Siku 12 za kutafakari tunaingiaje mwaka 2024

Tuna siku 12 za kumaliza mwaka 2023, natamani tutumie siku zilizobaki kuingia mwaka 2024 kutafakari kama taifa tulipotoka, tulipo na tunakokwenda, hasa tukizingatia matukio makubwa mawili, uchaguzi mkuu na wa Serikali za Mitaa.

Nasema hivyo kwa sababu tukiingia katika matukio hayo mawili bila maridhiano ya kitaifa, umoja na mshikamano kama Watanzania na sheria bora za uchaguzi, ninachelea kusema huko tuendako kunaweza kuwa giza, tena giza nene sana.

Kwa sababu sote ni Watanzania na hakuna mwenye hati miliki ya urais, ubunge, udiwani, kijiji ama kitongoji, hebu viongozi wenye dhamana ya uongozi waone fahari ya kutuachia kumbukumbu inayoishi hata kama bado wako hai leo.

Mwanazuoni na mwandishi wa vitabu Kalu Ndukwe Kalu wa Marekani anasema na hapa namnukuu: “The things you do for yourself are gone when you are gone, but the things you do for others remain as your legacy,” mwisho wa kunukuu.

Kwa tafsiri yangu ni kwamba vitu unavyojifanyia binafsi vinaondoka wakati unapokuwa umeondoka (duniani), lakini vitu vile unavyovifanya kwa ajili ya wengine, hivyo vitaendelea kubaki kama kumbukumbu inayoishi.

Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi naye alipata kusema, “maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa duniani na kutaka kila mmoja afanye lililo jema ili wawe hadithi nzuri kwa watakaosimuliwa atakapokuwa hayupo duniani”.

Wakati anakaribia miaka 94, tena akiwa Ikulu, Mwinyi alisema hana siku nyingi za kuiacha dunia, na hataki aende huko anapokwenda na aibu nyuma yake, na akasisitiza sana kwamba maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa duniani.

Ukiyasikiliza ni maneno rahisi kuyatamka, lakini wapo wanasiasa wameshindwa kuandaa maisha yao hapa duniani ili waache kumbukumbu inayoishi, na badala yake wamechagua kusifiwa na “chawa” wanaosifia hata kama hauko njia sahihi.

Sasa natamani hizi siku 12 tulizobakiza kuingia 2024 ambayo tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kila kiongozi wa kiserikali na kisiasa na Watanzania mmoja mmoja arudi kwa muumba wake, ili amuonyeshe njia sahihi ya kuacha ‘legacy’ (urathi).

Tunaweza kuchukulia kama ‘business as usual’ (mazoea) kwamba katika chaguzi zilizo mbele yetu tutafanya kama tuliyoyafanya mwaka 2019 na 2020, kwamba tunatunga hata sheria za uchaguzi kwa ujanja ujanja, ila tuelewe Watanzania wale sio hawa.

Duniani kote, shughuli ambayo huleta mgogoro mkubwa na pengine umwagaji wa damu ni uchaguzi pale unapopoteza sifa ya kuwa huru na haki, ndiyo maana natamani siku hizi 12 zilizosalia, tutafakari mahali itakapokuwa Tanzania mwaka 2024 na 2025.

Kuna nukuu maarufu ya Joseph Stalin ambaye anasema: “Those who vote decide nothing. Those who count the votes decide everything”, kwamba wanaopiga kura sio wanaofanya uamuzi bali wanaohesabu kura ndio huamua kila kitu.

Siamini kama hilo analolisema Stalin litatokea katika chaguzi zetu za mwaka 2024 na 2025 kwa sababu waswahili wanasema aliyeumwa na nyoka akiona ujani anashtuka.

Katrine Nenge (2019) katika andiko lake anasema moja ya sifa za uchaguzi huru na wa haki ni kuwa na mifumo bora ya kisheria, chombo huru na kinachokubalika, cha kusimamia uchaguzi, uhuru wa kufanya siasa na usawa kwa washiriki uchaguzi.

Sifa nyingine ni kuwa na usawa kwa wapiga kura, kuwa na hakikisho la uhuru wa kufanya siasa na wapiga kura wapewe taarifa sahihi kupita vyombo huru vya habari, ambazo zitawafanya wafanye uamuzi sahihi katika sanduku la kura.

Sifa nyingine ni kuwa na mazingira huru na salama yanayotolewa na polisi wenye weledi na wasio na maslahi na watawala, kampeni za haki, pasiwepo na vurugu za kisiasa na upande wa upinzani ukubali uchaguzi ulikuwa wa huru na haki.

Sasa katika mazingira ambayo tumepitia katika chaguzi nilizozisema na kama watawala wataziba masikio na tukaingia katika uchaguzi mkuu 2025 katika mazingira yale yale ya mwaka 2019 na 2020, tunaweza kuitumbukiza nchi kwenye shida.

Ieleweke kwamba hakuna mwenye hati miliki ya Tanzania, hivyo vyama vishindane kwa sera na hoja na mshindi apatikane kihalali kwa sababu tukubali au tukatae, chaguzi nilizozisema zimewaacha Watanzania na majeraha yanayovuja damu.

Uchaguzi ni wakati muhimu kwa raia na wanasiasa, kwa hiyo unapokuwa huru na haki na unaoaminika, unatoa taswira chanya kwamba Serikali iliyochaguliwa, iko kihalali na ina uhalali wa kisiasa na wala viongozi hawaongozi kwa mtutu wa bunduki.

Kwa hiyo, hizi siku 12, natamani kila mwenye dhamana ya kuhakikisha chaguzi zilizo mbele yetu zinakuwa huru na haki, basi ahakikishe anatuachia sheria nzuri kabla ya chaguzi hizo, ili hata akiondoka basi kumbukumbu yake iendelee kuishi.

Tunapotunga sheria za uchaguzi, hebu tusifanye hivyo huku tumeficha mapanga, au kuviziana viziana au kuweka vipengele vya sheria vya kuhakikisha zinalinda maslahi ya chama tawala, tubadili sheria tukiitizama mama Tanzania.