Prime
Rekodi ya Yanga, mlima mrefu Ligi Kuu
Muktasari:
- Yanga imeibuka na ushindi katika mechi tatu kati ya nne ilizocheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu.
Dar es Salaam. Ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya KMC jana kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam, umeifanya Yanga ipande kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha pointi 10.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalipachikwa na Andy Boyeli aliyefunga mawili huku Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli kila mmoja akipachika bao moja.
Wakati Yanga ikifurahia kuwepo kileleni mwa msimamo wa ligi, timu hiyo imeweka rekodi moya ya kibabe kwenye ligi ambayo huenda ikawa ngumu kufikiwa na timu nyingine.
Rekodi hiyo ni kutimiza mwaka mzima bila kupoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu.
Ushindi wa jana dhidi ya KMC, umeifanya Yanga kufikisha siku 368 ikiwa haijaonja ladha ya kupoteza mechi ya ligi tangu Novemba 7, 2024 ilipofungwa mabao 3-1 na Tabora United katika Uwanja wa Azam Complex.
Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja na siku tatu ambacho Yanga imefikisha bila kupoteza mechi ya Ligi Kuu, imeingia uwanjani katika mechi 24 za Ligi Kuu Tanzania Bara, ikipata ushindi mara 22 na imetoka sare katika michezo miwili tu.
Ushindi katika mechi 22 na sare mbili katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ilipopoteza dhidi ya Tabora United ambayo sasa inaitwa TRA United, mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi Kuu wamkusanya idadi ya pointi 68 ambapo 66 zimetokana na ushindi na mbili kwa sare.
Makali ya safau ya ushambuliaji yameonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa Yanga kutamba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara katika kipindi cha miezi 12 mfululizo kwani imefunga mabao 77 ikiwa ni wastani wa mabao 3.2 kwa mechi.
Haijaishia katika safu ya ushambuliaji tu kwani Yanga imekuwa bora katika safu ya ulinzi ambapo katika kipindi hicho imeruhusu nyavu zake kutikiwa mara sita tu ikiwa ni wastani wa bao 0.3.
KMC imeonekana kuchangia idadi kubwa ya mabao ya Yanga ndani ya kipindi hicho kwani yenyewe pekee imefungwa mabao 10.