Azam sasa yaanza kuitisha Simba

Muktasari:

  • Kitendo cha kutoshiriki mashindano hayo kitaifanya Simba isiwe na uwezekano wa kuvuna kitita cha Dola 700,000 (shilingi 1.8 bilioni) ambacho Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), hutoa kwa kila timu inayotinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambacho kinaongezeka zaidi ikiwa timu husika inafika hatua za juu za mashindano hayo.

Dar es Salaam. Hofu ya kupoteza nafasi ya kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita, imeuingia uongozi wa Simba ambao sasa umepanga kuelekeza nguvu zote katika mechi 10 zilizobaki ili imalize juu katika nafasi mbili, ikiwa na maana ni lazima iishushe Azam FC.

Kitendo cha kutoshiriki mashindano hayo kitaifanya Simba isiwe na uwezekano wa kuvuna kitita cha Dola 700,000 (shilingi 1.8 bilioni) ambacho Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), hutoa kwa kila timu inayotinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambacho kinaongezeka zaidi ikiwa timu husika inafika hatua za juu za mashindano hayo.

Kwa sasa Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 46, ikizidiwa na Yanga inayoongoza ikiwa na pointi 55, huku Azam FC ikishika nafasi ya pili na pointi zake 50, ikiwa ndiyo timu inayotishia nafasi ya Simba.

Tanzania msimu ujao itawakilishwa na timu mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo kwa mujibu wa kanuni ni mbili zitakazoshika nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi mwishoni mwa msimu huu, jambo lililoishtua Simba ambayo inaona inaweza kujikuta ikiangukia katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Mmoja wa vigogo wa Simba aliliambia gazeti hili kuwa katika kikao ambacho mwekezaji wa timu hiyo, Mohamed Dewji 'Mo' alikutana na bodi ya wakurugenzi ya Simba chini ya Salim Abdallah 'Try Again' miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuhakikisha Simba inapata ushindi katika mechi zote 10 ilizobakiza ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa na ikishindikana imalize katika nafasi ya pili ambayo kwa sasa inashikiliwa na Azam.

"Uongozi na mwekezaji tumekutana na kujadiliana kwa muda mrefu juu ya hatima ya timu katika mechi 10 zilizobakia maana matumaini pekee yaliyopo sasa ni kwenye ligi tu ambako nako hatuko katika nafasi nzuri.

"Tunafahamu kwamba ushindani ni mkubwa hivyo hata tukikosa ubingwa basi tumalize katika nafasi ya pili, tuweze kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Ligi ya Mabingwa ni mashindano ambayo yamechangia kuipa Simba ukubwa na thamani Afrika na duniani hivyo kama tukikosekana litakuwa ni pigo kubwa kwetu.

"Na kikao hakijahusisha viongozi na mwekezaji pekee bali pia benchi la ufundi chini ya kocha Abdelhak Benchikha ambaye alizungumza mambo yanayohusu viwango vya wachezaji wake, lengo likiwa ni kujua wanakabiliwa na changamoto gani ili ziweze kufanyiwa kazi," kilifichua chanzo hicho, lakini pia tumejadili kidogo kuhusu mchezo ujao wa dabi kufahamu tunatakiwa kufanya nini.

Michezo 10 ambayo Simba imebakiza kwenye Ligi Kuu ni dhidi ya Yanga, Dodoma Jiji, Mtibwa, Namungo, Tabora United, Azam, Kagera Sugar, Geita Gold, KMC na JKT Tanzania.

Hata hivyo, Azam inaonekana kuwa tishio kwa Simba msimu huu ikiwa imeizidi kwenye vitu vingi muhimu kwenye msimamo wa ligi. Timu tatu za juu kwenye msimamo, Yanga, Simba na Azam zimepoteza michezo miwili kila moja, lakini Azam imeizidi Simba kwenye mabao ya kufunga ikiwa imefunga 49 huku Simba ikifunga 40, lakini mabao ya kufungwa Azam imefungwa 16 Simba ikifungwa 19 pamoja na kwamba ina mchezo mmoja mkononi.

Hii inaonyesha kuwa kama Simba ambayo imeshacheza michezo 20 na Azam 22 haitachanga karata zake vizuri kwenye michezo kumi iliyobaki basi itashiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao.

Kwenye chati ya ufungaji, Feisal Salum wa Azam anashika nafasi ya pili akiwa na mabao 13, huku mchezaji wa Simba aliyepo kwenye chati hiyo ni Jean Baleke anashika nafasi ya tisa ambaye alishaondoka akiwa na mabao nane.

Kwenye chati ya pasi zilizozaa mabao yaani asisti, Azam ina wachezaji wawili Feisal sita, Lusajo Mwaikenda tano kwenye kumi bora huku Simba ikiwa na mmoja tu Clatous Chama mwenye pasi tano.