Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Upelelezi wa Polisi uwe na mwisho, hatua zifuate

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Charles Kitima

Tanzania inaingia katika kipindi cha hatari kinachoelekea kutishia misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu kutokana na ongezeko la matukio ya kuogofya ya utekaji, watu kushambuliwa na wengine kuuawa.

Matukio ya karibuni kabisa ni ya kushambuliwa Padri Charles kitima, katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kutoweka kwa mwanaharakati wa Chadema, Mdude Nyagali.

Kila mara yanapotokea matukio ya namna hii, kauli zilezile zimekuwa zikitolewa na vyombo vya dola: “Uchunguzi unaendelea.” Lakini kwa matukio yaliyo mengi, matokeo ya uchunguzi huo hayaelezwi wala kuon-ekana bayana na wahusika hawajulikani wala kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Hali hii inazua maswali mengi kuhusu ufanisi wa Jeshi la Polisi na dhamira ya kweli ya kupambana na uhalifu huu unaowadhuru raia na mali zao, jambo ambalo jeshi hilo limepewa wajibu wa kulinda.

Kama ambavyo matukio mengi yamekuwa hapo awali, haya ya kushambuliwa kwa Padri Kitima na Mdude, yamezusha hofu na maswali mengi katika jamii.

Hata hivyo, tofauti na matukio mengine, licha ya Polisi kutoa maelezo yaleyale yaliyotolewa kila mara, walau safari hii tumesikia kuna watu wamekamatwa mmoja akihusishwa na kumshambulia Padri Kitima na mwngine kwa kumtishia mtandaoni. Vilevile timu ya wapelelezi imetumwa Mbeya kufuatilia taarifa za askari kuhusika kumteka Mdude.

Pamoja na pongeza hatua hizi za awali kwa matukio haya mawili, bado yapo mengine mengi ambayo upelelelzi wake haujulikani umefikia wapi au umemalizika vipi.

Baadhi ya matukio hayo ni kama kushambuliwa kwa Tundu Lissu, kutoweka kwa Ben Saanane, Azory Gwanda, Simon Kanguye, Deusdedith Soka, Ali Kibao, Shadrack Chaula na mengine mengi, mambo ambayo ni kiashiria cha kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kutokana na hilo tumeona bora kuweka msisitizo, kwamba hali ya upelelezi usiofika mwisho haiwezi kuvumiliwa katika Taifa linalodai kuwa na misingi ya haki, uwazi na utawala wa sheria.

Pamoja na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu tukio la Kibao, ni zaidi ya miezi saba tangu litolewe, lakini hakuna mrejesho wowote kwa umma kuhusu uchunguzi huo. Mamlaka haziwezi kuendelea kutoa majibu mepesi, huku maisha ya watu yakiwekwa rehani.

Ni kweli kuwa kazi ya upelelezi ni ya kitaalamu na wakati mwingine huchukua muda mrefu, lakini hilo halipaswi kuwa kisingizio cha kutotoa taarifa za maendeleo ya uchunguzi kwa umma.

Wananchi wana haki ya kujua nini kinaendelea kuhusu usalama wao na iwapo Serikali yao inawalinda. Kauli za kukwepa kuwajibika hazisaidii zaidi ya kuendeleza hisia kwamba vyombo vya dola vinahusika au vinakingia kifua wahalifu kwa kutotenda wajibu wao.

Ni lazima Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vitambue kuwa kuchelewesha haki ni sawa na kunyima haki. Mambo haya hayawezi kuachwa yaendelee huku viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na raia wa kawaida wakiendelea kuishi kwa hofu.

Aidha, mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji mstaafu Chande Othman yafanyiwe kazi mara moja, hasa kuhusu maboresho ya mfumo wa polisi. Kukaa kimya, kuchelewesha uchunguzi au kutoa kauli zinazopingana ni kushindwa kutimiza wajibu wa msingi wa Polisi kulinda maisha ya raia na mali zao.

Tanzania haiwezi kuruhusu hali hii kuendelea kujitokeza kwa kutochukua hatua stahiki dhidi ya uhalifu. Jeshi la Polisi lifunge jalada la kisingizio cha “uchunguzi unaendelea” na badala yake litangaze maendeleo ya uchunguzi, lichukue hatua na liwajibike kwa umma.