Sababu zinazochochea mpenzi kuchepuka

Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la malalamiko kwa wanandoa wengi kutokuwa waaminifu. Wapo waliokabiliana na misuguano, mapigano na ugomvi kwa sababu ya jambo hilo.

Na wapo ambao tayari wameshaamua kutengana. Watoto wa familia nyingi sana wamebaki kuwa waathirika wa tatizo hili na bado hakuna dalili za tatizo hili kupungua.

Kila mmoja akiulizwa anatoa sababu yake binafsi ya kwa nini ametoka au alitoka nje ya ndoa yake, sababu hizi zinafanana na baadhi zinatofautiana.

Katika makala haya nimejaribu kuangalia baadhi ya sababu ambazo zimeripotiwa na wanandoa wengi wanaokuja kwenye ofisi zetu kwa ajili ya ushauri.

 Hii inafanya sababu hizi kuwa halisi na zitakazokupa msaada ukizielewa maana haziko kinadharia tu, bali zimetokea katika maisha halisi ya ndoa.

Pamoja na yote haya, ukweli unabaki kwamba matendo ya kukosa uaminifu kwenye ndoa au uhusiano yana athari mbaya sana na zinaweza kuambatana na maumivu makali na wahusika kuwa maadui badala ya wapenzi kama walivyokuwa awali.


Kutoridhishwa tendo la ndoa

Yamekuwepo malalamiko mengi kwa wanandoa wanaume na wanawake katika suala hili la tendo la ndoa.

Wanaume wanalalamika wake zao baada ya kuolewa na hususan wakishapata watoto wanaanza kuwa wazembe na wasiojituma kwenye tendo la ndoa kama walivyokuwa awali. Tafiti zinaonyesha mwanamume anapohisi kutoridhishwa kwenye tendo la ndoa ana nafasi kubwa zaidi ya kutoka nje mapema kuliko mke wake.

Wanawake wana uvumulivu wa ziada na kwa wale waliotoka nje ya ndoa zao walifanya hivyo baada ya uvumilivu wa miaka mingi na kukosa tumaini.

Kutoridhishwa katika tendo la ndoa kunaweza pia kusababishwa na maumbile ya mwili, kwa mfano watu wenye miili mikubwa na uzito mkubwa hupata shida kwenye kuwaridhisha wenzao ukizingatia kwamba tendo la ndoa ni zoezi la kimwili “physical exercise.”

Mtu wa jinsi hii anaweza kushindwa kwa sababu ya ukubwa wa mwili, kushindwa kuutuma mwili wake kadiri anavyotaka na pia wengine kuishiwa pumzi au kuchoka mapema, hivyo kufika kileleni mapema sana.

Hali hii husababisha kutoridhika kwa wanawake wengi sana kwenye ndoa.

Sababu nyinginezo zilizotajwa za wanandoa kutoridhishana kwenye tendo la ndoa ni kama vile uchafu, harufu zisizo nzuri, uelewa mdogo wa namna ya ufanywaji wa tendo hilo, makuzi na mapokeo, mambo yanayohusiana na mila, utamaduni au imani pamoja na magonjwa.

Pia, kutopata tendo la ndoa kwa muda mrefu ni sababu inayotajwa huku waathirika ni wanaume kuliko wanawake.

Tunaposema muda mrefu, hili ni suala la tofauti kwa mwanamume na mwanamke. Kwa mwanamume wiki moja yaweza kuhesabika ni muda mrefu kulingana na mazoea yaliyokuwepo kwenye ndoa hiyo.

Kisayansi na kibaiolojia, mwanamke ana uwezo wa kustahimili au kuvumilia kukaa bila kufanya tendo la ndoa kwa muda mrefu kuliko mwanamume.

Baadhi ya tafiti pia zimeonyesha watoto wengi wa nje ya ndoa wanazaliwa katika vipindi ambavyo tendo la ndoa lina shida, hii inamaanisha nyakati za ugonjwa, ujauzito, ugomvi au mambo mengine yaliyofanya mwanamume asipate tendo la ndoa.

Katika kipindi hicho mwanamume huamua kwenda pembeni na huko kukatokea mimba na baadaye mtoto. Utaelewa ukubwa au kiasi cha tatizo kwa kuangalia ukweli kwamba kwenye ndoa nyingi, wanaume ndio wanaoongoza kwa kuwa na watoto nje ya ndoa na sio wanawake.

Katika jambo hili la kutokupeana tendo la ndoa kwa muda mrefu, tumekuwa tukishauri kila mwanandoa ahakikishe anaweza kuzuia migogoro isiathiri tendo la ndoa ili wasikae muda bila kulifanya, na kama kuna safari au utengano wa lazima baina yao basi kuwepo na mawasiliano ya mara kwa mara na ikibidi wanandoa watembeleane.

 Umbali una athari kubwa sana kwenye ndoa nyingi. Kwa mara nyingine niseme hili, kunyimana tendo la ndoa kama adhabu au kwa matakwa yoyote binafsi hakujengi, bali kunabomoa, kwa sababu wengi wamejikuta wakitoka nje ya ndoa zao kwa sababu hii.