‘Sh1.6 bilioni idaiwe wizara siyo TFF’

Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
Muktasari:
Ni mkanganyiko unaoendelea kuhusu kodi ya mishahara ya makocha.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeambiwa iikabe koo Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kuhusu fedha za kodi ya makocha wa kigeni badala ya kulibebesha mzigo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
TRA imekuwa ikitakiwa ilipe Sh1.6 bilioni kama kodi ya makocha hao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah akisema shirikisho hilo halipaswi kulipa kodi hiyo kwa kuwa wizara ndiyo mlipaji wa mishahara ya makocha wa timu ya Taifa, ikiwa ni ahadi ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ya kulipia makocha wa michezo tofauti, ukiwamo mpira wa miguu.
Wiki iliyopita, TRA ilishikilia kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti za TFF kwa kile ilichodai kuwa kinatokana na kodi ya Lipa Kadri Upatavyo (PAYE) kwa makocha wa timu ya Taifa, kati ya mwaka 2010 na 2014.
Aidha, inadaiwa pia TFF haikulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa TRA ya Dola 6 milioni kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars na Brazil mwaka 2010, ikiwa ni mechi ya kirafiki wakati timu hiyo ya Brazil ikijiandaa na mchezo wa Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.
Kuhusu suala hilo Osiah amewataka TRA kuacha kuangalia kwa juu juu mkataba wa makocha wa Stars kwa kuwa waliingia TFF, lakini kuna kipengele kinachoonyesha Serikali ndiyo inayomlipa kocha.
“Sheria ya kodi, kifungu cha 80 (1) kinasema mwajiri ndiye atalipa mshahara, Serikali ndio inayomlipa kocha, TFF hailipi mshahara wa kocha italipaje kodi?” alihoji.
Alisema, “Utengenezwe mfumo sahihi wa malipo ya makocha kuliko ilivyo sasa kila siku itakuwa ni kugombana na TRA, halafu kwa vile fedha zilitoka moja kwa moja kwa Rais wote walioogopa kuhoji, wasiionee TFFna kuibebesha mzigo usiostahili wangalie nani analipa mshahara, alafu watake mtu mwingine alipe kodi, si sahihi.”
Osiah alisema, “Mechi ya Brazil iliundwa kamati maalumu na Serikali na katibu wa ile kamati ni mwekahazina wa wizara na ndiye aliyeshugulikia mambo yote mpaka kufungua akaunti maalumu, aulizwe yeye, TFF wangekataje VAT wakati fedha hazikupita kwao, TFF watakataje makocha kodi wakati Serikali inamlipa kocha mshahara moja kwa moja?” alihoji Osiah.
Aliongeza kuwa makubaliano yao na Serikali ni kuwa mkataba kocha Poulsen mkataba ule tulikubaliana TFF ilipe ziada ya fedha ambazo kocha amehitaji.
“Mfano, kama Serikali ilikuwa ikitoa Dola 10,000, basi Dola 7,000 zinatoka TFF na ikakubalika Serikali ikate kodi ya zile inazotoa na TFF ikate kodi ya ziada inayotoa.
“Kikao cha mwisho kilifanyika kati ya TFF, katibu mkuu wa Wizara ya Habari, viongozi wa Wizara ya Fedha na TRA, makubaliano ilikuwa ni Serikali ibadili mfumo, aidha fedha za kocha zikatwe kodi moja kwa moja ndipo wamlipe au zipite TFF, kisha TFF ili izikatie kodi, lakini mpaka tunaondoka Serikali ilikuwa bado haijatekeleza hilo, pia TFF walipoingia madarakani hawakuendeleza mazungumzo yale,” alisisitiza.
Majibu ya TRA
Ofisa Mwandamizi, Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Hamis Lupenja alifafanua sakata hilo alieleza kuwa ni malimbikizo ya makato ya makocha wa timu ya Taifa tangu enzi za Mbrazili Marcio Maximo.
“Makocha wa timu ya Taifa waliingia mkataba na TFF na si Serikali, hivyo TFF ndiyo ilipaswa kukata malipo ya kodi katika mishahara yao kwani yenyewe ndiyo ilikuwa mwenyeji wao hapa nchini ikashindwa kufanya hivyo.
“TRA inachokijua ni makubaliano ya kimkataba kati ya waliokuwa waajiri wake (makocha) na siyo Serikali, hivyo yenyewe ndiyo ilifanya makosa kushindwa kuwakata kodi waajiriwa wake na ikalimbikiza madeni, hicho ndicho chanzo,” alisema Lupenja.
Malinzi, Thadeo wanena
Kwa upande wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema amehuzunishwa na suala hilo la TRA ambalo linamtoa roho kwa kuwa ametumia nguvu nyingi kuwekeza katika maendeleo ya soka mipango ambayo imevurugika.
“PAYE ilipaswa kulipwa Hazina na siyo TFF kwa kuwa wao ndiyo wanalipa makocha mishahara, TFF kosa lake ni nini hapa, na tayari walishachukua Sh157 za klabu na waliahidi kuzirudisha baada ya kubaini ukweli mpaka leo hazijarudi.”
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo aliliambia gazeti hili jana kuwa, hawawezi kuingilia suala hilo kwa kuwa hawajapata taarifa rasmi kutoka TFF. “Hatuna taarifa juu ya suala la TFF na TRA, kama wangetupa taarifa rasmi tungejua jinsi ya kufanya, lakini sasa hatuwezi kusema chochote juu ya hilo kwa kuwa siyo taarifa rasmi,” alisema Thadeo.
Kabla ya kuondoka madarakani, Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani, 2005 alijua kuwa kuna tatizo kwenye mpira ndipo akatoa ahadi ya kulipa makocha pia hivi karibuni kwenye tuzo alizoandaliwa na waandishi wa habari, Kikwete alisisitiza kuendelea kumlipa kocha, Boniface Mkwasa kwa kiwango kile kile alichokuwa Serikali inawalipa walimu wa nje.