Vijana wa Ligi Kuu waliokubalika mapema

Monday November 23 2020
vijana pic
By Mwandishi Wetu

Ukipita mitaani huko hususani kwenye vijiwe vya kahawa na sehemu nyingine ambazo zinakusanya watu wanaoongelea soka utakutana na midahalo mbalimbali juu ya soka ambapo zingatio kuu huwa juu ya umri wa wachezaji wakati wengi wakiamini kuwa soka linapaswa kuchezwa na vijana wadogo ambao damu zao bado zinachemka.

Wengi wa vijana hao wamekuwa wakisajiliwa na timu lakini wasipate nafasi za kucheza kwenye vikosi vya kwanza kulingana na uwepo wa wakongwe kwenye timu.

Kibwana Shomary (Yanga)

Beki huyu wa pembeni (kulia) amesajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar ambapo mashabiki wengi wa timu hiyo walijawa na hofu juu ya usajili wake wakiamini kwamba kwakuwa umri wake ni mdogo (20), basi atakua hajakomaa kucheza kama ilivyokuwa kwa beki kisiki na mkongwe aliyekuwa akicheza nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka mitano kwenye timu hiyo Juma Abdul kuachwa.

Lusajo Mwaikenda (KMC)

Akiwa na miaka 20 tayari amemshawishi kocha mkuu wa KMC Habib Kondo, kumuingiza kwenye kikosi cha kwanza na kucheza kama mlinzi wa kati akisaidiana na mkongwe Andrew Vicent ‘Dante’ huku akionesha uwezo mkubwa wa kukaba, kuzuia na kuipanga timu pale inapobidi.

Advertisement

Lusajo ni miongoni mwa makinda waliokulia kwenye akademi ya Azam FC ambao kwa asilimia kubwa msimu huu wengi wao wamepata timu za kucheza na kuonesha uwezo wao.

Cyprian Kipenye (Ihefu)

Akitokea kwenye akademi ya mabingwa wa msimu ulioisha Simba, mshambuliaji huyu ameweza kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha wakubwa kwenye Timu ya Ihefu ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu.

Umri wake ni miaka 18 pekee lakini namna anavyopambana na mabeki wakongwe na wazoefu kwenye ligi huu utadhani naye ni mkongwe, hiyo ni moja ya sababu kuu zinazomfanya awe miongoni mwa makinda waliopenya kwenye timu zao msimu huu.

Issa Abushehe (Coastal Union)

Kule Tanga wanamuita ‘Messi’ hii ni kutokana na machachari yake akiwa uwanjani kufananishwa na vile afanyavyo nyota wa Barcelona ya Hispania Lionel Messi.

Abushehe akiwa na umri wa miaka 20, tayari amepenya moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Juma Mgunda na kuweza kutoa burudani kwa mashabiki wake na Coastal Union.

Dickson Job (Mtibwa)

Huyu ni miongoni mwa wavulana wachache waliopewa kazi ya wanaume na akaifanya kwa ufasaha kabisa. ukimtizama akiwa uwanjani ni dhahiri utamfananisha na mabeki wengi wakongwe na wakubwa kwenye soka duniani lakini kumbe jamaa bado kinda wa miaka 20 tu.

Umakini, nidhamu na uwezo wake mkubwa wa kuzuia mashambulizi vinamfanya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Mtibwa Sugar kwa mwaka wa pili mfululizo sasa na ni moja ya mabeki walioitwa na kocha Ettiene Ndayiragije kuunda timu ya taifa ya Tanzania iliyocheza mchezo wa kirafiki na burundi Oktoba 11, ambapo Taifa Stars ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Jimson Stephen (Gwambina)

Huyu ni mshambuliaji mwenye miaka 21 wa kikosi cha Gwambina chenye masikani yake wilayani Misungwi Mwanza. Licha ya kuwepo kwa wakongwe wengi kama Paul Nonga, Jacob Masawe na Rajab Athuman kikosini hapo tena kwenye safu ya ushambuliaji ambayo naye anacheza hapo lakini bado ameweza kuonesha uwezo na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ambayo kocho wake mkuu ni Novatus Frugence na mkurugenzi wa ufundi ni kocha wa zamani wa Yanga Mwishi Zahera.

Kwlvin Nashon (JKT Tanzania)

Miongoni mwa viungo wa kati wanaocheza kibabe sana ni pamoja na kinda huyu mwenye umri wa miaka 20, kijana huyu ni zao la ile Serengeti Boys iliyokuwa na vijana wengi wenye uwezo na ikashiriki fainali za mataifa ya Africa kwa vijana nchini Gabon mwaka 2017.

Israel Patrick (KMC)

Miongoni mwa mabeki wa pembeni ambao Tanzania inajivunia kuwa nao kwa sasa ni pamoja na kinda huyu mwenye umri wa miaka 21, ambaye msimu uliokwisha alikua akikipiga Alliance ammbapo pia alikua nahodha wa timu hiyo.

Msimu huu amejiunga na vijana wa Kinondoni KMC na haikumchukua muda kuzoea mazingira.

Aboutwalib Mshery (Mtibwa Sugar)

Uwepo wa makipa wakongwe Shaban Kado na Said Nduda kikosi hapo hakujamfanya kinda Aboutwalib Mshery (21) kuonesha ubora wake na kuhakikisha anakua chaguo la kwanza la makocha wa timuy hiyo.

Tangu ligi imeanza msimu huu Mshery ameonekana kuwa imara zaidi langoni kwa kuokoa michomo kibao kwenye mechi zote za Ligi Kuu alizocheza msimu huu na kuwafanya Kado na Nduda kukaaa benchi.


Seif Bihaki (Coastal Union)

Mlinzi pembeni wa kulia wa timu ya Coastal Union umri wake ni miaka 20 na tayari amekwisha jihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kutokana na uwezo anaounyesha uwanjani.

Advertisement