Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Kwa nini watia nia ubunge CCM wanatakiwa kujiandaa kisaikolojia?
Huku mitaani ni kama kuna msiba fulani kutokana na tetesi za baadhi ya watia nia nafasi ya ubunge kutopendekezwa lakini pia kuna wenye furaha yenye mashaka, licha ya kupendekezwa kuwa miongoni mwa majina matatu ya watia nia.
Napenda niwatahadharishe mapema watia nia wa ubunge CCM kuwa wajiandae kisaikolojia iwe ana uhakika kupitia vyanzo vyake kuwa yuko miongoni mwa majina matatu au amechinjiwa baharini, kuwa kichinjio cha kweli kipo Dodoma.
Hii ni baada ya vikao vya kamati ya siasa ya wilaya kukamilisha kazi ya uchujaji na kupendekeza majina matatu kwenda kamati ya siasa ya mkoa, ili nayo iwajadili watia nia wote na alama walizowekewa na kamati za siasa za wilaya.
Kisha nao watatoa mapendekezo yao kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Zanzibar, kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar.
Ni kama msiba kwa sababu wamepenyezewa za ndani kuwa hawakupewa alama A,B wala C bali wamewekewa alama kuanzia D lakini wale waliopo miongoni mwa majina yale matatu hawana furaha, kwa sababu hawana uhakika kama majina yatarudi.
Nataka niwatie moyo wale ambao wamepokea taarifa za kuwarusha roho kuwa hawapo kwenye yale majina matatu kwa sababu kukatika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi, kwani bado kuna vikao vya juu vinavyoweza kubadili kila kitu.
Kwa wale ambao wamepenyezewa za ndani kuwa majina yao ni miongoni mwa watatu ambao majina yao yamepelekwa kamati kuu, nao wanapaswa kujiandaa kisaikolojia, kwa sababu lolote linaweza kutokea.
Yaani kwa maneno mengine ni kuwa hakuna mwenye uhakika wa asilimia 100 kuwa jina lake litarudi licha ya kupendekezwa na kamati ya siasa ya mkoa na hii inatokana na sababu mbalimbali ikiwamo taarifa zilizokusanywa juu yao.
Lakini ukiacha hilo, vikao vya juu vya maamuzi, kupitia kamati za maadili au vyombo vya usalama, zinaweza kuwa na taarifa kuwa maamuzi dhidi ya mgombea fulani yamefanywa kwa upendeleo, kujuana, rushwa, urafiki au kubebana.
Ndio maana nimetangulia kuwatahadharisha watia nia wa ubunge CCM wajiandae kisaikolojia iwe wana uhakika kupitia vyanzo vyake kuwa yuko miongoni mwa majina matatu au amechinjiwa baharini, kuwa kichinjio cha kweli kipo Dodoma.
Kwa sababu sifa za kuteuliwa kwa mujibu wa kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola, toleo la 2021 zipo sita hivyo unaweza kuwa nazo zote lakini ukakiuka maadili yale yaliyopo katika kanuni ile ya 25.
Sifa za wagombea kwa mujibu wa kanuni ya 5(i) hadi (vii) na inawahusu wote waliojadiliwa na vikao ni pamoja na awe mwanachama wa CCM asiyetiliwa shaka yoyote katika eneo lake, mwadilifu na anayekubalika kwa wananchi kwa ujumla.
Awe na sifa zote zinazotakiwa na Katiba ya nchi au sheria au kanuni inayohusu uongozi anaotaka kugombea, awe anakubali kwa dhati imani, malengo na sera za CCM na awe msitari wa mbele kuhudhuria vikao cha chama vinavyomhusu.
Kanuni hizo zinamtaka awe mkweli, mwaminifu kwa CCM na mwenye tabia na mwenendo safi kwa jamii na awe mpenda maendeleo, mbunifu, hodari wa kazi, mwenye elimu, uzoefu, upeo mkubwa maendeleo ya kiuchumi.
Hizo ndio sifa kuu ambazo zinamwezesha mtia nia kupenya katika vikao hivyo vya mchujo isipokuwa kama ulifanya mambo ambayo yanakatazwa na Kanuni ya 25(1) hadi (7) ajue atakuwa amejipotezea mwenyewe sifa ya kuteuliwa.
Miongoni mwa makatazo hayo ni pamoja na kufanya kampeni za kupakana matope dhidi ya mtia nia mwenzako, kufanya vitendo vinavyokiuka katiba ya CCM, kanuni, na sheria za nchi na kufanya kampeni kabla ya muda rasmi.
Kanuni ya sita inasema ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake, kutoa misaada mbalimbali wakati uchaguzi wa ndani unapokaribia, ambayo dhahiri ina lengo la kuvutia kura wakati wa kura za maoni.
Ingawa hatujafika hatua ya kujua majina matatu yatakayorudishwa, lakini huko mitaani yanayoendelea Mungu ndiye anajua, kwani wapo ambao ni kama wana uhakika 100 majina yatarudi, wanakutana kwa siri na wapiga kura za maoni.
Kama alivyosema Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, Januari mwaka huu na kurudia kauli yenye maudhui kama hayo Mei 30 kwamba CCM kina macho na kinaona na kufahamu rafu zinazoendelea huko majimboni.
Kupitia kikao cha Mei 30, 2025, Rais Samia alitoa rungu kwa vikao vya uchujaji kufanya kazi yake kwa uadilifu na bila kumuonea mtu, akisema anayefaa aambiwe anafaa na asiyefaa aambiwe waziwazi kwamba hafai na sababu zielezwe.
Ninafahamu kuna manung’uniko ama ya chini kwa chini ama ya waziwazi na mengine huenda yalishapelekwa kwa Katibu mkuu CCM kutoridhishwa na ama mchakato uliofanywa na kamati za siasa wilaya au kamati za siasa za mkoa.
Ndio maana nimetangulia kusema wale ambao wana uhakika kupitia wasiri wao kuwa wapo miongoni mwa majina matatu yaliyopendekezwa basi wanapaswa kujiandaa kisaikolojia, na wale ambao hawajapendekezwa waishi kwa matumaini.
Kwa nini wajiandae kisaikolojia, ni kwamba wajiandae ili pale jina lake halitarudishwa wakati alihakikishiwa lipo, basi akae kwa kutulia, lakini wale wanaotakiwa kuishi kwa matumaini ni kwa sababu wanaweza kurudi.
Kesho Julai 14, 2025, kikao cha kamati maalumu ya NEC Zanzibar kitakaa kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa kamati kuu juu ya wanachama wanaoomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na viti maalumu kwa upande wa Zanzibar.
Julai 17 na 18, 2025 kikao cha sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa kitakaa kupokea na kuchambua majina ya wagombea ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi wa Jimbo na viti maalum kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya uteuzi.
Lakini Julai 19,2025, kutakuwa na kikao cha kamati kuu ya NEC ya taifa kufikiria na kuteua majina ya wana CCM wasiozidi watatu, walioomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo na viti maalum ili wakapigiwe kura.
Hiki ndio kipindi cha watia nia kumuomba Mungu kila mmoja kwa imani yake ili atende miujiza maana kamati za siasa za mkoa sio vikao vya mwisho vya kuamua majina halisi matatu, kichinjio halisi kipo Dodoma.
Lakini kwa watia nia ambao waliguswa kwa namna moja ama nyingine na kauli za mwenyekiti, na wakachukua fomu basi wao ndio wanapaswa zaidi kumuomba Mungu wao atende miujiza na wajiandae kisaikolojia pia.
0656600900