Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwelekeo wa elimu mpya kwa wote na matumaini yake

Katika kipindi cha miaka minne yaani 2020 mpaka 2024, sekta ya elimu nchini imepiga hatua kubwa, hususan kupitia mpango wa elimu bila ada na uboreshaji wa miundombinu ya shule.

Miundombinu inayoendelea kuboreshwa ni ile ya kuanzia shule za awali hadi za sekondari. Kwa kipindi kirefu, ilikuwa na changamoto lukuki zilizoonekana kutopatiwa majibu ya moja kwa moja.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, tumeanza kuona mafanikio hususan pale Serikali ilipoamua kwa dhati kuanza kukarabati, kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali ya shule inazomiliki kuanzia za awali mpaka sekondari.

Ndani ya miaka minne sasa, kuna ongezeko kubwa la vyumba vya madarasa sambamba na idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za msingi na sekondari.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, vyumba vya madarasa ya msingi vimeongezeka kutoka 128,425 mwaka 2020 hadi 155,330 mwaka 2024, ongezeko la asilimia 20.95.

Kwa sekondari, ongezeko ni la asilimia 72.71, kutoka vyumba 46,928 hadi 81,052. Hali hii imeongeza fursa ya upatikanaji wa elimu hasa vijijini, ambapo watoto wengi walikuwa wakikosa masomo kutokana na umbali au msongamano wa wanafunzi darasani.

Hata hivyo, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) inaelekeza idadi ya wanafunzi inayostahili kuwapo katika darasa moja kuwa ni 45 kwa shule za msingi na 35 kwa sekondari.

Mwaka 2022, uwiano wa darasa kwa wanafunzi ulikuwa 1:70 kwa msingi na 1:36 kwa sekondari. Hii inaonyesha kuwa licha ya hatua zilizopigwa, bado kuna changamoto ya msongamano wa wanafunzi.

Aidha, idadi ya wanafunzi waliokuwa wakinufaika na elimu bila ada imeongezeka kutoka milioni 14.9 mwaka 2020 hadi milioni 16.1 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 8.3.

Idadi hii kubwa ya wanufaika inaonyesha mafanikio ya mpango huo, hasa kwa watoto kutoka familia masikini ambao hapo awali walikuwa wanakosa elimu kutokana na gharama za ada.

Serikali pia imeongeza bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bila ada kutoka Sh312.06 bilioni kwa mwaka 2020 hadi kufikia Sh796.39 bilioni kwa mwaka 2024. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 155.16.

Fedha hizi zinagharamia uendeshaji wa shule, vifaa vya kujifunzia, pamoja na mahitaji ya msingi ya wanafunzi.

Katika juhudi za kuhakikisha kila mwanafunzi anapata kitabu chake, taasisi mbalimbali zimeshirikishwa. Mfano, Machi 2025, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ilianzisha harambee ya kuchangia zaidi ya Shilingi bilioni 297.29 kwa ajili ya kuchapisha vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia.

Harambee hiyo iliongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na iliwahusisha wadau kutoka sekta binafsi, mashirika ya dini na wananchi wa kawaida.

Binafsi nautazama mpango huu kuwa umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mzigo wa gharama kwa wazazi na kuziwezesha familia nyingi kuwekeza katika maeneo mengine kama afya na biashara ndogo.

Na hii inathibitishwa na Ripoti ya mwaka 2025 ya Tanzania Digest inayoonyesha kuwa mpango wa elimu bila ada umeongeza usajili wa wanafunzi hadi asilimia 27.9 kwa sekondari na asilimia 95.5 kwa msingi.

Utafiti mwingine wa mwaka 2022 mkoani Morogoro unaonyesha kuwa wazazi wamepata unafuu mkubwa na wanafunzi wengi wamejiunga na shule.

Pia, mpango huu umeongeza fursa za elimu kwa wasichana, hivyo kuchangia kupunguza pengo la kijinsia katika elimu.

Rais Samia amekuwa akisisitiza usawa katika elimu baina ya wasichana na wavulana, akiamini kuwa kila mtoto anapaswa kuwa na nafasi sawa ya kuchangia maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, changamoto bado zipo. Ripoti ya Hakielimu ya Mei 2025 inaeleza kuwa kuna upungufu wa walimu 268,902, hasa kwa masomo ya sayansi kama Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Pia, uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia bado ni changamoto kubwa kwa shule nyingi nchini.

Serikali imeanza kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hizo. Novemba 2022, Waziri Mkuu alizindua mpango wa kugawa vishikwambi kwa walimu ili kuwawezesha kutumia teknolojia kufundisha madarasa mengi kwa wakati mmoja. Vilevile, Juni 2025, Naibu Waziri wa Tamisemi, Zainab Katimba, alizindua awamu ya pili ya utoaji wa vifaa vya Tehama kwa shule 422, kwa gharama ya zaidi ya Sh12 bilioni.

Kwa ujumla, juhudi hizi zinaweka msingi thabiti wa kufanikisha malengo ya kitaifa ya kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora ifikapo mwaka 2030, sambamba na kujenga taifa lenye nguvu kazi yenye ujuzi itakayowezesha kukuza uchumi na maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.

Mchambuzi anapatikana kwa namba ya simu; 0763154141