Usajili wa Mbombo balaa! Mabosi Yanga wakuna vichwa

Saturday January 02 2021
mbombo pic
By Olipa Assa

KIKOSI cha Yanga kimeshatua jijini Dar es Salaam kutoka Nyanda za Juu Kusini kilipoenda kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara, ili kujiandaa na michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021, lakini unaambiwa yule straika mwenye nafasi kubwa ya kusainishwa Yanga wiki ijayo, Idriss Mbombo amewabana mabosi wa Jangwani kwa kuwaambia wazi kuwa anataka mshahara wa Dola 10,000. Hiyo ni sawa na Sh23 milioni.

Vinara hao wa Ligi Kuu waliotoka sare ya 1-1 juzi mjini Sumbawanga dhidi ya Tanzania Prisons ikiwa ni siku chache tangu waifumue Ihefu mabao 3-0, itaanza mechi za Kombe la Mapinduzi, Jumanne ijayo, kwa kuvaana usiku na Jamhuri ya Pemba, lakini akili za mabosi ni kuvuta straika mmoja matata dirisha dogo la usajili linalofungwa Januari 15.

Moja ya mastraika anayepigiwa hesabu na ambao wameshafanya mazungumzo naye ni Mbombo ambaye ameweka bayana dau analotaka upande wa mshahara.

Kama Yanga wakipitisha dau hilo, anakwenda kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara.

Yanga inamtaka staa huyo raia wa DR Congo kwa udi na uvumbi ili kukoleza safu yao ya ushambuliaji kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na kubeba ndoo.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezinasa kutoka kwa mmoja wa vigogo wa Yanga ni kwamba makubaliano yanakwenda vizuri na Mbombo tatizo bado lipo kwenye dau.

Advertisement

Habari zinasema kwamba mchezaji huyo ambaye ni swahiba wa Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe anasubiri simu ya Yanga tu kuaga Nkana ya Zambia ili aje Tanzania.

Licha ya Yanga kufanya siri kubwa usajili wa mchezaji huyo, Mwanaspoti linajua kwamba moja ya vitu vinavyowaumiza kichwa Yanga ni dau lake la mshahara wa milioni 23.

Lakini amewapagawisha viongozi baada ya kuwasisitiza kwamba: “Niwekeeni mzigo mezani, mimi nakuja kufanya maajabu.”

Mbombo aliliambia Mwanaspoti juzi kwamba makubaliano yake na Yanga ni siri, lakini kama wakimkamilishia waliyokubaliana na akatua Dar es Salaam atafunga sana kutokana na aina ya viungo waliopo sasa ambao anawaona kwenye televisheni na mitandao.

Mchezaji huyo ameliambia Mwanaspoti kwamba ana uhakika wa kutupia sio chini ya mabao 17 kama akitua Yanga.

Dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara linafungwa wiki mbili zijazo. Tayari Yanga imeshamsajili Saido Ntibazonkiza kutoka Burundi na ameshaanza kung’ara.

Advertisement