Uhuru wa habari ni wajibu wa kila mdau

Leo ni Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambayo huadhimishwa Mei 3, kila mwaka. Katika siku hii, wadau wanapata nafasi ya kutafakari umuhimu wa tasnia ya habari katika kuchochea uhuru wa kutoa maoni na maendeleo ya jamii.

Uhuru wa vyombo vya habari ni jambo muhimu kwa kila mtu, hasa katika mazingira yetu ya sasa ambapo changamoto za kijamii, kiuchumi na kisiasa zinahitaji ufikiaji wa taarifa sahihi na za kuaminika.

Katika maadhimisho ya siku hii ya uhuru wa vyombo vya habari, ni muhimu kutafakari kwa pamoja jinsi uhuru huo unavyoweza kusaidia katika maendeleo ya nchi yetu.

Tuzidishe juhudi za kuunda mazingira bora ya kufanya kazi kwa vyombo vya habari na kuhakikisha kwamba uhuru huo unalindwa na kudumishwa kwa manufaa ya jamii nzima.

Tanzania kama moja ya mataifa yanayoadhimisha siku hii, imeendelea kushuhudia mabadiliko tofauti yanayofanywa na Serikali katika kuhakikisha kwamba vyombo vya habari vinafanya shughuli zao kwa uhuru.

Hata hivyo, bado kuna mapungufu ambayo yanahitaji kushughulikiwa ili kuhakikisha uhuru huu unakuwa na maana halisi.

Kwa mfano, vifungu vya sheria vinavyolazimisha mwekezaji mzawa kumiliki angalau asilimia 51 ya hisa katika sekta ya habari vinaweza kuzuia uwekezaji na kuathiri ufanisi wa vyombo vya habari.

Tunapaswa kuona uhuru wa vyombo vya habari kama jukumu la pamoja kati ya Serikali, wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na wananchi wote.

Serikali inahitaji kuendelea kusaidia mazingira ya kazi ya vyombo vya habari na kuzingatia haki za waandishi, vivyo hivyo, wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuwekeza kikamilifu ili kuboresha viwango vya kitaalamu na kuhakikisha uhuru wa waandishi unatamalaki.

Wananchi wenyewe wanapaswa kusaidia kwa kudai uwajibikaji na kutoa mrejesho kwa vyombo vya habari.

Tunatafakari haya yote tukikumbuka kwamba hali ya vyombo vya habari katika miaka ya karibuni iliwekwa majaribuni, uhuru ulitoweka kwa kiwango kikubwa na viwango vya uandishi wa habari vilibadilika na baadhi ya vyombo vikabadili uelekeo kutoka katika kukosoa kwenda kwenye kupongeza na kujipendekeza, hali ambayo ilipunguza kwa kiasi kikubwa imani ya watumiaji wake.

Katika kipindi hicho, Bunge lilipitisha sheria nyingi ambazo kwa namna moja au nyingine zilipoka uhuru wa vyombo vya habari na kujenga mazingira ya kuvidhibiti.

Ingawa kwa sasa kuna mwanga unaonekana, lakini sheria nyingi ziizotungwa hazijabadilika, hali ambayo haileti matumaini sana kwa kuwa ipo siku hali iliyokuwepo inaweza kurejea.

Pamoja na maboresho hayo ya kisheria, sisi tunaamini kwamba bado kuna mambo yanahitaji kufanyiwa kazi zaidi ili kuimarisha uhuru kwa vyombo vya habari. Bado kuna vifungu kwenye sheria hiyo vinavyopunguza uhuru kwa vyombo vya habari kutekeleza majukumu yake, na sasa tukiwa na nia njema, basi msisitizo wa uhuru unaotakiwa uwekwe kwenye Katiba ili yeyote ajaye asiuyumbishe.

Tunajua kuwa mabadiliko ya sheria ni suala moja, lakini utashi wa kuvisaidia vyombo vya habari na kuvijenga ili viwe huru kutekeleza wajibu wake kama mhimili wa nne wa dola ni jambo jingine. Kama hakuna utashi huo, basi hata sheria nzuri hazitafaa.