Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Watanzania wa diaspora ni haki yao pia kupiga kura

T:


Nikiwa ughaibuni kushiriki katika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), baadhi ya watu wanajiuliza swali moja muhimu sana; la kwa nini Watanzania walioko nje ya nchi wanapoteza haki yao ya msingi ya kupiga kura?

Ni swali ambalo linapaswa kuibua mjadala wa kitaifa, hasa kwa kuzingatia mchango mkubwa wa Watanzania waishio ughaibuni katika maendeleo ya taifa letu.

Katika wiki hii ya vikao vya UNGA, mijadala mikubwa kuhusu mustakabali wa dunia inaendelea. Kuna majadiliano ya jumla, mkutano wa Biennial Summit kwa ajili ya uchumi jumuishi na endelevu, mkutano wa mazingira, afya ya akili na pia kumbukumbu ya miaka 30 ya Mpango wa Dunia kwa Vijana.

Mijadala hii yote inaonyesha namna ambavyo dunia inawajumuisha raia wake popote walipo. Hii ni tofauti kabisa na hali ya Tanzania, ambapo diaspora bado hawajapewa nafasi ya kushiriki kwenye chaguzi za taifa lao.

Baada ya kumaliza shughuli za UNGA, nitasafiri hadi Dallas kuhudhuria mkutano mkubwa wa Watanzania waishio Marekani, ujulikanao kama Tanzania Diaspora Investment Forum 2025 (TDIF).

Mkutano huu unalenga kuwahamasisha Watanzania wa ughaibuni kuwekeza nyumbani, kushirikiana na taasisi kama Tiseza na ZIPA. Huu ni mfano mwingine unaoonesha kuwa diaspora hawajakata mahusiano yao na Tanzania, wanataka kulijenga taifa lao.

Wengi wa diaspora hawa wameshaanza kuleta mafanikio yao nyumbani. Wamenunua nyumba bora, wanasaidia familia zao na wanawekeza kupitia taasisi kama UTT-AMIS.

Waziri Kombo ameeleza kuwa kwa mwaka 2024 pekee, diaspora wamewekeza zaidi ya Sh7.5 bilioni huku wakituma fedha za zaidi ya Sh2.1 trilioni kusaidia familia zao, miradi ya maendeleo na uchumi kwa ujumla.

Pamoja na haya yote, bado wananyimwa haki yao ya kupiga kura.

Ukiangalia mataifa mengine ya jirani kama Kenya, Uganda, Afrika Kusini, pamoja na mataifa makubwa kama Marekani, wananchi wao wanaoishi nje ya nchi wanaruhusiwa kupiga kura.

Wanaweza kuchagua viongozi wao bila kujali walipo duniani. Lakini sisi Watanzania bado hatujafikia hatua hiyo. Kwa nini?

Sheria yetu ya uraia ya mwaka 1995 (Sura ya 357) inatambua aina tatu za uraia: kwa kuzaliwa, kwa kurithi na kwa tajnisi (kuomba uraia). Sheria hiyo inakataza uraia pacha na ikiweka masharti kwamba Mtanzania anayepata uraia wa nchi nyingine hupoteza uraia wa Tanzania.

Hili limekuwa kikwazo kikubwa kwa diaspora wengi ambao wamelazimika kuchukua uraia wa nchi wanazoishi kwa sababu za msingi kama kazi, masomo au ulinzi wa kisheria. Hata hivyo, wengi wao bado wanajitambulisha kama Watanzania na wanatamani kushiriki kikamilifu katika masuala ya nchi yao hasa uchaguzi.

Ni wakati sasa wa kubadilika. Haki za msingi za Mtanzania ni pamoja na haki ya kuwa raia na haki ya kushiriki katika uamuzi wa nchi yake. Diaspora wengi wana vitambulisho vya Nida.

Kwa nini basi wasiingizwe kwenye mfumo wa kupiga kura kidigitali wakiwa popote walipo duniani? Teknolojia ipo, mifumo ipo, kinachokosekana ni utashi wa kisiasa na maboresho ya kisheria.

Katika muktadha huu, matumaini yanabaki kwenye mchakato wa kupata katiba mpya kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kama kitaendelea kuongoza dola.

Ikiwa chama hicho kitaibuka na ushindi Oktoba 29, mwaka huu, basi Watanzania wote ndani na nje ya nchi wanatarajia kuona katiba mpya itakayorekebisha upungufu huu.

Katiba hiyo mpya inapaswa kutambua mchango wa diaspora na kuwapa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi mkuu kikamilifu, hasa wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni muhimu kutambua kuwa Watanzania waishio ughaibuni si wageni wa nchi hii. Wao ni sehemu ya taifa. Wanachangia uchumi, wanasaidia familia zao na wanashiriki katika maendeleo ya jamii. Kuwanyima haki ya kupiga kura ni kuwanyima sauti yao katika uamuzi wa taifa lao.

Binafsi naiona hatua ya kwanza ya kufanya ni kuwaruhusu kupiga kura kwa njia za kidigitali kwa wale waliothibitishwa na Nida. Hatua ya pili ni kurekebisha sheria ya uraia ili kuruhusu uraia pacha kwa masharti maalum. Hatua ya tatu ni kuhakikisha Tume Huru ya Uchaguzi inaandaa mfumo rafiki kwa diaspora kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Kwa kuwa uchaguzi mkuu unakaribia, kila Mtanzania aliye ndani ya nchi na mwenye sifa, anapaswa kujitokeza kupiga kura.

Lakini pia tusisahau kupaza sauti kwa ajili ya wale walio nje ili nao kesho na keshokutwa wapate nafasi ya kuchagua viongozi wa nchi yao. Huu ndio usawa wa kweli wa kisiasa.