Mzimu wa ndoa za utotoni unavyohusishwa na mahari

Muktasari:
Licha ya kuwepo kwa sheria kali, huku baadhi ya watuhumiwa wakikamatwa na kupewa kifungo cha miaka 30 jela, bado mzimu wa ndoa za utotoni unaendelea kuzitafuna familia nyingi.
Licha ya kuwepo kwa sheria kali, huku baadhi ya watuhumiwa wakikamatwa na kupewa kifungo cha miaka 30 jela, bado mzimu wa ndoa za utotoni unaendelea kuzitafuna familia nyingi.
Baadhi ya wazazi, walezi na jamii zinazogubikwa na mzimu huu zinaangamia kwa sababu ya malipo manono ya mahari.
Kwa mfano, baadhi ya familia za jamii ya wafugaji zimekuwa zikivuna kati ya ng’ombe 15 hadi 30 ikiwa zitaozesha binti.
Kwa bei ya chini ya Sh300,000 kwa ng’ombe mmoja kijijini, mzazi au mlezi anapobaini kuchuma zaidi ya Sh5 milioni ikiwa atamuozesha binti yake, huwa haoni shida kukatisha ndoto zake za kielimu.
Mara kadhaa vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti ndoa zile zilizofikiwa kisha watoto kuokolewa, sasa vipi kwa watoto ambao ndoa zao ziliendeshwa kibubu?
Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi 11 duniani zenye mabibi harusi watoto baada ya makadirio kuonyesha wanawake watatu kati ya 10 waliingia kwenye ndoa wakiwa na umri chini ya miaka 18.
Takwimu hizo zilibainika Julai 2022, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Binti ya kukomesha ndoa za utotoni iliyohusisha vijana balehe, viongozi wa dini, wafanyabiashara, vyama vya kiraia na mashirika la Umoja wa Mataifa, likiwamo Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (Unicef) nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi kupitia uzinduzi huo alisema suala la ndoa za utotoni nchini limechelewa kufanyiwa mabadiliko ndio maana linaendelea kushamiri.
Hata hivyo, wadau wa masuala ya watoto wanalalamikia Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, inayoruhusu ndoa za watoto wenye umri wa miaka 15.
Kwa mujibu wa Unicef, Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa ndoa za utotoni, ukiwa na asilimia 59, Tabora (55) na Mara (55).
Inaeleza kuwa asilimia 31 ya wasichana nchini wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na asilimia tano kabla ya miaka 15.
Kwa mujibu wa wanasaikolojia na wanaharakati, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inapoingia kwenye jamii inayoongozwa na mila zinazoruhusu watoto chini ya umri wa miaka 18 kuozeshwa, hali inakuwa mbaya zaidi.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Regional Psychosocial Support Initiative (Repssi), Edwick Mapalala anasema sio rahisi kujenga msingi imara wa familia inayokumbatia na kuenzi ndoa za utotoni.
Anasema watoto wanatakiwa kusoma na kufikia ndoto zao za kimaisha bila kukatishwa njiani.
“Wanayo haki ya kufurahia utoto wao lakini hali ikiendelea hivi, huko mbele familia zitakosa mwelekeo, tutakuwa na wajukuu na vitukuu ambavyo hatutavifurahia kama sisi tunavyofurahiwa,” anasema Mapalala.
Anasema hali inazidi kuwa mbaya hasa wakati huu wa utandawazi.
“Sio tu wazazi na walezi peke yao ndio wanaolazimisha watoto wao kuolewa au kuwa na uhusiano, hata maisha yalivyo yanawalazimisha wato-to wafanye hivyo,” anasema Mapalala.
“Fikiria mtoto analelewa na televisheni, simu za mkononi hata huko vijijini kuna vibanda umiza. Ukienda shuleni watoto wanajua mambo makubwa sio kwa kufundishwa na wazazi au walezi ila kutazama. Tutaepukaje ndoa za utotoni?” anasema Mapalala.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Iringa, Dk Blaston Gavile anasema kuna haja kwa familia kurudi kwenye misingi ya awali ya malezi.
Matukio ya ndoa za utotoni
Siku chache zilizopita, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme alizima ndoa ya mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika moja ya shule za sekondari zilizopo Tabora.
Wazazi wa mtoto huyo walikuwa wanataka kukatisha ndoto zake kwa kumuozesha.
Ndoa hiyo ilikuwa inafungwa katika Kijiji cha Mwawaza, Wilaya ya Shinyanga baada ya wazazi wa mwanafunzi huyo kudaiwa kupokea mahari ya ng’ombe 15 kwa kijana mwenye umri wa miaka 21.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, mwanafunzi huyo aliyelipiwa mahari ya ng’ombe 15 bado yupo chini ya uangalizi maalumu.
Agosti 16 mwaka jana, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maofisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, walizuia ndoa ya utotoni aliyokuwa akifungishwa mtoto wa miaka 15 kwa mahari ya ng'ombe kumi na Sh200,000 kwa mtoto mwenzake mwenye miaka 17.
Ndoa hiyo ilikuwa inafungishwa katika Kijiji cha Manyada, Kata ya Usanda.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Deus Mhoja alisema walipata taarifa ya kufungishwa ndoa ya mtoto huyo kutoka kwa wasamaria wema, ndipo wakapanga mikakati ya kwenda kuizuia kufungwa.
Tukio jingine la ndoa ya utotoni iliyozuiliwa lilimuhusisha mwanafunzi wa kidato cha pili (15) Shule ya Sekondari Chamazi.
Mwanafunzi huyo alinusurika kuolewa baada ya Serikali kuingilia kati, huku mumewe mtarajiwa na mshenga wakikamatwa na polisi.
Wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro kamati ya usalama ya wilaya hiyo ilizima ndoa ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza Madege Sekondari aliyekuwa anataka kuolewa.
Wasichana waliokimbia kuozeshwa
“Hata kama nipo darasani sina furaha kwa sababu wadogo zangu wameshaozeshwa na sasa wanaishi kwa waume zao! Mmoja ana miaka 14 na mwingine 16,” anasema msichana aliyekimbia kuozeshwa.
Msichana huyu na wenzake wawili wanaosoma Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Namnyaki, Kijiji cha Image, Wilayani Kilolo, Mkoa wa Iringa walikimbia kuozeshwa baada ya kumaliza darasa la saba.
“Kabla sijaanza mitihani ya darasa la saba, baba aliniita akaniambia ole wangu nifaulu, aliniambia natakiwa niboronge kwa sababu yeye hana pesa ya kunilipia ada,” anaanza kusimulia Anitha, ambaye wakati huo alikuwa na miaka 14.
Anasema siku ya mtihani wake wa darasa la saba, mama yake aliyekuwa mjamzito alipata maumivu na kukimbizwa hopitali kwa ajili ya kujifungua.
“Bahati mbaya mama yangu alijifungua pacha walioungana, hivyo alibaki kulekule hospitali, hakurudi nyumbani.
“Nilipomaliza mitihani baba akauliza tena, mitihani ilikuwaje? Nikasema ilikuwa migumu, akauliza kama nitafaulu nikasema sijui kama nitafaulu,” anasema Anitha.
Anasema kwa sababu mama yake alikuwa bado anawauguza wadogo zake, alimuomba pesa baba yake ili aende Hospitali ya Ipamba kumtazama mama yake.
“Baba alinipatia nauli, nikapanda kwenye basi, kumbe alikuwa amewatuma vijana waniteke,” aliongea kwa uchungu na kuinama chini akilia.
Anasema hakujua kama baba yake anataka kumuozesha, aliamini kuwa haendi shule kwa sababu hana ada ya kumlipia.
Anitha anasema siku hiyo alipanda basi na alipofika njiapanda ya Tosamaganga, alishuka na kukuta bajaji imepaki kama inasubiri abiria. Alikaribishwa kwenye bajaji hiyo akaingia akijua inaelekea kwa mama yake kwa sababu walionekana kumfahamu.
“Vijana hawa na bajaji waligeuza kurudi nilikokuwa nimetokea. Walinipeleka kijiji kingine na mimi nilijua ndio hospitali. Nilipofika nikashangaa na kuwauliza, wakaniambia hakuna shida, kumbe baba aliandaa mpango wanitoroshe. Kisha niolewe. Nilifanikiwa kukimbia na nipo darasani,” anasema Anitha.
Msichana mwingine ambaye hakutaja jina lake anasema, “nilitoroka nyumbani kwa sababu baba alitaka kuniozesha, aliniambia wazi natakiwa niolewe na sio kusoma.”
Msichana huyo kutoka Kilosa, mkoani Morogoro anasema baada ya kumaliza darasa la saba, baba yake alimtafutia mume ili amuoe.
“Yule mwanamume alikuwa mzee, mwanzoni sikujua kama anakuja kunioa lakini baadaye mdogo wangu akanitonya. Nilijifanya sijui, wakalipa mahari,” anasema kilichomsaidia ni uamuzi wake wa kutoroka na sasa anaendelea na masomo yake.
Msichana mwingine, Neema anasema aliambiwa ajifelishe ili matokeo yakitoka, asichaguliwe na aolewe.
Neema anasema matokeo yalipotoka alikuwa amefaulu vizuri, jambo lililomuudhi baba yake.
“Akaanza kumkaripia mama kwa nini hajakaa na mimi kunielewesha ili nisifaulu darasa la saba, ndio baba akawa ameongea na mtu ili aje anitoroshe nikaolewe.
“Siku moja nimeenda shambani mama wa jirani akamuuliza mama yangu kwa nini sijaenda shuleni? Mama akamwambia baba hataki nisome, ndio yule mama akaniambia kuna shule inasaidia wasichana walio hatarini kuozeshwa, akaniunganisha na hii shule sasa hivi nipo kidato cha tatu,” anasema Neema.
Mkurugenzi wa Sekondari ya Wasichana ya Namnyaki, Mchungaji Paulo Ole Kampashi anakiri kuwa familia nyingi zimekuwa zikizima ndoto za watoto kielimu kwa sababu ya kukumbatia mila na desturi.
Ole Kampashi anasema bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuwaokoa watoto wa kike wengi ambao ndoto zao za elimu zinapotea kutokana na uwepo wa ndoa za utotoni.
Mapalala anasema lazima hatua zichukuliwe ili kupambana na hali hiyo.
“Hatua hizi sio za Serikali peke yake, ni jamii nzima,” anasisitiza.
Mkuu wa Dawati la Jinsia la Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai anasema zipo athari nyingi za ndoa kwenye umri mdogo, ikiwamo ukatili na mateso wakishaozeshwa kinguvu.
“Tunapokea kesi za ukatili na tunajitahidi kuzitatua, huku wale wanaofanya makosa wakichukuliwa hatua za kisheria. Changamoto ni kwamba, sio tu wanawake wanaofanyiwa ukatili, hata wanaume pia, japo waathirika ni wale walio na umri mdogo,” anasema.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Ilula Ophan Program (IOP), Edson Msigwa anasema ndoa za utotoni bado ni janga, hasa wanakoishi wafugaji, wakiwamo Wamasai.
“Tunajitahidi kuwafikia jamii zote na hapa kwenye kituo chetu tunaishi na wasichana waliokimbia ndoa za utotoni,” anasema Msigwa.
Nini kinafanyika
Mwakilishi wa Unicef Tanzania, Shalini Bahuguna anasema inabidi kutazama kwa makini fursa ambazo watoto wa kike wanazikosa kwa sababu ya ndoa za utotoni.
"Pale wasichana wanapowekewa mazingira ya kutarajia kupoteza elimu yao, utoto wao na ndoto zao ili waoelewe, ni jambo linalodhuru afya yao ya akili, na wanawekwa katika hatari ya kukumbwa na ukatili kila siku, unyonyaji, changamoto za kiafya na umaskini. Hawawezi kutimiza vipawa vyao na kutoa mchango wa maana katika jamii,” anasema Bahuguna.