Ahadi mbili za kocha mpya Simba

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha akizungumza na waadishi wa habari jana Novemba 28, 2023 jijini Dar es Salaam mara baada ya kutambulishwa rasmi na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Imani Kajula (kulia). Kushoto ni Khalid Tamim ambaye ni mkalimani. Picha na Loveness Bernard

Dar es Salaam. Wakati jana akitambulishwa rasmi kujiunga kwa mkataba wa miaka miwili, Kocha mpya wa Simba, Abdelhak Benchikha ametoa ahadi mbili kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo huku akiwaomba wampe ushirikiano katika muda wote atakaoinoa.

Benchikha ambaye kabla ya kujiunga na Simba aliiongoza USM Alger ya Algeria kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na ule la CAF Super Cup, alisema atahakikisha Simba inarudisha heshima ya mataji, pia atawafanya wachezaji wawajibike na kujitolea kwa ajili ya timu.

“Nina furaha kubwa kuwepo hapa. Tangu nilipoanza kuwasiliana na viongozi nilikuwa na shauku ya kuja. Jambo kubwa ambalo naomba ni mashabiki kutupa ushirikiano na naamini kupitia hilo tutafanikiwa pamoja.

“Kuna mambo mengi ambayo tayari nayajua na nimekuja na mikakati ambayo nitaifanyia kazi. Kuhusu wachezaji nitajua zaidi nikishaanza kazi na kuhusu mashindano ya ndani na kimataifa yote ni muhimu.  Mimi ni mpambanaji na nitapambana hadi tutafika.

“Mafanikio yatajengwa na Wanasimba wote hilo ndio muhimu zaidi. Kwa wachezaji sitaangalia majina bali anayefanya vizuri, kiwango cha mchezaji ndio kitafanya nimtumie,” alisema Benchikha ambaye anamudu vyema lugha ya Kiarabu.

Kocha huyo alisema sababu mbili zimechangia kwa kiasi kikubwa kumshawishi ajiunge na Simba ambazo ni mafanikio ambayo imekuwa ikiyapata katika mashindano ya kimataifa lakini ya pili ni maisha ya Tanzania ambako amesema kuna amani na utulivu na watu wake ni wakarimu.

Mtendaji mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema mchakato wa kumpata Benchikha haukuwa rahisi na wana imani kubwa kocha huyo kuifanya iwe tishio zaidi ndani na nje ya nchi.

“Mwalimu Benchikha atakuwepo kwa mkataba wa misimu miwili. Bodi ya Simba, menejimenti ya Simba imempa mwalimu uhuru wa kufanya kazi. Sisi ni moja ya klabu bora Afrika hatuwezi kufanya kazi kwa kumbana.”

“Walimu ambao kocha Benchikha amekuja nao ndio aliochukua nao ubingwa wa Shirikisho Afrika na Super Cup. Kocha Farid amefanya kazi na Benchikha kwa miaka 30 pamoja na kocha Kamal amefanya nae kazi kwa karibu,” alisema Kajula.

Kajula alisema Benchikha amekuja na kocha msaidizi Farid Zemiti na kocha wa viungo Kamal Boudjenane.


Jwaneng yawabadilishia uwanja

Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba umethibitisha kupokea barua kutoka CAF ya kujulishwa mabadiliko ya uwanja wa mechi inayofuata ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy kutoka ule wa taifa wa Gaborone kwenda Uwanja wa Obed Itani Chilume uliopo Francis Town nchini humo.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kwa sasa wanafanya tathmini ya utaratibu wa kuisafirisha timu kwenda Francis Town iwe kwa ndege ya kukodi au vinginevyo.

“Menejimenti itaamua na kutoa majibu. Kwa sasa tumepokea barua ya kubadilishwa kwa uwanja wa mechi  utakaotufanya tutembee kwa basi umbali wa kilomita zisizopungua 400 hivyo tungoje tutatolea uamuzi,” alisema Ally.