Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umuhimu wa Kiswahili Afrika Mashariki

Muktasari:

Huduma hii itawafaidisha wasomaji wengi duniani kote na hasa wanafunzi, walimu, watafiti na wapenzi wa Kiswahili duniani kote.

Katika makala iliyotangulia nilieleza juu ya juhudi za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilivyojitahidi kuendeleza lugha ya Kiswahili, ili iwe na taswira ya utangamano kwa wananchi wa nchi hizi. Tangu enzi za ukoloni Kiswahili kilionekana ni chombo cha kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala ya siasa, biashara, uchumi, elimu, utamaduni na ustawi wa jamii. Kuundwa kwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mwaka 1930 na baadaye Kamisheni ya Kiswahili mwaka 1999 ikaanzishwa lengo likiwa ni kuimarisha undugu huu.

Kwa kuzingatia hali hii ya ushirikiano, Kampuni ya Nation Media Group (NMG) ilibuni mradi wa kuendeleza jitihada hizi za viongozi wetu kwa kuunda mradi unaojulikana kama ‘ Swahilihub’. Swahilihub ni mradi unaotumika kuweka pamoja kazi za vyombo vya mawasiliano kama televisheni, redio na magazeti yaliyo chini ya NMG kuendeleza juhudi za kukiimarisha na kukiendeleza Kiswahili kwa wananchi wote wa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda.

Mradi huu utakuwa na tovuti moja ambayo itakuwa na taarifa mbalimbali kwa Kiswahili kama Habari, Utafiti, Tamthiliya, Riwaya, Michezo, Nyimbo, n.k. zote zikiwa kwa Kiswahili.

Wataalamu wa Kiswahili, waandishi, wachapishaji, waimbaji na waigizaji wanayo fursa ya kutunga kazi zao na kuzipitisha katika magazeti ya Mwananchi au Mwanaspoti ambayo yanamilikiwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa upande wa Tanzania na Taifa Leo kwa upande wa Kenya.

Kwa kutumia tovuti moja yanayoandikwa na Mwananchi na Mwanaspoti yatawekwa katika tovuti ambayo wadai wa Kiswahili wataweza kujua kinachoendelea Tanzania.

Huduma hii itawafaidisha wasomaji wengi duniani kote na hasa wanafunzi, walimu, watafiti na wapenzi wa Kiswahili duniani kote. Ieleweke kuwa vipo vyuo vikuu zaidi ya 100 duniani kote vinavyofundisha Kiswahili na Swahilihub itakuwa ni mwalimu bora wa Kiswahili.

Hata ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wako watu wengi ambao bado hawajawa na weledi wa kutosha wa kuzungumza na hata kusoma Kiswahili.

Hii itakuwa ni fursa nzuri ya kufundisha Kiswahili hatua kwa hatua. Hatua ya kwanza itakuwa ni Kiswahili chepesi kama kusalimiana, kufahamiana, kupata huduma za afya, kufanya biashara kwa kubadilishana vitu/fedha, kuwasiliana kwa njia ya michezo na burudani kama nyimbo na ngoma, filamu, n.k.

Kwa kutumia Kiswahili katika shughuli hizi, wananchi watajiona ni wamoja zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Hali hii ya maelewano itasaidia kupunguza migogoro baina ya makabila yaishio mipakani kwani wataweza kusuluhishana kwa kutumia lugha inayoeleweka na wengi.

Swahilihub inahitaji ushirikiano wa wadau kama Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) lenye wajibu wa kuendeleza na kukuza Kiswahili kwa mujibu wa Sheria Na. 27 ya mwaka 1967. Lengo ni kuona kuwa Kiswahili fasaha kinatumika ipasavyo katika shughuli za kazi katika ofisi za Serikali, mashirika ya umma na Taasisi zote za kitaifa na pale watakapoona misingi ya Kiswahili inakiukwa.

Hatua thabiti zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria. Mdau mwingine ni Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) ambayo ina jukumu la kutayarisha na kuthibitisha vitabu vya kiada na ziada kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Kwa kutumia lugha sanifu na iliyo fasaha, Tanzania itakuwa ni chanzo cha kuuza vitabu vyake nchi za jirani na hivyo kuwa ni vyanzo vya mapato mbali na kueneza Kiswahili sanifu.

Mdau mwingine ni Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linalosimamia sanaa nchini ikiwa ni pamoja na sanaa za kuchonga, kuchora na sanaa za maonyesho kama michezo ya kuigiza na filamu. Kwa kutumia sanaa tutaweza kukieneza Kiswahili katika nyimbo, michezo ya kuigiza na pia filamu.

Tunayo pia Wizara ya Habari, Michezo, Vijana na Utamaduni. Wajibu wake ni kuwa na sera kwa kila fani inayosimamiwa ili kuona kuwa tuna taifa lenye maadili. Kukiwa na sera ya Lugha, Taifa litakuwa lina mwelekeo unaolitambulisha duniani kwa kuwa na lugha ya taifa inayoheshimiwa kwa kutumiwa katika nyanja zake zote.

Mradi wa Swahilihub utajitahidi kuwaweka pamoja wadau hawa pamoja kama michango yao ya kujenga utangamano kitaifa, kikanda na kimataifa.