Aussems: Siogopi kufukuzwa Simba SC

Muktasari:

  • Kocha huyo kutoka Ubelgiji na aliyeifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na kutetea taji la Ligi Kuu Bara, aliliambia Mwanaspoti kila kitu kinachoendelea juu yake anakijua, ila hana wasiwasi kwa vile anatimiza majukumu yake vyema.

KUMBE zile kelele za baadhi ya mashabiki wa Simba za kutaka Kocha Patrick Aussems atimuliwe na huku kukiwa na taarifa za chinichini kwamba mabosi wa klabu hiyo wameanza kumjadili kabla ya kumuonyesha mlango wa kutokea, zimemfikia mwenyewe buana!
Aussems aliyeishuhudia timu yao usiku wa juzi ikicharazwa mabao 2-1 na KMC katika mchezo wa kirafiki, amesema amekuwa akisikia taarifa hizo za kutimuliwa kwake na kusema yeye hana presha na wala hahofii.
Kocha huyo kutoka Ubelgiji na aliyeifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na kutetea taji la Ligi Kuu Bara, aliliambia Mwanaspoti kila kitu kinachoendelea juu yake anakijua, ila hana wasiwasi kwa vile anatimiza majukumu yake vyema.
Aussema alisema pia anakiamini kikosi alichonacho kina uwezo wa kufanya vizuri zaidi kwenye Ligi Kuu kwa sababu mechi za ligi hiyo bado nyingi na hajui presha zilizoibuka sasa zinatoka wapi wakati timu haijafanya vibaya na inaoongoza msimamo mpaka sasa.
“Lazima ukutane na changamoto katika mahala kokote ambapo unafanya kazi na hilo nadhani ndio lipo wakati huu, lakini kama haitoshi kila kocha anaajiriwa ili afukuzwe kwa maana hiyo sina hofu yoyote na ninaendelea na majukumu yangu,” alisema Aussems na kuongeza kwa timu aliyonao anaamini inaweza kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita hata kama wametolewa CAF.
“Hata kama itatokea kutimuliwa, sitakuwa wa kwanza kwa vile katika soka hakuna kocha wa kudumu, ila bado naamini Simba haina sababu ya kuwa na presha kwa sasa, tuna kikosi imara nasi tunatekeleza majukumu yetu kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki,” alisema Aussems.
Licha ya kocha huyo kuonekana kutokuwa na presha, lakini ana kibarua kigumu kwa kuhakikisha mechi yao ijayo dhidi ya Ruvu Shooting wanashinda ili kujiweka salama, vinginevyo kama atapata matokeo mabaya huenda ikawa kazi nzito kwake kutokana na Ruvu msimu huu kuonekana tishio.
Wazee wa Kupapasa hao wameshazipiga timu za Yanga, Azam na KMC ambazo ziliwakilisha nchi kwenye mechi za kimataifa msimu huu sambamba na Simba, lakini pia kocha huyo atakuwa na kazi nzito mbele ya watani wao, Yanga, Januari 4 mwakani.
Mechi za watani mara nyingi hutumika kama mtego kwa makocha, hivyo ni wazi Aussems kama atasalia mpaka muda wa mchezo huo ni lazima awe amejipanga kwelikweli.

WASIKIE WADAU
Mchambuzi maarufu wa soka nchini, Alex Kashasha, alisema uamuzi wa Simba kutaka kumtimua Aussems, hauungi mkono kwani anaamini matatizo ya timu hiyo si katika eneo la benchi la ufundi.
“Hii taarifa ya Simba kuachana na Aussems nimeanza kuisikia tangu walipopoteza dhidi ya Mwadui na katika sare dhidi ya Tanzania Prisons, lakini ukiangalia timu ina matatizo mengi hata viwango kama vya wale Wabrazili watatu ni vya kawaida hata wachezaji wa ndani wapo wenye uwezo zaidi yao.”
“Hata kama Simba inataka matokeo mazuri, lakini sioni kama kutimuliwa kwa Aussems ni suluhu, halafu hii ni ligi kila timu inajipanga kusaka matokeo mazuri, hiki sio kipindi kizuri cha kutimua makocha, ila hayo ni maamuzi yao,” alisema Kashasha.
Naye mchambuzi na mwandishi wa habari za michezo, Edo Kumwembe, alisema mtazamo wake anadhani Aussems bado ni kocha sahihi kutokana timu hiyo inaongoza katika msimamo wa ligi na inacheza soka la kushambulia tofauti na hapo wanamtoa kwa sababu zao ambao wanazijua wao.
“Kama Simba wangeachana na Aussems, siku chache baada ya kutolewa na UD Songo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ningewaelewa labda walitaka wafike mbali, lakini kwa sasa sioni sahihi,” alisema Kumwembe aliyeungwa mkono na nyota wa zamani wa klabu hiyo Ulimboka Mwakingwe.
Mwakingwe alisema mpaka leo huwa hajui kwanini kila mara makocha wazuri na wanaofanya vizuri huwa wanatimuliwa, huku akisisitiza Aussems ni kocha anayeweza kuwapa mafanikio kama watamuamini na kushirikiana naye, kwani mpaka sasa hajafanya vibaya.
Rekodi zinaonyesha tangu ajiunge na Simba mwaka uliopita, Aussems ameiongoza timu huiyo kwenye mechi 72 za kimashindano zikiwamo 14 za Ligi ya Mabingwa Afrika ambako ilishinda mechi sita na kutoka sare tatu na kupoteza tano, akiifikisha pia robo fainali msimu uliopita.
Katika Ligi Kuu Aussems ameiongoza Simba kwenye mechi 47 za misimu miwili na kushinda 36, huku wakiyoka sare mechi saba na kupoteza minne, mbali na kutwaa Ngao ya Jamii mara mbili kwa kuzifunga Mtibwa Sugar na Azam FC, lakini akipoteza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Mashujaa ya Kigoma kadhalika kuiwezesha Simba kumaliza ya tatu katika Kombe la SportPesa.
Katika michuano hiyo ilicheza mechi tatu na kushinda miwili na kupoteza mmoja. Kwenye Kombe la Mapinduzi ilimaliza ya pili  ikifungwa na Azam na katika mechi tano ilishinda tatu na kutoka sare moja na kupoteza mechi ya fainali.