UCHAMBUZI: Shule zetu zinavyoshindwa kuzalisha kina Mkapa wengi

Tuesday March 31 2020

Kumbe Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliposema elimu yetu ina walakini na kushauri kuwapo kwa mjadala wa kitaifa ili kuinusuru, hakukurupuka na wala hakusema hivyo ili naye aonekane amekosoa viongozi.

Kuna baadhi ya watu wana mtazamo wa ajabu, wanataka viongozi wakistaafu watulie; wasiwakosoe waliowaachia kijiti hata kama wanavurunda.

Mkapa maarufu wakati wa utawala wake kwa kaulimbiu ya ‘Ukweli na Uwazi’ siku zote amekuwa akisema kile anachokiamini tena kwa ushahidi.

Ni ushahidi unaotokana na mengi aliyoyapitia katika safari yake ya masomo kuanzia Ndanda, St Francis (sasa Pugu) na baadaye Chuo Kikuu cha Makerere cha nchini Uganda.

Unapotazama wahitimu wengi wa leo katika ngazi mbalimbali za elimu, utakubaliana na anachokisema Mkapa.

Si tu wahitimu wetu wanaishi mbali na soko la ajira kwa kukosa ujuzi na umahiri wa kazi, pia hawana stadi za kujiamini, uwezo mdogo wa kujieleza sio tu kwa lugha za kigeni hata Kiswahili ambacho kwa walio wengi ni lugha yao ya kwanza.

Advertisement

Nimesema Mkapa anazungumza kwa ushahidi. Alichokiona kikifanyika enzi zake sicho kilichopo sasa katika mfumo wetu wa elimu hasa upande wa mbinu za ufundishaji zenye tija.

Kilichopo ni kuwa ama mbinu hizo hazipo au walimu kwa sababu ya kuwa nao ni zao la mfumo mbovu wa elimu, wanashindwa kuzifanyia kazi.

Nimemsoma Mkapa katika wasifu wake uitwao: My Life, My Purpose. Ana mengi anayoyakumbuka kuhusu mbinu za ufundishaji walizotumia walimu wake katika shule alikopitia; hatimaye kumfanya si tu mlumbi wa lugha ya Kiingereza na Kiswahili, lakini kuwa na uwezo wa kujiamini na jasiri akiwa mtumishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), serikalini na baadaye kwenye siasa.

Mkapa kwa mfano, anaeleza namna mashindano ya midahalo, michezo ya kuigiza, uandishi wa insha, ufasaha wa lugha ilivyokuwa sehemu ya maisha ya shule hasa alipokuwa shuleni Pugu.

‘’Ujuzi nilioupata kutokana na midahalo na kwenye michezo ya kuigiza, ulikuja kuwa na manufaa makubwa katika maisha yangu ya kazi hasa mbele ya jamii na bungeni,” anaandika Mkapa katika ukurasa wa 23.

Kuhusu midahalo, anasema: “Tulikuwa na midahalo mingi shuleni iliyotusaidia kuwa na uwezo wa kuhoji na kuwa na uzingativu wa mambo.’’

Hata nje ya shule anakumbuka namna walivyokuwa wakizigaragaza shule za watoto wa jamii ya Kiasia katika mashindano ya uzungumzaji na ufasaha wa lugha.

Leo shule zimeshindwa kutoa wahitimu wanaojiamini maishani na wasioweza hata kujieleza kwa lugha mbalimbali ikiwamo lugha mama ya Kiswahili.

Shule zinawaandaa kufaulu mitihani tena kwa kukariri maswali ya mitihani iliyopita.

Mkazo si kuwa na ujuzi wa kuzikabili changamoto za dunia, bali kuwa na ufaulu wa alama A.

Kinachovutia ni kuwa Mkapa anasema mfumo huu wa kuwajenga wanafunzi kupitia midahalo, michezo ya kuigiza na uandishi wa kibunifu aliukuta pia Chuo Kikuu cha Makerere, na huko hakujiweka nyuma alikuwa mshiriki. Sidhani kama haya yanafanyika katika vyuo vikuu vyetu.

Tunapowalalamikia wahitimu wetu kushindwa kujieleza wanapofanyiwa usaili wa kazi, tujiulize kama huko shuleni na vyuoni walijengewa misingi ya kujiamini kupitia mbinu kama midahalo, maigizo na mengineyo.

Jingine kubwa linalomtofautisha Mkapa na wengi ni mapenzi yake kwa vitabu. Mbali ya kuwa na maktaba nzima nyumbani kwake, anasema anaposafiri hakosi kutembelea maduka ya vitabu.

Utamaduni wa kusoma vitabu haukuja hivihivi kwake; bila shaka ni misingi aliyokuzwa nayo tangu akiwa mwanafunzi mdogo.

Leo si shuleni si nyumbani utamaduni huu umetoweka. Shule hasa za msingi hazina maktaba, nyumbani maktaba pekee ni mkusanyiko wa kanda za filamu ambazo leo zimekuwa sehemu ya maisha yetu na si vitabu

Tunapomsifu Mkapa kwa kuwa jasiri, anayejiamini na mlumbi (mzungumzaji mahiri wa lugha) ni kwa sababu aliandaliwa shuleni. Je, shule zetu zinawaandaa kina Mkapa?

Abeid Poyo ni mwandishi wa Mwananchi. 0754990083

Advertisement