AFCON itakavyoacha vilio Ligi Kuu England
Muktasari:
- Zaidi ya timu 17 zinaweza kuathiriwa huku takribani wachezaji 45 wakitarajiwa kuripoti katika timu zao za taifa.
London, England. Klabu za Ligi Kuu England zinajiandaa kwa pigo baada ya kufahamika kuwa wachezaji kadhaa wataondoka kwenda kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18.
Zaidi ya timu 17 zinaweza kuathiriwa huku takribani wachezaji 45 wakitarajiwa kuripoti katika timu zao za taifa.
Ingawa mashindano ya AFCON ni fahari kubwa kwa wachezaji barani Afrika, muda wake wa kufanyika katikati ya msimu umekuwa kikwazo kwa klabu za Ulaya, kama ilivyowahi kuigharimu Liverpool misimu ya nyuma.
Safari hii, Sunderland ndiyo watakaoumia zaidi baada ya kuthibitika kupoteza wachezaji saba wa kikosi cha kwanza.
Wachezaji hao ni Chemesdine Talbi (Morocco), Simon Adingra (Ivory Coast), Bertrand Traoré (Burkina Faso), Arthur Masuaku (DR Congo), Reinildo (Msumbiji), Noah Sadiki (DR Congo) na kiungo Habib Diarra (Senegal), ambaye ingawa amekuwa majeruhi tangu Septemba, bado ni sehemu ya kikosi muhimu.
Kwa klabu kama Manchester City, Marmoush na Aït-Nouri si wachezaji wa kuanzia mara kwa mara, lakini mchango wao hutumika kubadilisha mechi wanapoingia kama wabadilishaji mchezo.
Kwa upande mwingine, Arsenal, Chelsea na Leeds hazina sababu ya kuwa na wasiwasi kwani hakuna mchezaji wao atakayekwenda AFCON. Newcastle inaweza kuungana nao iwapo Yoane Wissa hatopata mwaliko kutokana na majeraha yake ya goti.
Kwa nini suala hili ni tete?
Kila baada ya miaka miwili, klabu za Ulaya hulazimika kukabiliana na pengo la wachezaji wao muhimu wanaokwenda kutumikia mataifa yao. Lakini kwa wachezaji, nafasi ya kuwakilisha nchi ni heshima ya juu.
Takwimu zinaonyesha kuwa AFCON ya 2023 ilifuatiliwa na karibu watu bilioni mbili, jambo linalothibitisha ukubwa wake.
Hata hivyo, presha kutoka kwenye klabu za wachezaji imekuwa ikileta sintofahamu mara kadhaa. Mfano ni André Onana, aliyekosa mechi ya kwanza ya Cameroon AFCON iliyopita baada ya kuchelewa kuwasili kutokana na shinikizo la Manchester United kumtumia dhidi ya Tottenham.
Wachezaji wengine kama Sébastien Haller wamewahi kukemea waziwazi kile wanachokiita “dhulma” au “kutotambua thamani” ya mashindano haya.
Akiwa Ajax mwaka 2021, Haller aliwahi kuulizwa kama angechagua klabu au taifa, na akajibu vikali:
“Swali hili linaonesha kutoiheshimu Afrika. Je, swali kama hili linaweza kuulizwa kwa mchezaji wa Ulaya kabla ya Euro? Bila shaka nitaenda AFCON. Ni heshima kubwa kuiwakilisha Ivory Coast.”
Orodha ya timu zitakazopoteza wachezaji
Sunderland – 7
Wolves – 5: Marshall Munetsi, Tawanda Chirewa (Zimbabwe), Emmanuel Agbadou (Ivory Coast), Tolu Arokodare (Nigeria), Jackson Tchatchoua (Cameroon)
Crystal Palace – 4: Ismaïla Sarr, Chadi Riad, Christiantus Uche na Cheick Doucouré
Nottingham Forest – 4: Ibrahima Sangaré, Willy Boly, Ola Aina na Taiwo Awoniyi
Manchester United – 3: Bryan Mbeumo, Amad Diallo, Noussair Mazraoui
Fulham – 3: Alex Iwobi, Calvin Bassey, Samuel Chukwueze
Burnley – 3: Axel Tuanzebe, Lyle Foster, Hannibal Mejbri
Everton – 2 hadi 3: Iliman Ndiaye, Idrissa Gueye; huenda akaongezeka Adam Aznou
Manchester City – 2: Omar Marmoush, Rayan Aït-Nouri
Brentford – 2: Dango Ouattara, Frank Onyeka
West Ham – 2: Aaron Wan-Bissaka, Yves Bissouma
Tottenham – 1 hadi 2: Pape Matar Sarr; huenda akaongezeka Bissouma
Liverpool – 1: Mohamed Salah
Aston Villa – 1: Evann Guessand
Brighton – 1: Carlos Baleba
Bournemouth – 1: Amine Adli
Newcastle – 0 hadi 1: huenda Yoane Wissa ataitwa na DR Congo
Arsenal – 0
Chelsea – 0
Leeds United – 0