Azam FC mwendo mdundo ASFC

TIMU ya Azam imefuzu robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 3-0, na kuweka rekodi ya kufika hatua hiyo kwa kila msimu tangu mashindano hayo yaliporejea upya msimu wa 2015-2016.

Mabao ya Azam katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex yalifungwa na Abdul Suleiman 'Sopu', Ayoub Lyanga na Feisal Salum 'Fei Toto'.

Rekodi zinaonyesha tangu 2015, michuano hiyo iliyofahamika kama Kombe la FA kurejeshwa ikiwa na jina jipya la ASFC, Azam haijawahi kutolewa hatua ya 16 bora kwani katika michezo yake tisa iliyocheza ilishinda yote na kutinga robo fainali.

Februari 29, 2016 iliichapa Panone mabao 2-1 ikiwa ni msimu iliyofika hadi fainali na kupoteza mbele ya Yanga kwa 3-1 na Februari 24, 2017 ilitinga tena na kuiondosha Mtibwa Sugar bao 1-0 kisha Februari 24, 2018 iliifunga KMC kwa mabao 3-1.

Msimu wa 2018/19 iliichapa Rhino Rangers 3-0 Februari 25, 2019 ukiwa ndio msimu iliyobeba ubingwa kwa kuinyoa Lipuli ya Iringa bao 1-0 katika fainali na msimu wa 2020/2021 ikakutana na Ihefu na kuiondoa kwa penalti 5-4 baada ya suluhu ndani ya dakika 90.

Azam iliendeleza moto wake tena ambapo Aprili 29, 2021 iliifunga Polisi Tanzania mabao 2-1 na Februari 12, 2022 ikafuzu kwa kuichapa Baga Friends 6-0 japo iliishia nusu fainali kwa kutolewa na Coastal Union kwa penalti 6-5 baada ya suluhu dakika zote 120.

Machi 5, 2023 katika hatua ya robo fainali, Azam iliitoa timu ya Mapinduzi ya Mwanza iliyokuwa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kwa kuifunga mabao 2-0, yaliyofungwa na Nathaniel Chilambo na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Cyprian Kachwele.

Akizungumzia hilo kocha wa kikosi hicho, Youssouph Dabo alisema ni jambo jema kwao kufuzu hatua hiyo muhimu kwani moja ya malengo yao makubwa msimu huu ni kuhakikisha wanatwaa taji hilo kutokana na ubora, upana wa wachezaji waliopo nao.