Arteta: Arsenal tunatakiwa kuamka upya

Muktasari:

  • Arsenal ilikuwa na nafasi kubwa ya kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England wikiendi iliyopita, lakini ikajikuta inalala kwa mabao 2-0 dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa Emirates.

London, England, Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema wachezaji wake wanatakiwa kuamka haraka kama wanataka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, msimu huu.

Arsenal ilikuwa na nafasi kubwa ya kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu England wikiendi iliyopita, lakini ikajikuta inalala kwa mabao 2-0 dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa Emirates.

Arsenal ilikosa nafasi nyingi kipindi cha kwanza, lakini makosa ya kipindi cha pili yakaigharimu na kuipa Villa ushindi huo muhimu msimu huu.

Kocha wa Villa, Unai Emery ambaye aliwahi kuifundisha Arsenal alimaliza ubabe wa timu hiyo ya London wa kutopoteza michezo 11 mfululizo.

"Tulikuwa na nafasi nzuri ya kushinda mchezo huu, timu ilionyesha kila kitu kwenye mchezo dhidi ya Bayern lakini tukashindwa, lakini hali hiyo imetokea tena kwenye mchezo dhidi ya Villa, matokeo yamekuwa yaleyale na kama tunataka kufanya vizuri lazima tubadilishe aina yetu ya kucheza.

"Kwa michezo iliyobaki tunachotakiwa ni kubadilika na kuonyesha mapambano yetu kwa nguvu kubwa, hakuna jambo lingine zaidi ya sisi wenyewe kubadilika.

"Tulijua kuwa hali hii inaweza kutokea, jambo la msingi tunalotakiwa kufanya ni kubadilika na kuweka kasi upya kwenye timu yetu.

"Kama tukipoteza mchezo mmoja tunakosa matumaini basi hatustahili kuwa timu bora ya soka, timu zote zinazowania ubingwa wa England Arsenal, Liverpool na Manchester City zinapoteza lakini zinaamka upya," alisema Arteta.