Ishu ya penalti ya Arsenal yazua mjadala

London. Refa raia wa Sweden, Glenn Nyberg aliyechezesha mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Arsenal na Bayern Munich juzi, amejikuta akipokea mashambulizi kutoka pande mbalimbali akituhumiwa kuchezesha vibaya mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Emirates.

Kuacha kuchukua hatua katika matukio kadhaa ambayo pengine yangeweza kuamua matokeo ya mchezo huo, kumefanya baadhi wahoji uwezo wa Nyberg ambaye pia ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) kuchezesha mechi za michezo ya Olimpiki itakayifanyika Julai 26 hadi Agosti 11 huko Ufaransa.

Miongoni mwa matukio ambayo yalishangaza wengi ni lile la beki wa Arsenal, Gabriel Magalhaes kushika mpira kwa mikono baada ya kuwa umeanzishwa na kipa David Raya lakini refa Nyberg hakuizawadia pigo la penalti Bayern Munich jambo ambalo limeonekana kuwakera kocha wa timu hiyo, Thomas Tuchel na wachezaji wake waliotamka hadharani kuwa refa alikosea kutoiadhibu Arsenal.

"Tulitakiwa kupata penalti ya wazi pindi refa alipopuliza filimbi. Kipa alipasia mpira na Gabriel aliushika na mikono yake. Ni penalti ya wazi kuwahi kuiona," alisema Kane kwa hasira.

Mshambuliaji Thomas Muller aliutafsiri uamuzi huo wa refa Nyberg kama wa hatari zaidi kuwahi kuuona katika mchezo wa soka.

"Refa yuko pale kusimamia sheria. Hata kama hauridhisha na sheria, sidhani sheria inasema hivyo. Sawa kama haikuwa kwa makusudi ndio uweke mpira chini kwa ajili ya golikiki? Sijui inasema nini lakini nadhani ilikuwa ni penalti ya wazi," alisema Muller.

Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel alisema kuwa alishangaa kuona timu yake imenyimwa mkwaju wa penalti kutokana na kosa la Magalhaes.

"kwangu mimi na sisi wote, refa alifanya kosa kubwa kwa kutotoa penalti. Najua ni hali ya kuchanganya lakini waliweka mpira chini, akapuliza filimbi, akatoa mpira na beki (Gabriel) akauchukua kwa mikono yake.

"Kinachotupa hasira zaidi ni ufafanuzi wa ndani ya uwanja. Aliwaambia wachezaji wetu kwamba ni kosa la kitoto na hawezi kutoa penalti ya namna hiyo katika robo fainali," alisema Tuchel.

Lakini wakati Bayern wakililia penalti hiyo, beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand yeye amemshutumu refa Nyberg kwa kushindwa kuizawadia penalti, Arsenal kwa tukio la kipa wa Bayern Munich, Manuel Neur kugongana na winga Bukayo Saka,akiamini kwamba Saka hakujingesha miguuni mwa kipa huyo kaka ambavyo refa alitafsiri.

"Kwa vipi ile (penalti) haikutolewa? Siamini kama haikutoleo licha ya uwepo wa VAR. Saka alikuwa ni mchezaji hatari zaidi kwa Arsenal anakiambia kuelekea kwenye lango. Ile nio penalti. Nilikuwa uwanjani siamini kuhusu hili. Ninatembea kila kona nikiwa nimwekea mikono kichwani," alisema Ferdinand.

Lakini ukiondoa matukio hayo mawili, refa Nyberg pia analalamikiwa kwa kushindwa kumuonyesha kadi nyekundu Harry Kane ambaye alionekana kumpiga kiwiko, Gabriel Magalhaes ambapo mwamuzi huyo kutoka Sweden aliamua kutoa kadi ya njano badala ya nyekundu.