Kaluta Amri Abeid na Saadan Abdu Kandoro
Jalada la Kitabu cha Historia ya Kaluta Amri Abeid.
Muktasari:
Mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa. Mwandishi mashuhuri Mathias Eugen Mnyampala akiandika juu ya maisha yake, alimtaja Kaluta Amri Abeid kama mtu hodari wa kutumia lugha ya Kiswahili katika fani ya kuimba Tajiwidi, mashairi na tenzi kwa mahadhi ya namna mbalimbali ya maghani.
Tunaendelea na maelezo kuhusu mchango wa Hayati Kaluta Amri Abeid, gwiji wa mashairi ya Kiswahili. Alikuwa pia na kipaji cha kusoma mashairi ya Kiingereza, Kiarabu, Kiajemi na Kiurdu.
Mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa. Mwandishi mashuhuri Mathias Eugen Mnyampala akiandika juu ya maisha yake, alimtaja Kaluta Amri Abeid kama mtu hodari wa kutumia lugha ya Kiswahili katika fani ya kuimba Tajiwidi, mashairi na tenzi kwa mahadhi ya namna mbalimbali ya maghani.
Kaluta kama mshairi:
Sheikh Kaluta Amri Abeid alitumia kipaji chake cha kuimba na kughani mashairi na tenzi na kuenzi matumizi ya Kiswahili akizidisha maneno yenye utamu na nahau ili kuwahamasisha wasomaji wa mashairi yake waijue lugha ya Kiswahili na kuithamini. Katika kitabu chake alichotunga na kukiita, ‘Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani za Amri’ (1953) aliwasaidia sana waandishi chipukizi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla kwa umahiri wake. Ilielezwa kuwa kitabu hiki kitawasaidia sana wale wanaojifunza utunzi wa mashairi. Kinatumika shuleni, vyuoni na asasi za lugha ya Kiswahili.
Alipokuwa na umri wa miaka 13 alifiwa na baba yake na aliwahi kutunga shairi la kumwombolezea baba yake kama:
Mola murehemu baba, baba aliyenizaa
Mola ni wewe Tawaba, mghofiri dhambi pia,
Peponi mpe maaba, na vyeo mzidishia,
Dua nitakabalia, Mola mghofiri baba.
Baba mwingi wa huruma, kwa wema alinilea,
Akaniita kusoma, dini na dunia pia,
Akanifunza ya wema, ya akhera na dunia,
Dua nitakabalia, Mola mghofiri baba.
Baba ninamkumbuka, vile nilivyomjua,
Mkarimu hana shaka, ni mwenye hadhi na sitawi,
Ni mtu alotukuka, vyeo akavipandia,
Dua nitakabilia, Mola mghofiri baba.
Huu ni mfano wa kazi ya ushairi inayoonyesha uwezo wake tangu akiwa mdogo.
Kaluta Amri Abeid kama karii:
Kutokana na umahiri wake katika kujishughulisha na lugha ya Kiswahili na uga wa ushairi, alichaguuliwa kama karii wa mashairi ya Kiswahili (yaani msomaji, mkosoaji na mwelekezaji wa matumizi na maandishi ya Kiswahili. Alipokuwa Tabora aliandika makala yake na kukitukuza Kiswahili akisema: “Kwa bahati tu nilizaliwa katika mji ambao Kiswahili kilizungumzwa wakati wote. Hivyo tangu nikiwa mtoto nililazimika kukitumia Kiswahili kama chombo cha kazi. Niliyachunguza maneno kabla ya kuyatumia wakati wa kuandika au kuzungumza. Pia nilifanya marekebisho ya maandishi ya waandishi.”
Kaluta Amri Abeid kama mwanaharakati:
Sheikh Kaluta Amri Abeid alichochea kasi ya matumizi ya Kiswahili kwa madhumuni ya kutukuza lugha ya Kiswahili.
Alikuwa na ushupavu wake katika kutetea misingi imara ya lugha ya Kiswahili aklisema: “Alikuwa hodari wa mijadala kwenye mashindano ya dini wakati yungali kiongozi wa dini.” Alishinda malumbano yaliyotokea baina yake na Dkt Lyndon Harries kutokana na mashairi guni hasa yaliyo katika kitabu kilichotafsiriwa na Mwalimu J.K. Nyerere cha Julius Kaisari (Shakespere). Alisisitiza kuwa Kiswahili ni lugha pekee inayofaa kuwa lugha ya Taifa na ya Serikali kwani inazungumzwa na watu wengi na imesheheni maneno mengi ya Kibantu. Pia sarufi yake ni ya Kibantu na ni rahisi zaidi kwa wananchi kujijua kuliko lugha za kigeni.
Kwa msisitizo mkubwa aliwakejeli kundi la watu waliotaka kutumia lugha za kigeni kama Kiingereza na Kiarabu ambao kwa hakika hawakuzijua vilivyo lugha hizi kwa kuzungumza au kuandika.
Alikuwa na mapenzi makubwa ya Kiswahili na tarehe 18/01/1962 aliandika makala kwenye mkutano yenye kichwa cha habari ‘Hatima ya Kiswahili’ akiwataka wananchi kukienzi, kukitukuza na kuweka nia njema ya ari thabiti ya kujifunza Kiswahili.
Alitafsiri Kurani Tukufu kwa Kiswahili na alipokuwa Waziri wa Sheria alitafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili na kuwafanya wananchi kuwa na shauku ya kujifunza sheria kwa Kiswahili.
Kuwa Mwenyekiti wa chama cha Kiswahili Afrika Mashariki
Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Washairi wa