Mpole atimkia FC Lupopo

WAKATI mshambuliaji George Mpole akizua sintofahamu kufuatia kuvunjwa mkataba na klabu yake ya Geita Gold jamaa anajielewa bana, Jana ametua nchini DR Congo kukamilisha dili lake na moja ya klabu kubwa ya huko.

Taarifa ambazo Mwanaspoti inauhakika nazo zaidi ya asilimia 80 ni kwamba Mpole ambaye alikuwa mfungaji bora msimu uliopita ametua Jiji la Lubumbashi tayari kwa kujiunga na matajiri wa FC Lupopo ya huko.

Hatua hiyo inakuja kufuatia Mpole kuvunjwa mkataba na Geita kwa kununua mkataba wake uliosalia kisha kuwalipa keshi wachimba madini hao ambao nao walibariki na kukubaliana na mchana nyavu huyo kutimka ndani ya timu yao.

Mapema Mwanaspoti linafahamu Lupopo ilikuwa ikisaka mshambuliaji mzuri na baada ya kuwafanyia tathmini Mpole na Reliant Lusajo waliamua kumchukua Mpole.

Mpole aliondoka nchini juzi kwa siri kubwa kwa Ndege ya Shirika la Tanzania na jana alikutana kwa mara ya kwanza na matajiri wa Lupopo kukamilisha dili hilo.

Mwanaspoti linafahamu zaidi Lupopo walimwekea ofa kubwa Mpole ambayo hakuna staa anayeweza kuifikia kwa wachezaji wanaocheza sasa katika klabu za Simba na Yanga.

Mpole ukiachana na dau lake la usajili imefahamika atakuwa anachukua kiasi cha Dola 12,000 kwa mwezi sawa na (Sh27.6 milioni) ndani ya Lupopo.

Pia atakuwa na bonasi zingine kama atakuwa na moto katika ufungaji huku pia akipewa nyumba na gari ya kutembelea.

Msimu uliopita Mpole alikuwa kinara wa mabao akifunga mabao 17 rekodi ambayo iliwavutia Lupopo hasa baada ya kumshinda Mkongomani Fiston Mayele aliyemzidi kwa bao moja.

Hata hivyo, msimu huu licha ya kufunga mabao 2 tayari mpaka anaondoka Geita mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa Stars alitumia muda mwingi akiwa nje akisigana na uongozi wa klabu yake.