Kila la heri Tamasha la Sanaa Bagamoyo

Wasanii wakifanya yakwao jukwaani
Muktasari:
Hili ni tamasha pekee linaloandaliwa na kuratibiwa na taasisi ya kiserikali, likibeba picha ya utamaduni wa Mtanzania halisi, likikutanisha mataifa mbalimbali kama washiriki lakini pia watazamaji.
Jumatatu ya Septemba 22, Tamasha la 33 la Sanaa la Bagamoyo litaanza, likiratibiwa na Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo, ikiwa ni sehemu ya kuonyesha vipaji walivyozalisha kwa mwaka huu, lakini pia ni msimu wa burudani na furaha kwa wakazi wa Bagamoyo na vitongoji vyake.
Hili ni tamasha pekee linaloandaliwa na kuratibiwa na taasisi ya kiserikali, likibeba picha ya utamaduni wa Mtanzania halisi, likikutanisha mataifa mbalimbali kama washiriki lakini pia watazamaji.
Kwa mwaka huu, tamasha hilo linatarajiwa kuhusisha makundi zaidi ya 40 ambayo ni rafiki wa Tamasha la Sanaa Bagamoyo. Vikundi hivyo ni vya hapa nchini, nchi jirani pamoja na Ulaya hali inayoleta sura ya kimataifa katika mtazamo wa kiutamaduni.
Kizuri na cha kufurahisha kuhusu tamasha hili ni kwamba, pia limebeba dhana ya kuwatambulisha wageni watakaoshiriki ambao pia wataelezwa na kuonyeshwa utamaduni wa Mtanzania na vivutio vya utalii ili wakirudi makwao, wakaeleze uzuri wa Tanzania na watu wake.
Kama inavyotambulika, Bagamoyo ni eneo linalotambulika kihistoria dunia nzima kutokana na kuwa moja ya vituo vikuu vya biashara ya utumwa enzi za ukoloni, ambapo maeneo mbalimbali yalihusika katika biashara hiyo inayosimuliwa zaidi katika historia ya Tanzania.
Ukiachana na biashara ya utumwa, kuna vivutio mbalimbali vinavyopatikana maeneo kama ya Kaole, Mbegani na kwingineko, ambapo wageni wangependa kuona au kupiga picha za kumbukumbu katika maeneo hayo ya kihistoria.
Mpaka hapa tunapata picha kamili kwamba huenda tamasha hili likawa lenye mtazamo mwingine kabisa likilinganishwa na matamasha mengine yote ambayo hufanyika Tanzania na huenda likawa na hadhi zaidi kwa kile kitendo cha kuenzi utamaduni, lakini pia katika kuitangaza nchi nje ya mipaka yake.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa tamasha hilo Abdulrahman Bura, tamasha hili halihusishi kwa kiwango kikubwa na muziki wa kizazi kipya. Lenyewe linahusisha muziki wa asili ya Tanzania, huku vipaji vipya ambavyo vimefundishwa na kuhitimu chuoni hapo vikipewa kipaumbele.
Changamoto inayolikabili tamasha hili ni wadau wa kujitokeza na kulidhamini.
Wengi wamekuwa wakilikwepa na kudhamini matamasha ya muziki wa kizazi kipya ambayo yameonekana kuwa na faida binafsi kwa kampuni mbalimbali.
Tofauti na matamasha mengine, ni katika Tamasha la Bagamoyo pekee, vikundi huchangia gharama za uendeshwaji wake bila kuchoka, huku wasanii hao wenye moyo na sanaa yao wakiamini kwamba ipo siku sauti yao itasikika na lengo lao la kutangaza utamaduni na utalii wa nchi litatimia.
Sisi hii tunaiona kuwa ni hatua kubwa ya kupigiwa mfano na tunaiita ya kizalendo. Zaidi, tunaipongezakwani ni wasanii wachache wenye moyo kama huu wa kufanya kazi kwa miaka 33, bila kuchoka, wala malipo. Tunaamini wanafanya hivyo wakijua kwamba kuna wenzao wanalipwa na kuna wadhamini katika tasnia hii.
Mwisho, tunawatakia kila la heri walimu, kamati ya maandalizi na washirika wote wa tamasha hili la kimataifa. Pia mtambue kwamba Tamasha la Sanaa Bagamoyo, siyo dogo kama ambavyo baadhi ya wadau wanavyodhani. Hilo ni tamasha kubwa, lenye sura ya kimataifa, hivyo tunategemea likifanyika kwa weledi kuashiria ukomavu hata kufikia miaka 100 . Kila la heri washiriki wote.