Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tusake suluhisho la rushwa kwa trafiki

Gazeti hili limechunguza na kuandika kwa kina namna rushwa ilivyoota mizizi barabarani, ikiwahusisha madereva kama watoaji na askari wa usalama barabarani wakiwa wapokeaji.

Kwa ujumla, tatizo la rushwa katika sekta ya usalama barabarani limeonekana kama halali na la kawaida, ili mhusika asiandikiwe faini iliyowekwa kisheria.
Licha ya vitendo hivi kwenda kinyume na sheria na mwenendo mwema wa askari wa polisi, bado vimezoeleka katika jamii, vikionekana kama matendo ya kawaida.
Ni katika mazingira hayo, kiongozi mkubwa aliwahi kutamka hadharani kwamba “hizo ni pesa za kubrash viatu”, hali ambayo tunaamini ilichochea zaidi vitendo hivyo.
Mathalani, madereva na makondakta wa mabasi, daladala, malori na magari madogo ya mizigo hutenga kati ya Sh2,000 na Sh5,000 ili kuwapa askari kila wanaposimamishwa ili kukwepa faini ya Sh30,000.
Ni kutokana na hilo, trafiki huonekana kama wanaogelea katika ukwasi wa fedha na mali na hivyo kufanya askari wa vitengo vingine kutamani na kuweka ushawishi kupangiwa huko majukumu.
Licha ya namna matendo yenyewe yanavyofanyika, hakuna hatua zinazoonekana kuchukuliwa.
Kwa mfano, Januari 2022 ilidaiwa askari mmoja amekamatwa na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) akipokea rushwa mkoani Iringa, lakini hadi sasa hakuna kesi wala hatua nyingine kuchukuliwa zilizotangazwa dhidi yake.
Si hilo tu, pamoja na matukio yenyewe kufanyika abiria na wapita njia wanaona, si maofisa wa Takukuru wala wasimamizi wa jeshi hilo wanaoona au kukerwa na kadhia hiyo.
Kwa namna suala hilo lilivyo, ni rahisi kukubaliana na madai kwamba katika hilo mhusika si mtu mmoja mmoja, bali tatizo la kimfumo na wanaohusika na mgawo ni wengi.
Ni kutokana uzito huo, ni lazima Serikali ichukue hatua madhubuti na endelevu kudhibiti hali hiyo, ikiwemo kuharakisha matumizi yaliyowahi kutangazwa, ya jaketi zenye kamera au kamera hizo kufungwa maeneo yote muhimu.
Mei mwaka huu, tulifarijika tulipomsikia Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango akilitaka Jeshi la Polisi kukamilisha mchakato wa matumizi ya kamera zitakazovaliwa na askari polisi, wakiwamo askari wa usalama barabarani.
Dk Mpango alisema hayo akizindua kituo cha Polisi Daraja A, Mtumba jijini Dodoma, kuwa waziri wa Mambo ya Ndani amemhakikishia kuwa mchakato huo umeanza. Kwamba lengo ni kuwa askari polisi watakapokuwa wakiongea na madereva au makondakta huko barabarani wataonekana na kusikika wanachokifanya na hivyo kupunguza rushwa katika sekta hiyo.
Japokuwa mpango huo ni mzuri, ipo haja ya kamera hizo kuwa na mifumo inayosomana na taasisi nyingine, ili isiwe rahisi kwa askari hao kufuta kumbukumbu, kama tulivyosikia katika kamera za kupima mwendo kasi hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, ni muhimu kwa wamiliki wa magari ya daladala, mabasi, malori na hata ya binafsi kuhakikisha si mabovu, ili trafiki akose makosa ya kuwaandikia ili wapate nguvu za kukataa rushwa.
Vilevile, vyombo vyenye dhamana ya kupambana na rushwa kama Takukuru na vinginevyo, vifungue makucha yake na kuhakikisha wanaotoa na kupokea rushwa wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na hilo, viongozi wa Jeshi la Polisi, wizara husika na Takukuru wachukue nafasi zao katika kusimamia maadili, hasa kuzuia rushwa inayotamalaki mbele ya macho yao na macho ya umma.