TAHARIRI: Mkakati huu wa kudai mikopo HESLB umechelewa
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imeanzisha ushirikiano na taasisi nyingine kwa lengo la kuboresha mfumo wa urejeshaji wa mikopo ya elimu na kupunguza changamoto zilizokwamisha malipo hayo.
Taasisi zilizoshirikishwa ni pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), na Taasisi ya Kuchakata Taarifa za Wakopaji ya Benki (Credit Info).
Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha wanufaika wote wanatimiza majukumu yao ya kurejesha mikopo kwa wakati ili mikopo hiyo iwanufaishe wengine.
Hatua hii inaonyesha kuwa bodi inatekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo Desemba 2024, mifumo yote ndani ya Serikali iwe inasomana.
Mifumo inayosomana inaruhusu tafiti na uchambuzi wa data kwa kutumia taarifa zilizokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali. Katika usimamizi wa mikopo, uchambuzi huo unasaidia kubaini maeneo yenye changamoto na kupanga mikakati ya marekebisho.
Hata hivyo, licha ya umuhimu wa hatua hii katika kuimarisha hali ya kifedha ya HESLB na kuongeza uwazi katika usimamizi wa mikopo ya elimu, imeanza kwa kuchelewa.
Hii ni kwa sababu wanufaika wengi hawajarejesha mikopo yao, na miongoni mwao wapo wenye shughuli zinazowaingizia kipato. Kukosekana kwa mifumo bora ya kufuatilia na kusimamia urejeshaji wa mikopo kumesababisha ucheleweshaji mkubwa wa kudai madeni kutoka kwa wadaiwa sugu, hali ambayo imeongeza mzigo wa kiutendaji kwa bodi.
Katika ushirikiano huu, ni muhimu kwa wadau wote kufanya kazi kwa karibu ili kuhakikisha mfumo unakuwa bora na wenye ufanisi zaidi kwa faida ya wanafunzi na Taifa kwa ujumla.
Mbali na mfumo huo, Nambari ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) isisahaulike, kwani inaweza kusaidia kupata taarifa za wafanyabiashara na waajiriwa katika sekta mbalimbali ambazo HESLB haijafikia.
Pia, TIN itasaidia kufuatilia taarifa za kifedha za mlipakodi na kuchunguza uwezo wake wa kifedha, jambo linalosaidia kuamua uwezo na muda wa kurejesha mkopo husika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia, jumla ya Sh600 bilioni bado ziko mikononi mwa wadaiwa, ikiwa ni madeni yaliyoiva. Kama fedha hizo zingerejeshwa, zingesaidia wanafunzi wengine kupata mikopo ya elimu ya juu na kuendelea na masomo yao.
Mikopo hii inawapa vijana nafasi ya kujiunga na taasisi za elimu ya juu, hasa wale ambao hawana uwezo wa kifedha wa kugharimia masomo yao. Kwa njia hii, inawawezesha kupata elimu na kuongeza ujuzi na maarifa yao, jambo linalochangia maendeleo yao binafsi na kitaaluma.
Hata hivyo, baadhi ya wanufaika ambao wapo kazini hawajarejesha mikopo hiyo, hivyo kuisababishia Serikali mzigo na kuwanyima fursa vijana wengine kuendelea na masomo.
Mikopo ya elimu ya juu husaidia kupunguza pengo kati ya walionacho na wasionacho katika jamii kwa kutoa fursa sawa kwa watu wenye vigezo kupata elimu. Hii inahakikisha kila mtu, bila kujali hali yake ya kifedha, anapata nafasi ya kuboresha maisha yake kupitia elimu.
Katika mazingira ya kiuchumi ya sasa, tatizo la wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawana ajira linaonekana kuwa changamoto kubwa kwa bodi na kwa Taifa kwa ujumla.
Hakta hivyo, tunatambua kuwa ukosekana kwa ajira kunaathiri uwezo wa wanufaika kurejesha mikopo yao, hivyo kusababisha ongezeko la deni la mikopo isiyorejeshwa.