Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KIUME: Mwambie binti yako, ‘kutokuolewa siyo dhambi’

Dada zetu wamekuwa wateja wa ‘wachungaji wa mchongo wa kisasa’. Mama zetu wamekuwa mateja wa ‘masheik wa mchongo’ wa kisasa.

Wanapishana kwenye vilinge vya waganga wa kienyeji wakiwa wamebeba kuku weupe na weusi utadhani wanafanya biashara ya kutotolesha mayai.

Huyu anaingia, huyu anatoka, wote wanatafuta dawa ya shida moja tu… NDOA. Kama siyo kutafuta mtu wa kumuoa, basi ni kuhakikisha mtu ambaye ameshamuoa anatuliza mapepe na kutulia ndani ya nyumba.

Hizi siyo hadithi mpya, mimi na wewe tunaziona na kuzisikia sana mtaani kwetu. Kama siyo kutokea kwenye familia yako basi ya rafiki yako. Ninachojaribu kusema tunazijua hizi hadithi.

Kwa sababu hiyo, nakuhimiza mwanamume mwenzangu, ukipata muda kaa na binti yako na umwambie kuwa kutokuolewa siyo dhambi.

Kwa sababu huku mtaani wenzie wamechanganyikiwa kwa kuwa wamefikia umri wanaodhani ndio wa kuolewa, lakini bado hawajazipata hizo ndoa.

Wanahisi wana gundu na bahati mbaya, wanahisi sio wazuri wa kutosha au labda hawana tabia nzuri au kuna kitu wanakosea.

Kaa mwambie binti yako kuwa, akifikia umri huo na hajaolewa siyo kwamba ana gundu au bahati mbaya.

Kuolewa hakuna uhusiano wowote na bahati nzuri kwa sababu ndoa siyo kitu kizuri wala siyo kitu kibaya, hakibebi hali yoyote kati ya hizo mpaka itakavyoamuliwa na mhusika.

Ukiamua kuona ni nzuri basi ni nzuri, ukiamua kuona kinyume, huwa hivyo pia.

Asidhani yeye siyo mzuri, mwambie ni mrembo sana, lakini ndoa haziji kutokana na uzuri wako, zinakuja kutokana na makubaliano ya wawili walioamua kuoana, ndiyo maana kuna wanawake wazuri walioolewa na kama wapo wabaya, basi nina uhakika wapo walioolewa pia.

Labda hana tabia nzuri, ila mueleze kuwa ndoa siyo mshahara wa tabia njema. Na mwambie kwamba hatakiwi kuwa na tabia nzuri kwa sababu ya kuolewa, anatakiwa awe hivyo kwa sababu yeye ni binadamu.

Mpe mfano kwamba uasherati siyo tabia mbaya kwa sababu hakuna mwanamume anayetaka kuoa mwanamke muasherati, bali ni tabia mbaya kwa sababu uasherati ni uchafu, unakuja na maradhi na kadhia nyingine lukuki.

Msisitizie kwamba jeuri, kiburi, mvivu na vitabia vyote vichafu, siyo vichafu kwa sababu wanaume watamuogopa, ni vichafu kwa sababu ataogopwa na kila binadamu, hakuna bosi anayetaka mfanyakazi kiburi, hakuna shangazi anayependa mpwa jeuri, kama ambavyo hukuna mwanamume anayependa kuoa mwanamke wa hivyo, mueleweshe awe mtu mwema siyo kwa sababu ya ndoa, bali kwa sababu dunia inahitaji watu wema.

Hakikisha husahau kumdadavulia kuwa kutokuolewa ni dhambi kwa wanawake wasiojielewa kwa nini wapo duniani.

Ajue kuwa siku zote wanawake wasiokuwa na ndoto zozote, ndoto yao huwa kuolewa.

Mwanamke ambaye hana mpango wa kuja kuwa mmiliki wa gazeti kubwa la fasheni Afrika Mashariki, ndoto yake huwa ni kuoelwa.

Mwanamke ambaye hana ndoto kubwa ya kuwa spika wa bunge au mwanasiasa mkubwa msaidia watu, ndoto yake kubwa huwa kuolewa.

Mwanamke ambaye hajui yupo duniani kwa ajili ya nini, huishi kwa ajili ya kuolewa, kubebeshwa mimba, kuzaa, kulea watoto na kuzeeshwa, kufariki na kuzikwa.

Sijakwambia umwambie ndoa ni kitu kibaya au asiolewe, hapana. Mwambie ndoa inaweza kuwa kitu kizuri lakini kamwe asikae chini kuisubiri. Aendelee na maisha yake, aendelee kufukuzia ndoto zake, ndoa itakuja itamkuta huko huko mbele ya safari.