Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msemo huu unatafakarisha, wahusika chukueni hatua

Kuna msemo ambao siku hizi unasikika mara kwa mara katika mikusanyiko ya wananchi, kwenye mitandao ya kijamii na hata katika vijiwe vya mazungumzo utasikia wanasema; "Huyo anatuletea siasa."

Cha kushangaza mara nyingi kauli hiyo huwa haitolewi tu pale kiongozi anapozungumzia uchaguzi au chama cha siasa. Hata anapozungumzia miradi ya maendeleo au jambo lolote linalotaka kutanzua mkwamo fulani kwa watu, wapo wanaohitimisha kuwa anafanya siasa.

Swali la kujiuliza ni kwa nini hali imefikia hapo? Kwa nini sehemu ya wananchi imeanza kutafsiri karibu kila kauli ya viongozi kwa ‘miwani’ ya kisiasa badala ya kuiona kama mawasiliano ya kawaida ya uongozi?

Binafsi naona jibu lake si rahisi kwa sababu linatokana na sababu nyingi zinazoshabihiana. Kwanza, mipaka kati ya shughuli za kisiasa na shughuli za kiutawala imezidi kuwa finyu. Mara nyingi viongozi wana majukumu ya kisiasa na wakati huohuo ni viongozi wa umma. Wanapozungumza mbele ya wananchi, wakati mwingine huchanganya maelezo ya utekelezaji wa majukumu yao na ujumbe wenye mwelekeo wa kisiasa.

Kwa mwananchi wa kawaida, si rahisi kutenganisha ni wapi taarifa ya Serikali inaishia na wapi ujumbe wa kisiasa unaanzia.

Pia, naona kama nchi imeingia katika zama ambazo mawasiliano ya viongozi yanasambazwa kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii. Kauli moja inaweza kukatwa sekunde chache na kusambazwa bila muktadha wake.

Wengine huichambua kwa mtazamo wa kisiasa, wengine kwa mtazamo wa kijamii na wengine kwa hisia binafsi. Mwishowe, maana halisi ya ujumbe hupotea na kinachobaki ni mjadala wa kisiasa.

Sababu nyingine ni historia ya mawasiliano yenyewe. Kwa miaka mingi, wananchi wamezoea kuona viongozi wakionekana hadharani zaidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa nchi.

Hali hiyo imejenga mtazamo kwamba kila kiongozi anapozungumza sana hadharani, huenda kuna agenda ya kisiasa inayofuatia. Hata pale anapotekeleza wajibu wake wa kawaida, baadhi ya wananchi hutafsiri kwa mtazamo huo.

Aidha, kuongezeka kwa mijadala ya kisiasa kwenye majukwaa ya kidijitali pia kumebadili namna watu wanavyopokea taarifa.

Hivyo, leo hii, karibu kila jambo linaweza kugawanya mitazamo. Habari kuhusu mradi wa maendeleo inaweza kutafsiriwa kisiasa; kauli kuhusu elimu inaweza kuibua mjadala wa kisiasa; hata taarifa ya afya inaweza kuhusishwa na siasa.

Hii inaonyesha kuwa wakati mwingine tatizo halipo kwenye kauli yenyewe, bali kwenye namna inavyopokelewa.

Lakini si jukumu la wananchi pekee, viongozi pia wana wajibu wa kujenga mazingira ya mawasiliano yanayopunguza tafsiri zinazokinzana.

Kauli zisizoeleweka, zenye utata au zinazoweza kueleweka kwa namna tofauti huwaacha wananchi na maswali mengi kuliko majibu. Katika zama ambazo taarifa husafiri kwa sekunde chache, uchaguzi wa maneno unakuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Pia kuna suala la imani. Pale ambapo wananchi wana imani kubwa na taasisi na viongozi wao, huwa rahisi kupokea taarifa kama zilivyo.

Lakini pale kiwango cha imani kinapopungua, hata ujumbe ulioandaliwa kwa nia njema unaweza kutafsiriwa kwa mashaka. Hivyo, mawasiliano bora hayaishii kwenye uchaguzi wa maneno; yanategemea pia kiwango cha uaminifu kilichojengwa kati ya viongozi na wananchi.

Hivyo suluhisho ni kwa watawala kuanza upya kujenga utamaduni wa mawasiliano unaoweka wazi tofauti kati ya taarifa za utekelezaji wa majukumu ya umma na ujumbe wa kisiasa. Wananchi wanahitaji kupata taarifa zilizo wazi, zenye ushahidi na zinazojibu maswali muhimu kuhusu maisha yao.

Kadiri taarifa zinavyokuwa wazi na zenye kueleweka, ndivyo nafasi ya tafsiri zinazozua mabishano zinavyopungua pia. Viongozi wanapaswa kuendelea kusisitiza hoja kuliko hisia, takwimu kuliko kauli za jumla na maelezo kuliko misemo inayoweza kutafsiriwa kwa namna mbalimbali. Hilo litasaidia kujenga mawasiliano yanayoaminika na kupunguza hisia kwamba kila tamko lina lenga mtazamo wa siasa.

Kwa upande mwingine, wananchi nao wana wajibu wa kusikiliza ujumbe kwa ukamilifu kabla ya kuuhukumu. Kusoma, kusikiliza na kutafuta muktadha ni sehemu ya uwajibikaji wa kiraia.

Vyombo vya habari navyo vina nafasi muhimu. Vinapaswa kuendelea kutoa taarifa kwa usahihi, kuweka kauli katika muktadha wake na kutenganisha habari na maoni. Hilo naona litawasaidia wananchi kujenga uelewa mpana badala ya kuongozwa na vipande vya taarifa vinavyosambaa mitandaoni