Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuwaige Japan kuelekea Afcon 2027

Tanzania tutakuwa miongoni mwa nchi tatu ambazo zitaandaa kwa pamoja fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, nyingine zikiwa ni Kenya na Uganda.

Haya ni mashindano makubwa zaidi katika mpira wa miguu barani Afrika kwani yanashirikisha timu bora zaidi za soka za taifa barani Afrika huku nyingi zikiwa na vikosi vinavyoundwa na kundi kubwa la wanasoka bora wanaocheza soka la kulipwa katika ligi mbalimbali maarufu duniani hasa barani Ulaya.

Kwa maana hiyo ni ndoto kwa kila taifa hapa Afrika kushiriki ama kuandaa fainali za Afcon, fursa ambayo sisi Tanzania na wenzetu tumeipata kwa mwaka huo wa 2027.

Tunaona juhudi za Serikali ya Tanzania katika ujenzi wa viwanja vipya na pia ukarabati wa vilivyopo pamoja na vile vya mazoezi sambamba na miundombinu mingine ili hadi ifikapo 2027 tuwe na utayari wa kuandaa fainali hizo.

Uwanja wa Benjamin Mkapa unaendelea kukarabatiwa na muda mfupi ujao Uwanja wa New Amaan Complex nao utaaanza kuboreshwa lakini kuna ujenzi wa Uwanja wa Samia kule Arusha huku pia serikali ikipanga kujenga uwanja mkoani Dodoma.

Wiki mbili zilizopita kulisainiwa mikataba ya uboreshaji wa viwanja 20 ambavyo vitatumika kwa ajili ya mazoezi ya timu zitakazoshiriki mashindano hayo.

Kwa upande mwingine Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na mikakati ya kupata timu bora ya taifa ambayo italeta ushindani dhidi ya timu nyingine shiriki.

Wakati tukiwa katika maandalizi, tunapaswa kukumbuka kwamba kuna maisha kabla, wakati na baada ya kumalizika kwa fainali hizo za Afcon.

Maisha ya kabla ndio kama haya ya wakati huu ambayo ni mchakato wa maandalizi na yale ya wakati ni ushiriki wa timu na masuala mengine ya kiugavi lakini maisha ya baada ni kipindi ambacho kama nchi tutakipata kuanzia pale fainali hizo zitakapofikia tamati.

Kuna faida za kiuchumi lakini hapa nazifikiria zaidi faida za kisoka nikitamani kuona fainali hizo za Afcon 2027 zikituachia alama endelevu nayo ni kuwa na muendelezo wa timu yetu ya taifa kushiriki mashindano hayo na mengine makubwa kisoka.

Hatupaswi baada ya kumalizika kwa Afcon turudi katika maisha ya kusindikiza wenzetu na kutazama mechi za mashindano kama hayo au yale ya Kombe la Dunia katika luninga kwani hakutakuwa na maana ya sisi kuandaa fainali hizo za 2027.

Tutazame mfano wa Japan ambayo mwaka 2002 ilishirikiana na majirani zao Korea Kusini kuandaa fainali za Kombe la Dunia ambazo Brazil ilitwaa ubingwa.

Miaka mingi nyuma kabla ya hapo, Japan haikuwa inafanya vizuri katika mashindano ya kuwania kufuzu fainali hizo za mashindano hayo makubwa ya soka duniani.

Muda mfupi baada ya kushinda tenda ya kuandaa fainali hizo za Kombe la Dunia, waliweka mikakati ya muda mfupi na ile ya muda mrefu ambayo itawafanya wawe na ushiriki mzuri katika mashindano watakayoandaa nyumbani na yale ya miaka mingi itakayofuata.

Tenda ya kuandaa fainali hizo za mwaka 2002, walishinda mwaka 1996 hivyo kwanza wakaweka lengo la kuhakikisha wanafuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998 zilizofanyika Ufaransa ambazo waliamini zitawapa uzoefu wa kutosha kwanza wa kuandaa na pia kushiriki mashindano hayo makubwa kwa vile walikuwa hawajawahi kushiriki tangi yalipoanzishwa mwaka 1930.

Walifanikiwa kushiriki katika fainali za mwaka 1998 na wakaishia hatua ya makundi lakini baada ya hapo kumalizika kwa fainali za 2002 wakafuzu kwa mara tano mfululizo na sasa wako katika nafasi nzuri ya kufuzu fainali za 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico kwa vile wanaongoza kundi lao katika mashindano ya kuwania kufuzu kupitia kanda ya Asia.

Fainali za mwaka 1998 ambazo walishiriki kwa mara ya kwanza, ziliwapa darasa kuwa wanahitajika kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya Japan hasa barani Ulaya kwa vile waliingia katika fainali hizo wakiwa na kikosi chenye wachezaji wa ndani ya Japan tu.

Waliposhiriki fainali za mwaka 2002, kikosi chao kilikuwa na nyota wanne wanaocheza soka la kulipwa na baada ya hapo wamekuwa na namba kubwa ya wachezaji wanaocheza katika ligi mbalimbali Ulaya ambao leo wamekuwa chachu ya mafanikio ya taifa hilo.

Miongoni mwa hatua ambazo Japan walichukua katika kufanikisha hilo ni kufungua shule na vituo vya kisasa vya soka ambavyo viliandaa na vinaendelea kuandaa vijana wenye umri mdogo kwa kuwapa misingi na mbinu bora za kuwafanya wawe wanasoka mahiri.

Mfano wa vituo hivyo ni kituo cha soka cha kimataifa cha Japan ambacho kilianzishwa mwaka 2002.

Bado hatujachelewa na nafasi ya kukaa chini kuchora mkakati wa namna gani tunaweza kuitumia fursa ya kuandaa fainali za Afcon kujenga kesho endelevu ya soka letu na mafanikio ya timu yetu ya taifa ipo.

Kwa kuwa serikali inaonyesha utayari wa kuhakikisha fainali hizo zinaandaliwa kikamilifu, ni wajibu wetu wadau wa soka kuiunga mkono kwa kuandaa mikakati ambayo itawezesha kile tunachokitamani kitimie kama ambavyo wenzetu Japan walithubutu na kisha baadaye wakafanikiwa.

Kuiga mazuri kwa waliofanikiwa sio dhambi hasa kama hicho kinachoigwa kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa umma katika miaka mingi itakayofuata hapo baadaye.