Prime
Samia aahidi kongani ya viwanda, Ruvuma kuwa kitovu cha biashara
Muktasari:
Ni vile vitakavyoanzishwa kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya chakula na biashara, misitu na madini. Wananchi wasema ukosefu wa ajira ni tatizo sugu kwa watu wa mkoa huo.
Ruvuma. Ahadi ya kuanzisha kongani za viwanda na kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa kitovu cha biashara ukanda wa kusini, imeibua matumaini kwa wakazi wa mkoa huo hasa vijana wanaokabiliwa na changamoto ya ajira.
Viwanda hivyo ni vile vitakavyohusika na kuongeza thamani ya mazao ya chakula na biashara, misitu na madini katika Wilaya za Mbinga, Namtumbo, Nyasa na Songea.
Ahadi hiyo imetolewa leo Jumatatu Septemba 22,2025 na mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ikiwa ni siku ya pili na ya mwisho ya ziara yake ya mikutano ya kampeni mkoani humo.
Akihutubia wanachama wa CCM na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Songea Mjini, Samia amesema endapo atapa ridhaa ya miaka mitano mingine ya kuongoza nchi, mkoa huo utanufaika na kongani za viwanda zitakazozalisha ajira.
Sambamba na kuanzishwa kwa kongani hizo, Samia ameahidi kuendelea kutekeleza miradi ya kuunganisha umeme katika vitongoji vyote mkoani humo ili viwanda hivyo viweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuwavutia wawekezaji wengine.
“Tunataka tutakapoanza kuweka kongani za viwanda, kwenye kila wilaya umeme uwe umeshafika. Hili litakwenda sambamba na kuboresha huduma za mawasiliano, kama tunataka kuufanya mkoa huu kuwa kitovu cha biashara ni lazima huduma hizi muhimu zipatikane kutavutia wawekezaji zaidi.
“Madaba tutaweka viwanda vya kuongeza thamani mazao ya misitu ili kuongeza ajira na kukuza uchumi kwa ujumla na uchumi wa vijana. Tunakusudia pia kuweka viwanda vya kuongeza thamani ya zao la kahawa na parachichi lengo likiwa ni kuhakikisha mazao haya yanauzwa yakiwa yameongezwa thamani,” amesema Samia.
Ahadi hiyo imeonekana kupokewa vyema na wakazi wa mkoa Ruvuma, akizungumza na Mwananchi Rebeca Mbepela amesema ni taarifa inayotoa matumaini makubwa hasa kwa vijana ambao wanahangaika mtaani.
“Watoto wetu wako tu nyumbani hawana ajira tumewasomesha lakini bado wameendelea kuwa mzigo, tunaposikia ahadi ya namna hii naona kabisa inaenda kugusa maisha ya wengi, nimesikia mengi ila hili ndiyo limenigusa naamini likitekelezwa kama lilivyosema litaleta manufaa makubwa,” amesema Rebeca.
Kwa upande wake Selestine Mapunda mkazi wa Matarawe amesema ukosefu wa ajira ni kilio cha watu wengi hivyo hatua ya kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao mkoani humo kutaleta ahueni.
“Sio kwamba watu wanapenda kuwa kwenye umaskini ukweli ni kwamba hawana vya kufanya sasa hivi Songea imeshakuwa mji mkubwa kama huna chanzo cha kukuingizia kipato maisha lazima yawe magumu.Tukipata hivyo viwanda na hizo shughuli za bandari ya Mbamba Bay italeta unafuu mkubwa,” amesema.
Mbali na ahadi hiyo ya kongani ya viwanda Samia amesema akipata ridhaa ya kuongoza tena, Serikali yake itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo ikiwa ni pamoja na huduma za ugani.
“Niwashukuru Wana Ruvuma mmeweza kuchangia vyema kwenye suala la usalama wa chakula ndani na nje ya nchi. Niwasihi mbolea na pembejeo zinazotolewa kwa ruzuku mzitumie msiuze kwa kuwa mkiuza mnawapa faida watu wa nchi jirani mnaowauzia,” amesema Samia.
Ameahidi pia kujenga soko la kisasa eneo la Manzese akieleza kuwa ujenzi huo utahusisha miundombinu ya kuwawezesha wamachinga waweze kufanya biashara zao.
Kuhusu miundombinu ya barabara amesema Serikali yake itaendeleza miradi ya ujenzi ambayo ilianza kutekelezwa chini ya ilani ya 2020/2025 kabla ya kuanza miradi iliyoelekezwa kwenye ilani mpya.
Hata hivyo amekubali kulifanyia kazi ombi la mgombea ubunge Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro aliyeomba kujengwa kwa barabara ya bypass yenye urefu wa kilomita 14 ili kukabiliana na msongamano wa magari ambao umeanza kuonekana katika mji huo.
Akizungumza kwenye mkutano huo mgombea mwenza kwa tiketi ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wakazi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku uchaguzi.
“Katika mikoa 11 niliyopita wamesema wataichagua CCM hasa watani zetu wasukuma wamepania kuongoza kwa wingi wa kura, sasa ndugu zangu wa Ruvuma naomba tushindane na mikoa mingine tuwashinde kwa kura nyingi.
“Heshima niliyopewa ya kuwa mgombea mwenza ni ya mkoa wa Ruvuma naomba tulipe kwa kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo. Tunza kitambulisho chako na siku hiyo uwahi mapema kituoni ukapige kura,” amesema Nchimbi na kuongeza:
“Nakumbuka mwaka 2015 nilipoungana na mama Samia kwenye kampeni Lindi na kueleza kuwa nastaafu siasa uliniambia wewe ni kijana wetu huwezi kupumzika, tutakutumia kwa mambo mengine nilijiuliza ni yapi haikupita muda nikateuliwa kuwa balozi kisha katibu mkuu wa chama. Nina kila sababu ya kusema asante kwa imani hii.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho amesema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Samia amewatendea haki wananchi wa Ruvuma.
“Kwenye ilani ya 2025/2030 tumeona kuna miradi mingine hii ndiyo sababu wananchi wana imani na wamenihakikisha kwamba kura zao zote zitaenda CCM.
“Kitendo cha kumchagua mtoto wa Ruvuma kuwa mgombea mwenza kimetuongezea furaha na hamasa kubwa, tembea kwa kujiamini kura zote za mkoa wa Ruvuma ni zako. Tumejipanga hakuna hata jimbo moja litakalopotea katika mkoa wetu,”
Wagombea ubunge wanena
Mgombea wa ubunge viti maalumu mkoa wa Ruvum,a Jackline Msongosi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Samia imefanyika kazi nzuri mkoani humo zilizochagiza ustawi wa wanawake.
“Changamoto ya maji inamhusu mwanamke, katika mkoa wetu tunapata maji kwa asilimia 86, tunashukuru pia kwa ruzuku ya mbolea, viatilifu na mbegu kwa haya yote wanawake tuna kila sababu ya kukupa kura zetu,” amesema.
Mgombea ubunge wa viti maalumu, Mariam Joka amesema fedha zilizotolewa kwa ajili miradi ya maendeleo mkoani humo zimegusa katika sekta zote ikiwemo elimu, afya, maji na nyinginezo za kijamii.
“Ukija kwenye kilimo tumepata ruzuku za pembejeo, tunapata mbegu bora zinazowezesha mkoa wetu kuendelea kufanya vizuri kwenye uzalishaji wa mazao. Hatuna cha kulipa zaidi ya kuahidi kura za kutosha,” amesema Mariam.
Mgombea ubunge jimbo la Madaba, Omary Msigwa amesema licha jimbo hilo kupata hospitali iliyowaondolea adha ya kutembea kilomita 120 kufuata huduma bado wana uhitaji wa vituo vya afya na nyumba za watumishi.
“Wananchi Madaba wameachana na kusafiri kilomita 120 kufuata huduma za afya kufuatia kujengwa hospitali. Ila huko mbele tunaomba tupate vituo zaidi na nyumba za watumishi.
“Pia tunaomba ufanyike uboreshaji wa barabara ya Wino-Upinga kilomita 48 imekuwa ikikata mawasiliano kipindi cha masika. Tunaomba pia viwanda vya kuchakata mazao na stendi ya mabasi Madaba pamoja na soko kuu la kisasa katika mji wa Madaba,” amesema Msigwa.
Naye mgombea ubunge jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama amesema uamuzi wa kuweka ruzuku kwenye mbolea umechangia kwa kiasi kikubwa wakazi wa jimbo la Peramiho na mkoa mzima wa Ruvuma kuongeza uzalishaji kwenye kilimo.
Amesema ruzuku za mbolea imesababisha kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 1.3 milioni hadi tani 1.5 milioni.
“Ulipoingia mwaka 2021 nyuso za wakazi wa Peramiho zilikuwa na masikitiko kutokana na bei ya mbolea lakini sasa ruzuku imesababisha kilimo kuongezeka na maisha ya wakazi yamebadilika, sasa wamejenga nyumba za bati na vijana wamenunua bodaboda,” amesema Jenista.