Polisi isake kiini cha ujambazi, si kutoa sababu

Muktasari:

  • Matukio ya ujambazi na uhalifu yanayojitokeza hivi sasa yamesababisha wasiwasi kwa jamii, licha ya viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi kuweka bayana kuwa, wanaoshiriki vitendo hivyo watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Matukio ya ujambazi na uhalifu yanayojitokeza hivi sasa yamesababisha wasiwasi kwa jamii, licha ya viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi kuweka bayana kuwa, wanaoshiriki vitendo hivyo watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Kwa takribani mwezi mmoja sasa mkoani Dar es Salaam kumekuwa na matukio ya uhalifu ambapo watu wanaodhaniwa ni majambazi huvamia maduka, majumbani, hupora fedha na kuua baadhi ya watu.

Tunajua vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha amani, utulivu vinaendelea kuwepo nchini, lakini tungependa kazi hiyo ifanywe kwa nguvu na kisasa zaidi ili taswira ya taifa isichafuliwe na wahalifu wachache.

Mei 7, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam alitoa onyo kwa wanaojihusisha na ujambazi na uhalifu waache kupima kina cha maji na kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kulifanyia kazi jambo hilo.

Tunatambua kuwa ulinzi na usalama usipokuwa imara uzalishaji mali nao huwa shakani, taifa nalo husuasua katika maendeleo kwa kuwa wananchi hawawezi kwenda kwenye shughuli za kujitafutia kipato kwa uhuru na amani kwa kuwahofia wahalifu.

Tunaamini katika ulimwengu wa kisasa wa maendeleo ya teknolojia, kamera za kurekodi matukio zingefungwa katika maeneo tofauti tofauti ili wanaofanya uhalifu watambulike mapema.

Tunajua si jambo rahisi kwa askari kuwepo katika kila eneo na kila wakati kutokana na uchache wao, lakini uwepo wa teknolojia za kisasa husaidia kuimarisha ulinzi na kuzuia tukio kabla ya kutendeka.

Tumeshtushwa kusikia kuwa uhalifu unaotokea Dar es Salaam unatokana na ongezeko la idadi ya watu kutoka katika mikoa mingine na wingi wa watu waliotoka gerezani.

Sababu hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Camillius Wambura. Tunaamini Polisi wanapaswa kusaka kiini cha tatizo na si kutoa sababu za kuelezea ukubwa au udogo wa tatizo.

Tunajiuliza hivi katika hiyo mikoa wanayotoka hao wahalifu ndiko kuna ulinzi imara zaidi kuliko Dar es Salaam na ndio sababu wameshindwa kufanya uhalifu wao huko na kuamua kuja Dar ambako kumelegalega?

Kama ni hivyo, kwanini Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wasiwaulize wenzao ni mbinu gani wanazotumia kuwadhibiti wahalifu nao wazitumie?

Tunajiuliza kama Polisi wamebaini watu wengi wanaotoka gerezani hawajaacha tabia za kihalifu kwanini wasizungumze na Jeshi la Magereza na wakaweka mpango mzuri wa kuboresha mafunzo ya kubadili tabia kwa wafungwa na mahabusu?

Tunaamini ushirikishwaji wananchi katika ulinzi pia kutasaidia kufichua wahalifu na vitendo vya kihalifu. Maboresho au mabadiliko yanayofanywa katika jeshi hilo yasiwasahau wananchi.

Tungependa pia Jeshi la Polisi lijitathmini kwa kuwa zipo tuhuma kuwa baadhi ya askari wanashiriki kwenye ujambazi, wizi, kuvujisha siri na kuwaonea watu kwa kuwabambikia makosa.

Tunaamini tathmini ya kina ikifanywa kwa Jeshi la Polisi, likiwashirikisha wananchi, likinunua vifaa vya kisasa na kuendesha misako ya wahalifu haya matukio ya uhalifu na wahalifu yatapungua.