Simba, MO Dewji hakuna anayemlinda mwenzake

Penzi lililo imara ni lile ambalo kila mmoja anawajibika kwa mwenzake na kumlinda iwe katika nyakati za shida na raha.

Walio katika penzi imara wanacheka na kufurahi pamoja wakati wanapopitia nyakati za furaha na katika nyakati za huzuni wanalia na kusikitika pamoja pasipo mmoja kumuacha mwenzake.

Kama ambavyo ni suala la kawaida kwa penzi la kweli kutojificha basi kinyume chake ni sahihi kwamba penzi lisilo la kweli halijifichi.

Kulindana ndio msingi sahihi wa penzi lililo la kweli na hiyo inanikumbusha zaidi ya miaka 20 iliyopita kuliibuka kampeni moja iendayo kwa jina la ‘Kama Kweli Unampenda Utamlinda’.

Ukitazama kwa jicho la tatu kinachoendelea ndani ya Simba unaweza kuhisi penzi baina ya klabu hiyo na mwekezaji wake wa asilimia 49 za hisa (ikiwa mchakato wa uwekezaji utakamilika), mfanyabiashara Mohammed Dewji haliko sawa na kuna namna linayumba.

Kwa nini nimepata nguvu ya kusema hivyo? Ni kwa sababu kila upande hautoi ulinzi kwa mwenzake. Mohammed Dewji kwa sasa haipi ulinzi Simba na Simba haimpi ulinzi Mohammed Dewji.

Tuanzie kwa Simba kwa nini nafikiri haimpi ulinzi Mohammed Dewji?

Tangu 2018 hadi sasa, Simba haijakamilisha mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wake. Mchakato umechelewa kwa sababu kuna baadhi ya masuala hayajakamilishwa na mengine kuwekwa sawa kwa upande wa klabu na mwekezaji.

Lakini katika sehemu kubwa ya muda huo wote, Mohammed Dewji amekuwa akitoa kiasi kikubwa cha fedha kusaidia uendeshaji wa klabu hasa katika usajili, malipo ya stahiki za watumishi na shughuli nyingine muhimu za klabu.

Hili hata viongozi wa Simba wamekuwa wakikiri hadharani kwa nyakati tofauti hivyo kama wao wanakiri hilo, sisi ni nani tulipinge?

Fedha hizo za Dewji tunaweza kuzielezea kama za hisani tu kwa vile bado mchakato haujakamilika na ndio maana inakuwa ngumu kumuwajibisha na klabu inaishia kumuomba tu kwa sasa.

Kama mchakato ungekuwa umekamilika na yeye akatambulika kisheria kama mwekezaji wa asilimia 49 za hisa za Simba, klabu ingekuwa na mamlaka (authority) ya kumbana pindi asipotoa kwani ikiwa klabu itaingiza faida baadaye, Dewji atakuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa kwa vile ndiye mmiliki wa kiasi kikubwa cha hisa, baada ya klabu inayomiliki asilimia 49.

Na kwa vile anatoa fedha hizo kwa hisani, Simba pengine ingeweza kumtengenezea mazingira mazuri ya yeye kushawishika kutoa fedha pale klabu inapokwama kwa kumpa fursa ambayo ingemfanya naye aonje fedha itokanayo na mpira.

Tumeona matangazo ya bidhaa zake katika jezi za Simba ambayo kwanza anayalipia lakini bado hayamrudishii Dewji angalau nusu ya kile ambacho amekuwa akikitoa ndani ya klabu hiyo.

Katika hali ya kawaida, Dewji atashawishika vipi kuendelea kutoa fedha klabuni huku akiwa harudishi chochote cha kueleweka? Kati yetu sisi yupo ambaye anaweza kuwa tayari kuingiza fedha nyingi katika sehemu ambayo haimrudishii huku kukiwa hakuna mfumo rasmi wa kumlinda?

Mfano mdogo tunaweza kuutumia wa watani wao wa jadi Yanga ambao katika kipindi hiki ambacho bado hawajakamilisha mfumo wao mpya wa uendeshaji, wamekuwa wakipokea ufadhili mkubwa kutoka kwa mfanyabiashara Ghalib Said Mohammed kupitia kampuni yake ya GSM.

Mbali na ufadhili, Yanga imeingia mkataba wa udhamini na kampuni ya mfanyabiashara huyo na kumpa haki za kutengeneza na kusambaza jezi na bidhaa zingine zenye nembo ya klabu yao ambapo kuna kiasi kimekuwa kikienda klabuni na kingine kwa GSM kila jezi moja inapouzwa.

Hapo GSM ananufaika moja kwa moja na klabu anayoifadhili kwa vile jezi ni bidhaa ambayo shabiki atahitaji kuinunua na kuitumia ili ajitambulishe kama sehemu ya klabu.

Ni tofauti kwa MO Dewji kwani matangazo yake ya sabuni na bidhaa nyingine za kampuni yake kuwa kwenye jezi ya Simba, yanaweza yasimrudishie kitu kwani shabiki anaweza kuwa na bidhaa nyingi mbadala anazoweza kununua na kutumia tofauti na jezi ambazo hana chaguo mbadala zaidi ya kununua zile za klabu yake.

Ni rahisi GSM kutoa fedha za kuisaidia Yanga kwa sasa hata kama bado haijakamilisha mchakato wa mabadiliko kwa vile kama isipokuwa imara, anafahamu fika kuwa biashara ya jezi itayumba na yeye hatoingiza chochote.

Hiyo ni tofauti na Dewji ambaye analazimika kutoa fedha nyingi lakini hana uhakika wa kurudisha angalau nusu yake.

Fikiria kama Dewji ndio angekuwa anasimamia uzalishaji na uuzaji wa jezi na bidhaa za Simba angekubali kuona timu inafanya vibaya? Asingekubali na pengine angeweka kikubwa zaidi ya kile anachoweka sasa pasipo kujali mchakato umekamilika au la ili tu timu ifanye vizuri watu washawishike kununua.

Lakini kuna hili la namna ambavyo Simba imekuwa ikifanya usajili wake, haionekani kama inamlinda mtu anayeichangia kiasi kikubwa cha fedha.

Fedha nyingi zinatumika kusajili na kuvunja mikataba ya wachezaji wengi magarasa, je kuna mtu atakuwa tayari kuendelea kutoa fedha zake kila mara huku wachezaji wanaoletwa wengi wanashindwa kuifanya timu hiyo kuwa tishio uwanjani?

Ukigeukia upande wa pili, Dewji naye anashindwa kuilinda Simba kwa namna tofauti jambo ambalo linatia shaka juu ya hatima yake ya baadaye ndani ya klabu hiyo.

Mosi ni namna ambavyo amekuwa akitumia njia zisizo rasmi kufikisha madukuduku yake huku katiba ya klabu hiyo ikifafanua wazi kipi cha kufanya na kipi cha kutofanya.

Mara kadhaa ameshuhudiwa akitumia mitandao ya kijamii kutuhumu kuwa amekuwa anakwamishwa na baadhi ya watu ndani ya Simba katika suala lake la kuwekeza ndani ya klabu hiyo.


Hayo anayafanya huku akifahamu fika kuwa njia sahihi ya kufanya hivyo ni mkutano mkuu wa klabu hiyo au vikao vya bodi ya wakurugenzi kwa mujibu wa katiba ya Simba.


Lakini pia Dewji amekuwa na hulka ya kuitoa timu kwenye reli nyakati kadhaa inapokuwa inakabiliwa na mechi au matukio muhimu na makubwa jambo ambalo kwa namna moja linapunguza morali na hamasa ya kuhakikisha jambo husika linafanikiwa.

Mfano, wakati Simba inajiandaa na mchezo muhimu wa kuwania kufuzu hatua ya robo fainali ya


Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Jwaneng Galaxy, Dewji aliachia mahojiano yake mtandaoni yaliyomuonyesha akisema kuwa ameinunua klabu hiyo.

Inawezekana alikuwa na nia nzuri lakini nyakati ambazo aliachia mahojiano hayo haikuwa sahihi kwa vile ingeweza kuvuruga utulivu wa timu kuelekea mechi ngumu ambayo ilikuwa mbele yake.


Wahenga wanasema kinga ni bora kuliko tiba.

Simba na Dewji wanapaswa kuanza kulindana kuanzia sasa kama kweli kila upande unamhitaji mwingine.

Hiyo ndio kinga nzuri badala ya kungojea mambo yameharibika, watakuwa wamechelewa.


Charles Abel ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kupitia [email protected]