Anthony Taylor ataja sababu za kuachana na soka
Muktasari:
- Anthony Taylor alikuwa mwamuzi wa Ligi Kuu ya England (EPL) kwa misimu 16, akichezesha jumla ya mechi 432 za ligi hiyo.
Mwamuzi maarufu wa soka England, Anthony Taylor (47) ametangaza kustaafu kazi hiyo huku akisema mahitaji makubwa ya urefa ndio yamemfanya achukue uamuzi huo.
"Kuwa mwamuzi katika kiwango cha juu kabisa imekuwa heshima kubwa, lakini shinikizo ni kubwa sana na uchunguzi wa kila unachofanya haukosi.
"Kwa sasa ninaamini ni wakati mwafaka wa kuachia nafasi na kuanza ukurasa mpya katika maisha yangu ya kazi.
"Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wasaidizi wangu wawili, Gary na Adam, waamuzi wenzangu na kila mtu anayehusika na mchezo huu kwa msaada wao katika miaka yote iliyopita. Zaidi ya yote, ninawashukuru familia yangu na marafiki kwa kuniunga mkono bila kuyumba licha ya kujitolea na kujinyima ambako kazi hii imehitaji," amesema Taylor.
Mchezo wake wa mwisho kama mwamuzi ulikuwa wa Fainali za Kombe la Dunia 2026, ambao Hispania iliibuka na ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Ureno katika hatua ya 16 bora, Julai 6 mwaka huu.
Katika maisha yake ya uamuzi, Taylor alisimamia jumla ya mechi 839 katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.
Historia ya kumwaga kadi ndiyo inayomtambulisha zaidi Taylor kwani katika mechi hizo 839 alizochezesha, ametoa udadi ya kadi 3,105 ambapo kati ya hizo, kadi za njano ni 2953 na 152 ni nyekundu.
Pia anetoa idadi ya penalti 260.
Katika muda huo, alikuwa mwamuzi wa Ligi Kuu ya England (EPL) kwa misimu 16, akichezesha jumla ya mechi 432 za ligi hiyo.
Mbali na Ligi Kuu ya England, alichezesha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2024 ambayo Real Madrid iliifunga Borussia Dortmund, fainali za Kombe la FA mwaka 2017 na 2020, fainali ya Kombe la Ligi mwaka 2015, pamoja na fainali ya mchujo ya Championship mwaka 2018.
Sambamba na Kombe la Dunia la mwaka huu, Taylor pia alichezesha Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, pamoja na michuano ya Euro ya mwaka 2020 na 2024.