Arsenal, Man City zaangukia pua Ligi ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Manchester City ambayo ndio mabingwa watetezi wa michuano hii imetolewa na Real Madrid kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 4-4.

Licha ya kuingiza timu mbili katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, England imeshindwa kupenya katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Arsenal kutoka nchi hiyo ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya mchezo wa kwanza kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 kisha marudiano kule Ujerumani ikachapwa bao 1-0.

Manchester City ambayo ndio mabingwa watetezi wa michuano hii imetolewa na Real Madrid kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 4-4.
Miamba hii ilifikishana katika hatua ya penalti baada ya kutoshana nguvu katika dakika 90.

Mchezo wa mkondo wa kwanza kule Hispania ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3 kisha marudiano ukamalizika kwa sare ya 1-1.

Katika mechi hiyo bao pekee la Man City lilifungwa na Kevin de Bruyne dakika ya 76 huku lile la Madrid likifungwa na Rodrygo dakika ya 12.

Kwa matokeo haya rasmi sasa katika hatua ya nusu fainali Bayern Munich itakutana na Real Madrid huku Borussia Dortmund ikivaana na PSG, mechi zote za mkondo wa kwanza zikipigwa Aprili 30 kisha marudiano ni Mei 07.