Ulevi unavyochangia kuchepuka

Ushawishi wa kilevi, unaelezwa kuwa moja ya sababu zinazochangia wenza kuchepuka. Wako watu wanaojiamini sana na wanajihisi wenye uwezo wa kujizuia, lakini mara wanapokuwa katika ulevi hushindwa kujizuia.

Hili liko kwa wanawake na wanaume, tabia ya ulevi hupunguza uwezo wa mtu wa kufikiria ilivyo sahihi.

Unaweza kukuta watu wameketi pamoja na wanaheshimiana, lakini kwa kadiri wanavyoendelea kulewa wanaanza kushikana maungo na kila mmoja anaona ni sawa tu.

Heshima na nidhamu waliyokuwa nayo awali imeshapeperukia dirishani kwa sababu ya ushawishi wa ulevi.

 Hali hii ina majuto sana, maana mtu anajikuta ameshiriki ngono na mtu mwingine, pasipo utashi wake.

Majuto yanakuwa makubwa zaidi, maana mara nyingine hata usiri unakuwa haupo, heshima na nidhamu yako yote inaathirika. Zipo pombe ambazo badala tu ya kukuondolea aibu, zinaweza kukulegeza mwili na viungo na kuongeza hamu ya ngono.

Ndio maana watu wanaotumia vilevi wanashauriwa kuwa na wenza wao katika nyakati hizi ili walau wajizuie kuingia mitegoni.

Watu wengi tuliowahoji nyakati za ushauri wanakiri safari ya kuingia kwenye uhusiano ya kingono na watu wa nje ilisindikizwa zaidi na matumizi ya kilevi na wengine wanaendelea kukiri ni ngumu kuchepuka bila kuwa na kilevi akilini.




Kutostahimili ukaribu usio na mipaka

Kuna watu ambao wamejikuta wakikamatika katika uhusiano wa kingono na wale waliowaita marafiki wa karibu.

Mwanzoni alionekana kama rafiki, mnashauriana, mnasaidiana, mnasindikizana, mnatembeleana na wala haukuwahi kudhani mngefikia hapo mlipofikia.

Lakini kwa sababu mlishindwa kuwa makini kwenye kuilinda mipaka ya urafiki wenu, sasa uhusiano wa kawaida na wa urafiki umekuwa uhusiano wa kingono.

Hali hii huathiri uthamani wa urafiki baina ya watu na mara nyingine waliokuwa marafiki wanaweza kuwa maadui.

Ukaribu zaidi na mtu wa jinsia ya tofauti na wewe huwa sio mzuri sana kwa afya ya uhusiano au ndoa.


Kulipiza kisasi

Aina hii ya kuchepuka huwa kwa wanaume na wanawake, ingawa inaripotiwa zaidi kuonekana kwa wanaume kwa sababu ya ukweli kwamba wanaume wanaweza wakakwazika na bado wasifunguke kuelezea walivyokwazwa.

Lakini wakati huo huo wana kiu ya kulipiza kisasi kwa maumivu waliyoyapata, tofauti na wanawake ambao wao kufunguka ni rahisi na ni kawaida kwao.

Wanaume kwa kawaida wanaweza kuamua kutoka nje ya ndoa kwa sababu tu amekasirishwa na kuona haheshimiwi katika mambo fulani kwenye uhusiano.

 Kwa mfano akihisi hasikilizwi, hapewi kipaumbele, hahudumiwi, anachosema hakifuatwi, anavyotamani havifanywi basi kuna uwezekano mkubwa akaanzisha uhusiano pembeni kwa siri.

Tafiti za kisaikolojia zinasema mwanamume anapochepuka kwa msukumo wa hali kama hizi, ile hali ya kujihisi anafanya kosa inapungua au kupotea kabisa.

Kwa hiyo, anaweza kujihesabia haki kabisa kwa kile anachokifanya. Hii inaweza kumfanya aendelee kuchepuka kwa muda mrefu zaidi tofauti na mwanamke ambaye hata hali hii ikijitokeza wengi huwa wanajihisi kuhukumiwa na kujisikia vibaya moyoni.


Tabia ya asili, mfano au urithi

Pamoja na kwamba uhusiano nje ya ndoa ni tabia na mazoea ya mhusika, lakini tusisahau ziko kesi ambazo ni zaidi ya tabia.

Ziko nyakati tunazoshughulikia kesi ya ushauri unayoona wazi tabia ya mtu fulani sio ya kujitakia au matamanio ya kawaida lakini kuna udhihirisho wa nguvu inayomsukuma kufanya ngono.

Mtu anaweza kuwa hatamani kabisa au hapendi anachokifanya, lakini atajikuta tayari ametumbukia kwenye ngono na baada ya kufanya tendo hilo anajuta, lakini bado kesho atarudi kule kule.

Ipo mifano ya familia ambayo baba aliwahi kufahamika kuwa na tabia hizi za kuchepuka, kwa bahati mbaya watoto wake wakaandamwa na roho ile ile ya baba yao.

Mwisho niseme hali ya kutokuwa mwaminifu kwenye uhusiano ina nafasi kubwa sana kwenye kuleta uharibifu.

Wako walioharibu ndoa zao na zikapasuka wakati bado walikuwa wanazipenda ziendelee kuwepo. Japokuwa kuchepuka hufanywa kwa siri kubwa, lakini mara nyingi huwa ni za muda mfupi na kuna nyakati zinavuja au kuibuliwa na hapo ndipo machungu, majuto na machozi hutokea. Inawezekana majuto na machozi yakakupa nafasi ya kujirekebisha na kuiboresha ndoa yako iliyopata nyufa baada ya kuchepuka, lakini inawezekana kabisa ukajuta, ukalia sana na bado usiiokoe ndoa yako, maana yamkini mwenzako hatakuwa tayari kuendelea na wewe.

Kama unaipenda ndoa yako basi utailinda kwa kuwa mwaminifu.