Giannis afunga pointi 50, Bucks bingwa NBA

Giannis afunga pointi 50, Bucks bingwa NBA

Muktasari:

  • Giannis Antetokounmpo jana alifunga pointi 50 za kihistoria na kwa wakati zikihitajika zaidi, alipoiongoza Milwaukee Bucks kutwaa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1971 ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) kwa kuilaza Phoenix Suns kwa pointi 105-98.

Milwaukee, Marekani. Giannis Antetokounmpo jana alifunga pointi 50 za kihistoria na kwa wakati zikihitajika zaidi, alipoiongoza Milwaukee Bucks kutwaa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1971 ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) kwa kuilaza Phoenix Suns kwa pointi 105-98.


Bucks imeshinda fainali hiyo inayohusisha mechi saba kwa kuibuka na ushindi katika mechi nne dhidi ya mbili za wapinzani wao na kuwa timu ya tano katika historia ya NBA kutwaa taji hilo baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo.


Antetokounmpo, ambaye anakuwa mchezaji wa saba katika fainali hizo kufunga pointi 50 katika mechi moja, alitumbukiza vikapu 17 vya mipira ya adhabu kati ya 19 na kunyakua ribaundi 14 huku akifuta mipira mitano wakati Bucks ikiondoa ukame wa takriban nusu karne wa kukosa kombe.


"Naishukuru Milwaukee kwa kuniamini. Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa kujituma pamoja nami," alisema Antetokounmpo. "Nashukuru niliweza kufanikisha."


Kitendo cha mchezaji huyo mwenye miaka 26 raia wa Ugiriki kufunga pointi 50 kimemfanya alingane na Bob Pettit aliyefikia idadi hiyo mwaka 1958 alipoiongoza St. Louis Hawks kuishinda Boston.


"Alituweka nyuma yake. Tulipomuhitaji, alituambia tumpe mipira tu," mlinzi wa Bucks, Khris Middleton alisema. "Inafurahisha kuwa katika safari hii pamoja naye."


Antetokounmpo, ambaye ameshinda tuzo ya mchezaji bora mara mbili na ambaye kulikuwa na wasiwasi wa hali ya goti lake kabla ya mechi ya kwanza, pia analingana na Michael Jordan na Hakeem Olajuwon kwa kushinda tuzo mbili za mchezaji bora wa fainali hizo na mchezaji bora wa mwaka anayejihami katika msimu mmoja.


"Ni binadamu wa aina yake. Nimejifunza mengi kwake. Ni kiongozi wa aina yake," alisema kocha wa Bucks, Mike Budenholzer. "Wachezaji hawa ni mabingwa. Wanafurahia kuwa bora kila siku."


Naye Mgiriki huyo alikuwa na maneno ya shukrani kwa timu na kocha wake.
"Nina furaha nimeweza kufanya hili kwa ajili ya Milwaukee," alisema Antetokounmpo. "Na kocha Bud anasema lazima tufanye hivi tena."


Suns haikuweza kufurukuta katika kampeni yao ya kutaka kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza katika historia yao ya miaka 53. Mlinzi wa Phoenix, Chris Paul, akicheza fainali hizo kwa mara ya kwanza katika miaka 16 aliyocheza NBA na sasa akiwa na miaka 36, aliongoza ufungaji kw aupande wa Suns akiingiza pointi 26.


"Inaumiza, vibaya sana," alisema kocha wa Suns, Monty Williams. "Lakini ninashukuru sana tulipata nafasi ya kugombea ubingwa. Robo ya nne ilikuwa ni ushahidi mzuri kwamba tusingeweza kufunga kiasi cha kutosha. Yaani, hatukuweza kutumia nafasi."