Prime
AS FAR yaitangazia vita Yanga CAF
Muktasari:
- Yanga ipo kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na timu za Al Ahly ya Misri, AS FAR ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria.
Rabat, Morocco. Kocha Mkuu wa AS FAR ya Morocco, Alexandre Dos Santos amesema kuwa wanafanya maandalizi makubwa kwa ajili ya mechi yao ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Yanga itakayochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar, kati ya Novemba 21 hadi 23 mwaka huu.
Santos amesema kuwa sababu zinazowalazimisha kujipanga vilivyo kwa ajili ya mechi hiyo ni ubora na uzoefu mkubwa wa Yanga pamoja na lengo waliloweka la kuhakikisha wanapata ushindi katika michezo yote ya kundi hilo.
"Tunahitaji maandalizi ya dhati kabisa. Mechi mbili za mwanzo zinakuja haraka, na tutachukulia kama mashindano madogo ya mechi sita ambapo kila mchezo ni muhimu zaidi.
"Mechi ya kwanza ni dhidi ya Yanga. Tutaiandaa vyema timu iweze kwenda Tanzania na kujaribu kushinda ambacho ndio kitu cha msingi. Lengo letu ni kuikabili kila mechi, kushinda na kucheza vyema kuliko wapinzani," amesema Dos Santos.
Kocha huyo amesema kuwa wao AS FAR wanafahamu wapo katika kundi gumu hivyo wanapaswa kufanya kazi ya ziada ili waweze kutinga hatua ya robo fainali.
"Kucheza na Al Ahly, Young Africans na Kabylie zitakuwa mechi sita za kiwango cha juu zitakazotuwezesha kujituma zaidi.
"Kundi letu ni la ushindani, lina nguvu sana. Ninaamini kila timu ina uwezekano wa kuwa na Ligi bora ya Mabingwa. Kila mtu anataka kusonga mbele na matarajio kwa kundi kama letu ni makubwa kwa wafuasi wetu kwa sababu ni changamoto kubwa," amesema Santos.
Mtazamo wa Dos Santos umeungwa mkono na kipa wa timu hiyo, Ahmed Reda Tagnaouti.
""Kama mnavyojua, kundi letu lina klabu zenye uzoefu mkubwa wa Ligi ya Mabingwa.
"Tumejipanga vyema kwa ajili ya programu hii na tunatumai kusonga mbele kwa raundi inayofuata. Kuhusu nafasi yetu itakuja mechi baada ya mechi. Muda ukifika kwa kila mchezo, tutakuwa makini kabisa," alisema Tagnaouti.