaye amewahi kuwa Meneja Mkuu wa CRDB na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, hakupata upinzani wowote mkubwa na alilipata jimbo kwa mteremko akawa mbunge wa Ruangwa kwa tiketi ya CCM kwa mara ya pili (2000 – 2005).
Mwaka 2005 ulikuwa tofauti kidogo ndani ya CCM jimboni Ruangwa. Mambo mawili yalitokea: La kwanza ni CCM kuleta mgombea mpya na la pili kukua polepole kwa vyama vya CUF na Chadema. Katika uchaguzi wa mara hii, bendera ya CCM ilipeperushwa na Sigifrid Selemani Ng’itu (marehemu). Matokeo ya mwisho yalimpa ushindi Selemani Ng’itu wa CCM ambaye alipata kura 39,167 (asilimia 78.8) huku akifuatiwa na Mohamed Said Kutwambi wa CUF aliyekuwa na kura 7, 478 (asilimia 15.0) na Chadema ikiwakilishwa na Juma Hamisi Lichonyo ikajipatia kura 2,499 (asilimia 5.0) na kuchukua nafasi ya tatu.
Selemani Ng’itu aliliongoza jimbo la Ruangwa lakini mola alimpenda zaidi kabla ya kumaliza kazi yake, alifariki dunia Novemba 2, 2009 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu. Kwa sababu alifariki mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi Mkuu mwingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ililazimika kufuata sheria na kutotangaza uchaguzi wa marudio katika jimbo hilo.
Oktoba 2010 haikuwa mbali sana, ghafla ilifika na vyama viwili peke yake ndivyo vilijipanga ukizingatia kuwa mbunge aliyekuwa anaongoza jimbo hili alishatangulia mbele ya haki. Chama cha Mapinduzi (CCM) kikamleta Majaliwa Kassim Majaliwa huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiwakilishwa na Abubakar Safi Kondo. Matokeo yalipotangazwa, Majaliwa wa CCM ndiye aliyekuwa mshindi kutokana na asilimia 72.98 (kura 27,671) na Abubakar wa CUF alipata asilimia 23.8 (kura 9,024).
Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge, Majaliwa ambaye ana stashahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Stockholm – Sweden na shahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa wizara ya Tamisemi. Pamoja na kuutaka ubunge mwezi Oktoba, Majaliwa anakabiliwa na changamoto kubwa jimboni mwake hasa zinazotokana na wakulima wa korosho kunyimwa stahili zao. Ikiwa CUF itajipanga vizuri, ikapata mgombea mpambanaji na mwenye nguvu, jimbo la Ruangwa ni jepesi sana, lakini akikosekana mtu anayekubalika na mwenye sifa za kuchagulika (za juu au zinazolingana na Majaliwa) – jimbo hili litaendelea kuwa mali ya CCM.
Ukiongea na wananchi wa Ruangwa utaona kabisa hisia zao juu ya mbunge wao, hawamsemi vizuri. CUF kupitia Ukawa isipojipambanua vizuri, CCM watachekelea sana, kwamba wameendelea kulimiliki jimbo ambalo kwa hakika lilipaswa kwenda upinzani.
Kesho Jumapili tutaendelea na majimbo ya Kilwa Kaskazini, Kilwa Kusini na Liwale.
(Julius Mtatiro ana uzoefu mkubwa wa uongozi katika siasa. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759, “mailto:[email protected]” [email protected] – Uchambuzi huu ni maoni binafsi ya mwandishi).