Arsenal yafikia pazuri kumnasa Eze
Muktasari:
- Msimu uliopita, Eze aliibuka kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa Palace, akifunga mabao 14 na kutoa pasi 11 za mabao kwenye mechi 43 za mashindano yote aliyocheza.
London, England. Arsenal imefanikiwa kuvuruga mipango ya mahasimu wao wa kaskazini mwa London, Tottenham Hotspur, kwa kufikia makubaliano ya kumsajili staa wa Crystal Palace, Eberechi Eze, kwa dau la pauni milioni 60 (Sh200 bilioni).
Spurs ilikuwa kwenye mazungumzo na Palace kwa takriban siku 10 wakihangaika kukamilisha uhamisho huo kwa pauni milioni 55 pamoja na nyongeza, lakini mpango huo sasa umevunjwa na Arsenal iliyoingia kwa kasi baada ya Kai Havertz kuumia goti.
Kwa mujibu wa taarifa, Eze tayari alikuwa ameanza kuvutiwa na wazo la kujiunga na The Gunners tangu alipokutana na kocha Mikel Arteta pamoja na mkurugenzi wa michezo Andrea Berta mwezi uliopita, japokuwa ofa rasmi haikutolewa kwa wakati huo.
Inadaiwa Spurs walishakubaliana na Eze, na nyota huyo wa England mwenye umri wa miaka 27 alikuwa tayari kusaini, lakini Palace ilikataka kumwachia ili aendelee kupatikana kwenye mchezo wa Europa Conference League dhidi ya Fredrikstad ya Norway.
Hapo ndipo Arsenal walipoingia haraka na kuvuruga dili, hatua ambayo imeacha mashabiki wa Spurs wakikerwa, huku wengine wakikosoa namna klabu yao ilivyoshindwa kukamilisha usajili huo kama ilivyokuwa kwa Morgan Gibbs-White aliyekwenda Nottingham Forest mapema majira haya ya joto.
Spurs ilimfuata Eze baada ya James Maddison kupata majeraha ya goti yatakayomfanya kukosa sehemu kubwa ya msimu huu. Hata hivyo, Palace walikuwa bado wanahangaika kumpata mrithi wake, hali iliyochelewesha makubaliano.
Kwa sasa, Tottenham bado inamuwinda winga wa Manchester City, Savinho na Yoane Wissa wa Brentford, ingawa klabu zao hazipo tayari kuwauza.
Eze amekuwa akiendelea na mazoezi na Palace sambamba na beki Marc Guehi anayehusishwa na Liverpool.
Eze alianza kucheza kwenye akademi ya Arsenal akiwa kijana mdogo na baada ya hapo alijiunga na akademi za Fulham, Reading na Millwall, kisha akatua Queens Park Rangers (QPR) mwaka 2016 ambapo kipaji chake kilianza kung’aa.
Mwaka 2020, Crystal Palace ilimnunua kutokea QPR kwa dau la pauni milioni 17.5 (Sh56 bilioni) na tangu hapo amekuwa nguzo muhimu ya kikosi cha Palace.
Kwenye timu ya taifa, Eze aliitwa England kwa mara ya kwanza mwaka 2023 na amekuwa sehemu ya kikosi cha Thomas Tuchel.
Msimu uliopita wa 2024/25, Eze aliibuka kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa Palace, akifunga mabao 14 na kutoa pasi 11 za mabao kwenye mechi 43 za mashindano yote aliyocheza, kiwango kilichovutia vilabu vikubwa vya Premier League kuhitahi huduma yake.