Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujenzi usiomalizika unaongeza maumivu

Unguja. Ni dhahiri kwamba Zanzibar inajengwa na kubadilika kwa kasi kubwa kimazingira na kimwonekano.

Mtu aliyekaa nje ya visiwa hivi kwa miaka minne anaweza kushangazwa na mabadiliko makubwa yaliyotokea. Maeneo mengi yamebadilika na hata taswira zake zimegeuka; majengo yaliyokuwa yamechakaa yanaendelea kutoweka na kupisha maendeleo mapya.

Mbali na majengo ya kisasa ya taasisi, biashara na masoko, kuna ujenzi mkubwa wa miundombinu ya barabara za mijini na vijijini unaoendelea karibu katika kila mkoa. Tangu kuingia madarakani Novemba 2020, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, aliahidi kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali. Kwa kiwango kinachoonekana sasa, azma hiyo inaelekea kufikiwa. Barabara nyingi zinazoingia, kutoka na kuzunguka mji wa Unguja zimefunguliwa upya kwa ajili ya ujenzi.

Hili ni jambo la kupongezwa kwani linaonesha dhamira ya kuifanya Zanzibar iendane na hadhi yake kama kitovu cha utalii. Aidha, barabara za mitaani zimeanza kujengwa kwa zege au kuwekwa lami, jambo lililoanza kushuhudiwa kwa miaka kadhaa sasa.

Hata hivyo, pamoja na maendeleo hayo, kuna changamoto zinazojitokeza. Baadhi zinatokana na mazingira, lakini nyingine zinatokana na uzembe wa mamlaka na wakandarasi wanaotekeleza miradi kwa mazoea.

Ikumbukwe kuwa katika maeneo mengi ya ujenzi kuna miundombinu mingine muhimu kama maji na umeme ambayo huathirika wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wa umeme, nguzo ni miundombinu inayoonekana wazi, hivyo huhitaji ushirikishwaji wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kabla ya kuhamishwa. Hata hivyo, mchakato huo umekuwa ukisababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara katika baadhi ya maeneo.

Changamoto kubwa zaidi ipo kwenye miundombinu ya maji iliyo chini ya ardhi. Mabomba hukatwa wakati wa ujenzi na kusababisha wananchi kukosa huduma muhimu ya maji. Mara nyingi miundombinu hiyo huchukua muda mrefu kurekebishwa na kurejeshwa katika hali ya kawaida.

Kero kubwa inayowakumba wananchi ni utaratibu wa ujenzi kutokamilika kwa wakati. Mara nyingi barabara hufumuliwa na kujengwa kwa sehemu, huku baadhi ya maeneo yakiwekewa lami au zege na mengine kuachwa na kifusi. Baada ya hapo makandarasi huhamia sehemu nyingine kabla ya kukamilisha kazi.

Matokeo yake ni barabara kujengwa vipandevipande bila mitaro wala njia za watembea kwa miguu. Baada ya miezi kadhaa mkandarasi hurudi kujenga sehemu ya mitaro, lakini mara nyingi hakamilishi kwa wakati. Hivyo, mradi mmoja unaweza kuchukua muda mrefu huku ukiendelea kuwasababishia wananchi usumbufu mkubwa.

Hali hii husababisha uharibifu wa mara kwa mara wa miundombinu ya maji pamoja na kero za vifusi, vumbi na maji kutuama wakati wa mvua. Tatizo hili si la wakandarasi pekee, bali pia la wasimamizi wa miradi wanaoruhusu utaratibu huo kuendelea.

Ni wakati sasa kwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha hali hiyo inakoma. Wananchi wanapaswa kupata huduma bora bila kulazimika kupoteza huduma nyingine muhimu wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mbali na usumbufu kwa wananchi, kujenga barabara bila kukamilisha mitaro kuna athari za moja kwa moja kwa serikali. Maji ya mvua hukosa njia ya kupita, hubaki juu ya lami na kusababisha mashimo. Hivyo, kabla hata ya barabara kukabidhiwa rasmi, baadhi ya sehemu huanza kuharibika.

Hali hiyo huongeza gharama kwa sababu serikali hulazimika kulipia matengenezo au ujenzi upya wa sehemu zilizoharibika. Fedha za walipa kodi hupotea wakati ambapo zingeelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo.

Aidha, uwepo wa vifusi mbele ya nyumba na maeneo ya biashara huathiri shughuli za wananchi. Maji yanapotuwama huongeza mazalia ya mbu na hatari ya magonjwa kama malaria. Wakati wa mvua barabara huwa na matope, na wakati wa jua huzalisha vumbi linaloweza kusababisha matatizo ya macho, ngozi na mfumo wa upumuaji.

Maji yasiyopata njia ya kupita huingia kwenye makazi ya watu na kusababisha mafuriko ndani ya nyumba. Biashara pia huathirika kutokana na ucheleweshaji wa usafiri na shughuli za kila siku.

Katika mazingira hayo, baadhi ya wananchi hupoteza imani na serikali na kuanza kuona miradi hiyo kama njia ya matumizi mabaya ya fedha za umma badala ya kuwa suluhisho la matatizo yao.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia hali hii ni mipango duni ya awali na jitihada za kupunguza gharama ili miradi ianze haraka. Mara nyingi mifumo ya mitaro husahaulika katika hatua za usanifu wa miradi.

Suluhisho la msingi ni kuweka utaratibu unaosisitiza kuwa hakuna barabara inayopaswa kujengwa bila mfumo kamili wa mitaro ya kupitisha maji.

Mradi usiokuwa na mfumo wa maji ya mvua usiruhusiwe kuanza kutekelezwa. Hatua hiyo itapunguza hasara, kuongeza ubora wa miradi na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.