Nafasi ya Mbowe uchaguzi wa mwenyekiti Chadema
Joto kali limepanda ndani ya Chadema baada ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na makamu wake, Tundu Lissu kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo.
Awali, Lissu alikuwa ametangaza kutetea nafasi yake ya umakamu mwenyekiti, lakini baadaye akabadilisha msimamo na kujitosa kwenye uenyekiti.
Wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbowe alieleza sababu ya kuendelea kugombea nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 20, akisema bado ana nguvu na kwamba kuna mambo makubwa ya kushughulikia, likiwamo dai la Katiba mpya na mfumo wa uchaguzi.
Ukimsikiliza Lissu katika hoja zake, anaeleza haja ya kuwa na mwenyekiti mpya baada ya miaka 20 ya Mbowe, huku akisisitiza haja ya kuwa na ukomo wa madaraka, mfumo bora wa fedha, mfumo bora wa uchaguzi.
Katika tathmini mbalimbali kuhusu wagombea hawa, utaona kila mmoja ana nguvu na udhaifu kwa upande mwingine.
Kura za maoni kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha Lissu anaungwa mkono zaidi na wapenda mabadiliko ndani na nje ya chama hicho, wakiwamo wanaharakati wa masuala ya Katiba wasio na vyama, lakini kwa upande wa ndani ya chama, wengi wanaomuunga mkono ni wanachama wa vyeo vya chini wasio na uamuzi. Hiyo inaweza kumgharimu kwenye uchaguzi huo.
Kwa upande wa Mbowe, anaonekana kuungwa mkono zaidi na viongozi waandamizi wa chama hicho, wakiwamo wenyeviti wa kanda, wenyeviti wa mikoa na wengineo ambao wengi wao ni wapigakura. Hiyo ni faida kwa sababu inampa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi kirahisi.
Hata hivyo, changamoto ambayo naona itakayomkabili Mbowe ni kundi kubwa la wananchi waliojenga matumaini kwa chama hicho kwa muda mrefu. Hivyo, atakuwa na kazi kubwa ya kurejesha imani ya watu hao ambao wengi si wanachama wa Chadema.
Kuna kundi kubwa la watu, hasa vijana wanatamani nchi ipate mabadiliko ya kisiasa, ikiwemo kuiondoa CCM madarakani, lakini wamechoshwa na mwenendo wa Chadema, huku baadhi yao wakiona chama hicho kimepoa.
Katika mkutano wake huo, Mbowe alieleza umuhimu wa maridhiano, akasema sio lazima kuridhiana na CCM, bali hata makundi mengine, yakiwamo ya viongozi wa dini, wanaharakati, wanasiasa na wasomi.
Kwa hiyo, endapo Mbowe atashinda, ana kibarua kigumu cha kuyaaminisha makundi hayo na wapigakura wengine kuwa ana mikakati madhubuti ya kuipaisha Chadema ndani ya kipindi kifupi.
Katika suala hilo la maridhiano, linalolalamikiwa na makada wa chama hicho, ni kushikamana mno na CCM.
Inaonyesha hakukuwa na umakini wa kutosha katika kushughulikia suala hilo, mpaka baadhi ya wanachama wakaanza kulalamika kwamba chama kimejilegeza mno kwenye maridhiano hayo.
Katika hatua hiyo, ndipo ikaonekana Chadema ilijitoa kwenye mazungumzo ya maridhiano na kuambulia faida hizo, zikiwamo za kuachiliwa kwa waliodaiwa kushitakiwa kisiasa, kupewa ruzuku, waliokimbia nje ya nchi kurudi na nyinginezo.
Maoni yanayotolewa na wadau, wakiwamo wanachama wa Chadema ni kukifanya chama hicho kuongeza makali katika kudai mabadiliko ya Katiba na mfumo bora wa uchaguzi.
Pamoja na umakini na busara za Mbowe, hasa anaposhughulikia migogoro ndani ya chama chake, lakini ameonekana kufumbia macho mambo mengi ndani ya chama hicho na ndiyo yanaibuliwa na viongozi wenzake.
Tumesikia malalamiko ya chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho, huku nyingine zikiahirishwa. Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema alimlalamikia mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho kuwa alihusika katika vurugu za uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa mkoa huo. Je, huyo kiongozi amechukuliwa hatua gani?
Kuna malalamiko yaliyotolewa kuhusu ukomo wa madaraka, mfumo wa uchaguzi na wa fedha. Yote Mbowe ameyajibu, lakini yamekuwa yakijirudiarudia mno. Lisemwalo lipo, kama halipo linakuja.
Mbowe anabebwa na historia nzuri ndani ya Chadema ya kukitoa chama hicho kutoka kuwa chama kidogo hadi chama kikuu cha upinzani nchini.
Pia amekijenga chama hicho kutoka ngazi ya msingi na kukifanya kiaminiwe na watu wengine ambao sio wanachama.
Endapo Mbowe atashinda uchaguzi na kuendelea kuwa mwenyekiti, atakuwa na uwezo wa kukimudu chama hicho kwa uzoefu alionao, lakini bado anakabiliwa na kibarua kigumu cha kulinda imani ya makundi mengine nje ya chama.